Friday, 10 April 2026

MWANAMKE CHUMA MAENDELEO GROUP YATOA MSAADA KWA WAFUNGWA WANAWAKE GEREZA LA KAHAMA 'TAMASHA KUBWA LA MWANAMKE CHUMA 2026 NI KESHO'


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Katika kuendeleza jitihada za kijamii na kuonesha mshikamano wa dhati kwa wanawake wenzao, Kikundi cha wanawake maarufu kinachojulikana kama Mwanamke Chuma Maendeleo Group kimetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wafungwa wanawake katika Gereza la Kahama Mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea kilele cha Tamasha la Mwanamke Chuma 2026 litakalofanyika Aprili 11, 2026 Mjini Kahama.

Msaada huo uliokabidhiwa unajumuisha mahitaji muhimu ya kila siku kama vile sabuni, taulo za kike, dawa za meno, nguo, lishe ya watoto, kandambili (ndala) pamoja na mafuta ya kujipaka ikiwa ni hatua ya kupunguza changamoto ndogondogo zinazowakabili wafungwa hao na wakati huo huo kuwapa faraja ya kihisia.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo Ijumaa Aprili 10,2026 , Mwenyekiti wa Mwanamke Chuma Maendeleo Group, Bi. Neema Moshi, amesema kuwa hatua hiyo inatokana na dhamira ya kundi hilo kuhakikisha kuwa wanawake wote, bila kujali walipo, wanapata faraja na kuendelea kuamini katika thamani yao.
Neema Moshi akizungumza

“Tukiwa na kaulimbiu ya ‘Nguvu ya Ujasiri’, tumeona ni muhimu kuwafikia wanawake wenzetu waliopo gerezani ili kuwatia moyo na kuwaonesha kuwa hawako peke yao. Tumekuja kama wawakilishi wa wanachama wetu kuwapa ujumbe wa matumaini na mshikamano,” amesema Bi. Moshi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Tamasha la Mwanamke Chuma 2026 ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Redio cha Gold FM, Bi. Neema Mghen, amesisitiza kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kuhamasisha matumaini na ujasiri kwa wanawake waliopo gerezani.
Neema Mghen akizungumza

“Tumekuja kuwaambia kuwa walipo si mwisho wa maisha yao. Ndoto zao bado zina thamani na wana nafasi ya kuanza upya. Wanapaswa kuendelea kuwa na ujasiri na kujiandaa kuwa wanawake imara watakapotoka hapa,” ameeleza Bi. Mghen.

Naye Mkuu wa Gereza la Kahama, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Bonis Njoka Gervas, ametoa shukrani kwa kundi hilo kwa msaada na faraja walioutoa, akieleza kuwa hatua hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa urekebishaji wa wafungwa.
Bonis Njoka Gervas akizungumza

“Wafungwa wanahitaji sana faraja na kutiwa moyo. Msaada kama huu unasaidia kuleta utulivu na amani gerezani huku ukiwajengea matumaini wanapokuwa wakisubiri kumaliza vifungo vyao au kesi zao,” amesema.

TAMASHA LA MWANAMKE CHUMA 2026 

Maandalizi ya Tamasha la Mwanamke Chuma 2026 yamekamilika, ambapo tukio hilo kubwa linatarajiwa kufanyika Jumamosi, Aprili 11, 2026 katika Ukumbi wa Malex Hall, Kahama kuanzia saa 11 jioni.

Tamasha hilo, linaloandaliwa na Kituo cha Redio cha Gold FM, limejipambanua kama jukwaa muhimu la kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi kupitia elimu, mitandao na fursa mbalimbali.
Tamasha la mwaka huu linatarajiwa kupambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo msanii mkongwe wa muziki wa Taarab, Mzee Yusuph, huku mtaalamu wa maendeleo ya familia na uchumi, Dkt. Chris Mauki, akitoa mada maalum zitakazolenga kuwainua wanawake na jamii kwa ujumla. 

Aidha, shughuli hiyo itasindikizwa na ucheshi na uchangamshi kutoka kwa MC maarufu, Dkt. Kumbuka.

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ambaye atahitimisha rasmi tamasha hilo linalotarajiwa kuvuta washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa.

Mbali na burudani na elimu, tamasha hilo pia litahusisha utoaji wa tuzo kwa wanawake waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali, ikiwemo ubunifu, ujasiriamali, ushonaji, upishi, saluni pamoja na wanawake wenye ushawishi chanya katika jamii.

Kwa mujibu wa waandaaji, tamasha hilo ni zaidi ya burudani, ni jukwaa la kuibua vipaji, kuhamasisha uthubutu na kuimarisha mchango wa mwanamke katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Wananchi wa Kahama na maeneo jirani wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo muhimu ambalo linabeba ujumbe wa matumaini, uthubutu na nguvu ya mwanamke wa kisasa.










Share:

MUYINGA AISHUKIA CHADEMA KUHUSU KIINI CHA VURUGU ZA OKTOBA 29



Na mwandishi wetu, Dar

Mwanaharakati wa kijamii, Alphonce Patrick Muyinga ameonya kuhusu baadhi ya wanasiasa na wanaharakati kutumia nguvu kubwa kuvuruga na kuanzisha chokochoko dhidi ya Tume huru ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akiwataka kuiacha Tume hiyo kukamilisha kazi yake kwa mustakabali wa amani na haki ya Watanzania.

Muyinga amebainisha hayo leo Ijumaa Aprili 10, 2026, siku moja mara baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kuzungumza na wanahabari na kuhamasisha maandamano nchini pamoja na kuishutumu serikali kuhusu kuendelea kushikiliwa kwa mwanasiasa Tundu Lissu, akisema zote hizo ni njama za kuvuruga utendaji wa Tume ya Oktoba 29.

"Watanzania wote tunajua Rais Samia aliunda Tume hii kuchunguza yaliyotokea Oktoba 29, leo Tume inakaribia kumaliza kazi tujiulize kwanini Heche na genge lake la wanakaa kuchochea, kutengeneza propaganda, kutumia nguvu kubwa kuvuruga uchunguzi wa tume. Wanaficha nini? Kuna nini hawataki tume ije kusema? Tuache! Tume imalize kazi yake ije iseme. Suala la Lissu ni la kisheria na lipo mahakamani kama zlivyo kesi za wengine." Amesema Muyinga.

Muyinga amemkosoa Makamu Mwenyekiti huyo wa Chadema pia kuhusu namna ambavyo amekuwa akikwepa kuzungumzia ajenda za maendeleo nchini na badala yake kuhamasisha vurugu na kutaka Vijana kupinga na kuharibu jitihada mbalimbali za maendeleo nchini, akiwataka Vijana kuzinduka na kujifunza kuhusu Chadema na siasa zao za mihemko wanazofanya wao pamoja na washika wao.

Mwanaharakati huyo amehimiza utulivu kwa watanzania na wapenda haki wote wa ndani na nje ya nchi katika kipindi hiki ambacho Tume ya Oktoba 29 inapokwenda kukamilisha jukumu lake, akiwasihi pia kuwakataa kwa nguvu wale wote wanaoanzisha uchochezi na tuhuma mbalimbali dhidi ya Tume na serikali kwa lengo la kuikwamisha Tume hiyo kumaliza kazi yake na kukabidhi kwa mamlaka kwa hatua zaidi.
Share:

Thursday, 9 April 2026

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA APRILI 10, 2026

Share:

SANGU ASISITIZA UMUHIMU WA TAASISI ZA KIDINI KATIKA KULINDA AMANI YA NCHI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, ametoa wito kwa taasisi za kidini nchini kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri na kulinda amani, akitambua mchango wao mkubwa katika kudumisha utulivu wa kijamii. 

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 ya Kanisa la WRC huko Kivule, Dar es Salaam, Waziri Sangu alibainisha kuwa ushirikiano kati ya serikali na viongozi wa kiroho ni nguzo imara inayohakikisha wananchi wanaishi kwa mshikamano na upendo, jambo ambalo ni msingi wa maendeleo ya taifa.

Katika kutilia mkazo umuhimu wa amani, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, aliwasihi viongozi wa dini kutumia nafasi zao kukemea vitendo vyote vinavyohatarisha usalama, ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoweza kuchochea taharuki. 

Alisisitiza kuwa serikali inategemea maombi na malezi ya kiroho kutoka kwa madhehebu mbalimbali ili kujenga jamii yenye maadili mema, ambayo itakuwa vigumu kushawishika kujiingiza katika uhalifu au uvunjifu wa amani.

Kwa upande wao, viongozi wa kisiasa waliohudhuria hafla hiyo, akiwemo Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Mbunge wa Kivule, Ojambi Massaburi, walikiri kuwa malezi ya kiroho yamekuwa na mchango mkubwa katika kuandaa viongozi waadilifu. 

Walibainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anatambua thamani ya taasisi hizi na anaendelea kuunga mkono juhudi zao za kuliombea taifa. Kupitia maadhimisho hayo, ilibainika kuwa elimu ya uzalendo na mshikamano, hasa kuhusu Muungano, itaendelea kutolewa kwa vijana ili kuhakikisha tunu ya amani inarithishwa kwa vizazi vijavyo bila kutetereka.
Share:

GAVANA TUTUBA :TANZANIA IMEPIGA HATUA MIFUMO YA MALIPO YA KIKANDA



Na mwandishi wetu,Morocco

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuunganishwa na mifumo ya malipo ya kikanda, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha ndani na nje ya nchi pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumza leo Aprili 3, 2026 jijini Tangier, nchini Morocco, wakati wa mjadala wa mawaziri katika Kikao cha 58 cha Tume ya Uchumi ya Afrika (ECA), Gavana Tutuba amesema hatua hiyo inaifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya mtandao wa malipo barani Afrika.

“Tanzania ni sehemu ya mifumo ya malipo ya kikanda ikiwemo Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS) na Mfumo wa Malipo wa Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC RTGS). Kwa sasa benki za biashara nchini zinaendelea kujiunga na Mfumo wa Malipo wa Afrika (PAPSS), unaowezesha miamala ya kifedha kati ya nchi za Afrika kwa haraka na ufanisi,” amesema Bw. Tutuba.

Ameeleza kuwa kuimarika kwa mifumo hiyo kutachochea biashara ya mipakani na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika, huku akibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kutumia teknolojia ya fedha kuboresha sekta hiyo.

Aidha, amesema uwepo wa mifumo hiyo ni matokeo ya maendeleo ya teknolojia ya fedha (fintech), akisisitiza kuwa BoT inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana wabunifu kupitia majukwaa mbalimbali ili kuibua suluhisho za kidijitali zitakazoboresha huduma za kifedha nchini.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Gavana Tutuba amesema teknolojia ya fedha pamoja na ubunifu wa kidijitali vitaendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani.

Kikao hicho kimewakutanisha mawaziri wa fedha, mipango na maendeleo ya uchumi pamoja na magavana wa benki kuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika kujadili mwelekeo wa uchumi wa bara hilo na namna ya kuimarisha mifumo ya kifedha.
Share:

JAMII YATAKIWA KUSHIRIKIANA NA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KULINDA AMANI



Jamii imetakiwa kushirikiana kwa karibu na Vyombo vya ulinzi na usalama na mamlaka nyingine za uongozi zilizopo nchini katika kutoa taarifa za matukio ya uvunjifu wa amani, uhalifu na wahalifu pamoja na kutumia vyema mitandao ya Kijamii ili kudumisha na kuendeleza amani, utulivu na usalama wa nchi kama msingi mkuu wa uhai, maendeleo ya kiuchumi, kijamii na ustawi wa haki.

Kadhalika Waandishi wa habari hapa nchini wamehimizwa kutumia kalamu zao vyema na kuandaa maudhui kwenye majukwaa yao ya habari ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini ili kuhakikisha kuwa amani hiyo inaendelea kuwepo pamoja na kuendeleza mshikamano wa Watanzania kwa kuuhabarisha kuhusu hatua mbalimbali za maendeleo na namna wanavyoweza kunufaika na amani na utulivu unaoendelea kuwepo nchini.

Wito huo umetolewa na  Epimark Aqwesso na  Gabriel Hilonga Silo, wakazi wa Wilayani Karatu Mkoani Arusha, wakitahadharisha watanzania kurejea katika matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kadhia waliyokutana nayo kutokana na kukwama kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.

"Amani tuliyonayo hapa nchini kwetu ndio inatufanya tuendelee kukusanyika na kufanya shughuli zetu nyingine za kijamii na kiuchumi. Mnakumbuka tukio la Oktoba 29, 2025? wengi wetu tulishindwa kufanya shughuli zetu, hofu ilitanda na wengi waliingia mitini na kujificha, hali hii isijirudie tena, Vijana wa sasa (GenZ) tukumbuke kuna maisha kesho na kamwe tusiharibu amani ya nchi yetu." Amesema Bw. Aqwesso.

Kwa upande wake Bw. Silo amehimiza Vijana kutumia vyema fursa ya amani iliyopo nchini kwa kujiendeleza kiuchumi, akieleza namna ambavyo serikali imeendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji, akisisitiza kuwa amani ndio uhai wa Nchi na wananchi wake na kutaka jamii kushirikiana kuilinda.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO ALHAMISI APRILI 9,2027



         
Share:

Wednesday, 8 April 2026

SERIKALI YAINUA UTALII WA TIBA: WAGONJWA WA NJE WAFIKIA 3,018



Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kukuza utalii wa tiba, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuongeza uchumi wa sekta ya afya na mchango wake wa pato la Taifa.

Hayo yamesemwa leo Aprili 08, 2026, na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, bungeni jijini Dodoma, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Catherine Canute Joachim, katika Bunge la Kumi na Tatu, Mkutano wa Tatu, Kikao cha Nne.

Akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Afya,.Mhe. Mohamed Mchengerwa, Dkt. Samizi amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza zaidi kwenye uboreshaji wa miundombinu ya hospitali, ikiwemo kujenga majengo mapya na kukarabati yale yaliyochakaa.

Aidha, amesema Serikali inaendeleza upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa kama PET/CT Scan, Angio Suite, Cathlab, na CT Scan, sambamba na kuendeleza mafunzo ya kitaaluma kwa wataalamu wa afya ili kuhakikisha huduma zinakuwa za ubora wa kimataifa.

“Serikali pia inaanzisha huduma mpya za ubingwa bobezi na kuhakikisha hospitali zinapata ithibati za kimataifa, na kuzitangaza katika masoko ya kimataifa ili kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi,” amesema Dkt. Samizi.

Takwimu zinaonyesha ukuaji wa utalii wa tiba: katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, wagonjwa 3,018 kutoka nje ya nchi walipatiwa huduma za ubingwa bobezi katika hospitali za rufaa za mikoa, kanda, maalum na taifa.

Aidha, Dkt. Samizi ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika rasilimali watu kupitia Samia Health Super-specialization Program, ambapo wataalamu 1,483 wanafadhiliwa kusomea fani za ubingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza ubora na uwezo wa hospitali zetu.
Share:

Tuesday, 7 April 2026

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO APRILI 8,2026

Magazeti






Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger