UDOM wagoma
WANAFUNZI 84 WA PROGRAMU MAALUMU YA DIPLOMA YA UALIMU UDOM MBARONI KWA KUHAMASISHA MAANDAMANO MKOANI DODOMA
Baadhi ya Wanafunzi 84 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakiwa chini ya ulinzi kwa tuhuma za kuhamasisha uvunjifu wa amani Chuoni hapo na kufanya maandamano haramu kutoka Chuoni kuelekea katika Ofisi mbalimbali za viongozi wa Serikali zilizopo mjini Dodoma leo.
Dodoma.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma inawashikilia wanafunzi 84 wa chuo Kikuu UDOM kwa tuhuma za kuhamasisha uvunjifu wa amani Chuoni na kufanya maandamano haramu kutoka Chuoni kuelekea katika Ofisi mbalimbali za viongozi wa Serikali zilizopo Dodoma Mjini leo tarehe 14.01.2015 majira ya 05:30hrs.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – (SACP) ameeleza kuwa chanzo cha wananfunzi hao wa programu maalum ya Diploma ya Ualimu kufanya uhalifu huo ni kikao walichofanya wananfunzi hao tarehe 13.01.201 wakidai kuongezewa posho ya chakula na kwamba hata kiasi ambacho wanapewa wamechelewa kupewa.
Hata hivyo uongozi wa Chuo uliwaeleza kuwa wenye mamlaka ya kuzungumzia swala la kuongezewa posho ni Bodi ya Mikopo na siyo chuo. Hivyo walitakiwa kufuata taratibu za kuwasilisha madai yao. Pia walielezwa kuwa hundi kwa ajili ya fedha za posho zao zimeshasainiwa na kuwasilishwa Benki ili waweze kuanza kupewa posho zao.
Baadhi ya Wanafunzi 84 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakiwa kwenye gari ya polisi baada ya kutiwa mbaroni…
Viongozi waliohamasisha uvunjifu huo wa sheria baadi wamekamatwa na baadhi wanaendelea kutafutwa ili nao waweze kuchukuliwa hatua stahiki. Ushahidi uliokusanywa unaonyesha jinsi viongozi hao wameshiriki kuhamasisha kupitia vikao rasmi na visivyo rasmi, katika vikundi, kupita katika mabweni na kutuma sms.
Kamanda MISIME ametoa wito kwa Wanafunzi hao kutumia taratibu zilizowekwa na Serikali na Chuo kuwasilisha malalamiko yao ngazi kwa ngazi na siyo kufanya vitendo vya kuvunja sheria ambavyo vitawasababishia kukamatwa. Endapo watafanya hivyo wasije kulaumu mtu kwani hatua zitachukuliwa kulingana na Sheria inavyoelekeza ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
0 comments:
Post a Comment