WAHALIFU
wa mtandao pamoja na wasambazaji wa picha za utupu na ngono,
wasambazaji wa taarifa za uwongo, za kibaguzi na matusi na watu wengine
ambao wanafanya udanganyifu unaohusiana na kompyuta wametungiwa sheria
kali ambayo itawafanya kwenda jela hadi miaka 10 au kulipa faini
isiyopungua Sh milioni 50.
Miongoni
mwa miswada ya sheria utakaowasilishwa bungeni na Serikali wiki hii
mjini hapa, ni Sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 ambayo
imeainisha makosa mbalimbali yanayofanywa na wananchi katika kipindi
hiki ambacho matumizi ya mtandao wa kompyuta yameongezeka.
Baadhi
ya makosa yaliyoainishwa kwenye sheria hiyo ni kughushi kunakohusiana
na masuala ya kompyuta, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, ponografia
za watoto, picha za utupu, matusi na ngono, makosa yanayohusiana na
utambuzi, uwongo, ubaguzi, matumizi ya kibaguzi, mauaji ya kimbari na
unyanyasaji kupitia mtandao wa kompyuta.
Katika
sheria hiyo, mtu atakayesambaza ponografia ya watoto kupitia mtandao wa
kompyuta atawajibika kulipa faini isiyopungua Sh milioni 50 au mara
tatu ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria au kifungo kisichopungua
miaka saba jela au vyote kwa pamoja.
Mkosaji
pia ataamriwa kumlipa mwathirika fidia. Kwa upande wa kusambaza picha
za ngono, matusi, uasherati atalipa faini isiyopungua Sh milioni 30 au
kwenda jela miaka 10 au vyote.
Lakini
mtu atakayesambaza picha za utupu atalipa faini isiyopungua Sh milioni
20 au kwenda jela miaka saba au kutumikia adhabu zote kwa pamoja.
Pia
kweye muswada huo mtu ambaye atatoa taarifa, data au maelezo kwa njia
ya picha, maandishi, alama au aina nyingine yoyote zikiwa ni za uongo
akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh milioni 3 au kutumikia
kifungo jela kisichopungua miezi sita au vyote.
Kwa
upande wa ubaguzi, sheria hiyo inakataza mtu kutumia mtandao wa
kompyuta kutozalisha vitu vya kibaguzi kwa madhumuni ya kuvisambaza na
iwapo atatiwa hatiani atalazimika kulipa faini ya Sh milioni tatu au
kifungo cha mwaka mmoja jela.
Pia
mtu akimdhihaki mtu mwingine kwa kupitia mfumo wa kompyuta kwa mwelekeo
wa ubaguzi wa rangi, kabila, asili, utaifa au dini fulani akitiwa
hatiani atatozwa na Mahakama faini ya Sh milioni tatu au kifungo cha
mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja.
Pia
sheria hiyo inakataza mtu kuchapisha au kusababisha kuchapishwa vitu
vinavyochochea au kuhalalisha matendo yanayopelekea mauaji ya kimbari na
makosa dhidi ya binadamu kwa kupitia mtandao wa kompyuta.
Mtu
atakayefanya hivyo atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika
kulipa faini isiyopungua Sh milioni 10 au kutumikia kifungo
kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Pia
muswada huo wa sheria unakataza mtu kutoanzisha usambazaji wa taarifa
zinazotumwa bila ridhaa na ukitiwa hatiani utatozwa faini ya Sh milioni 3
au mara tatu ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria au kutumikia
kifungo kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
0 comments:
Post a Comment