JAJI
Mkuu, Mohammed Chande Othman, amesema Mahakama Maalumu ya Uhujumu
Uchumi na Ufisadi itaamua kesi kwa muda usiozidi miezi tisa na kwamba
itaanza na majaji 14.
Aidha,
wameandaa kozi maalumu kwa majaji 14 watakaofanya kazi katika mahakama
hiyo itakayoanza Julai 11 hadi 15, mwaka huu, kwenye Chuo cha Mahakama
Lushoto mkoani Tanga, ili kupeana mwongozo juu ya uendeshaji wa mahakama
hiyo.
Jaji
Mkuu alisema, kesi zitakazoendeshwa katika mahakama hiyo ni zile ambazo
upelelezi wake umekamilika ili uamuzi utolewe mapema. Kwa mujibu wa
Jaji Mkuu, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupambana na uhalifu
huo.
Aliyasema
hayo jana wakati alipotembelea Maonesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara
ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere
vilivyopo katika Barabara ya Kilwa, ambayo alisema yamezidi kuwa bora
kuliko miaka mingine.
Alisema
baada ya sheria hiyo ya uhujumu uchumi kupitishwa na Bunge, imekuwa na
marekebisho mengi na kuboreshwa kwa kiasi kikubwa.
Jaji
Mkuu alisema pia, hatua inayofuata ni Rais kutoa idhini ya sheria hiyo
na baadaye kupitishwa kwa kutangazwa katika Gazeti la Serikali ili ianze
kutumika.
Alieleza
kuwa baada ya kutangazwa katika Gazeti hilo la Serikali, Jaji anatakiwa
kutunga kanuni mbalimbali, mojawapo ikiwa ya kulinda mashahidi kutokana
na kuwa sheria hiyo inahusu makosa makubwa na hatari ya ugaidi, rushwa
na uhujumu uchumi.
“Tuko
mbioni kutunga kanuni hizo na kuhakikisha mashahidi wanalindwa. Jengo
la mahakama hii litakuwa katika Chuo cha Sheria karibu na Mlimani City
na tayari tumepeleka wasajili watendaji,” alisema.
Mwishoni
mwa wiki, Jaji Mkuu huyo alisema kuwa majengo ya mahakama hiyo
yatakabidhiwa leo. Kutokana na maelezo yake, Mahakama iko tayari
kuendesha divisheni hiyo, baada ya kukabidhiwa majengo hayo.
Alisema
wataanza kutoa semina kwa majaji na watumishi wengine wa mahakama hiyo
juu ya namna divisheni hiyo itakavyoendesha shughuli zake.
Aidha, aliweka wazi kuwa hadi sasa hakuna kesi hata moja iliyokwishatambuliwa kwamba itashughulikiwa na mahakama hiyo.
0 comments:
Post a Comment