Wednesday, 15 October 2025

RC MAKALLA AWAHAKIKISHIA USALAMA WAZEE WA MKOA WA ARUSHA SIKU YA UPIGAJI KURA OKTOBA 29



Na Mwandishi wetu, Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amewahakikishia wazee na wananchi wa Mkoa wa Arusha kuwa wamejipanga Vyema kuhakikisha siku ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kutakuwa na amani na mazingira tulivu ya upigaji kura, akitoa wito kwa kila Mwananchi mwenye sifa kujitokeza kwa wingi kuchagua Viongozi wanaowataka ili kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo.

CPA Makalla ametoa wito huo wakati wa matembezi ya amani ya Wazee wa Mkoa wa Arusha, waliofanya matembezi hayo Jijini Arusha kwaajili ya kuliombea Taifa amani kama sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Wakianzia matembezi hayo kwenye Viunga vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kwenda Mnara wa saa, Metropole, Idara ya maji, kituo cha Mabasi Arusha na baadaye kumalizia tukio lao kwenye Viwanja vya Makumbusho Jijini Arusha.

"Kupiga kura ni haki ya Kikatiba ya kila Mtanzania. Wazee wangu mtukumbushe na kuwakumbusha Vijana kuitunza amani, kutumia vyema mitandao ya kijamii lakini Vijana wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi. Niwahakikishie mtapiga kura kwa amani na atakayeshinda atangazwe kushinda." Amesema.

Makalla amewahakikishia wananchi wote amani na usalama katika kipindi hiki cha lala salama za Kampeni, wakati wa upigaji kura na hata baada ya kura, akisema amani ni muhimu kwa maendeleo pamoja na ukuaji wa sekta ya utalii katika Mkoa huo ulio kitovu cha utalii kwa upande wa Tanzania bara.

Kwa upande wao baadhi ya wazee walioshiriki matembezi hayo kwaniaba ya wenzao wamewasihi wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuhimiza kila mmoja kulinda amani ya Mkoa wa Arusha, wakisema amani imekuwa tunu muhimu ya maendeleo na ustawi wa watu wa Mkoa wa Arusha.


Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO OKTOBA 15,2025

Magazeti

 





Share:

Tuesday, 14 October 2025

AGNESS SULEIMAN KAHAMBA (AGGYBABY ) ASHINDA TUZO YA MWIGIZAJI BORA WA KIKE WA TANZANIA MWAKA 2025


Msanii wa Muziki na Maigizo Bi Agness Suleiman Kahamba maarufu kama (Aggybaby) amepokea Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike wa Mwaka 2025 kutoka Achievers Awards International ya nchini Nigeria kutokana na kazi zake za sanaa ya uigizaji na shughuli zake za huduma kwa jamii kupitia taasisi yake—Tupaze Sauti Foundation (Tanzania).

Waandaaji wa tuzo hizi wametambua kazi nzuri anayoifanya mwanatasnia Agness katika sekta ya filamu hususani kupitia tamthiliya za "Panguso", "Huba" na kazi zake nyingine za filamu katika mtandao wa YouTube.

Tuzo hii ni alama ya ushirikiano wa kifilamu uliodumu kwa muda mrefu kati ya Tanzania na Nigeria .Bi Agness amebainisha kwamba waandaaji wa tuzo hizi wanavutiwa sana na filamu kutoka Tanzania kipekee wautaja utamaduni wetu, amani na ushirikiano unaooneshwa katika filamu zetu kuwa alama ya utu wa mwafrika—akinasibisha yale wanayoyaona kupitia tamthiliya ya “Kombolela”.

Leo, Jumatatu Tarehe 13 Oktoba 2025—Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga (PhD) amekutana na kufanya mazungumzo na mwanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza nchini—Agness Suleiman Kahamba @aggybaby__

Pia Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Gervas Kasiga (PhD) amempongeza Agness kwa juhudi zake za kufanya kazi bora za filamu na kwa kuiwakilisha vyema Tanzania katika majukwaa ya filamu kimataifa.


Aidha, Dkt. Kasiga (PhD) amemsihi Agness kuendelea kufanya kazi zake za sanaa kwa ubunifu na weledi mkubwa ili kuutangaza vyema utamaduni wetu wa Kitanzania ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.
Share:

NAKAWALE KUWA LANGO KUU LA KIUCHUMI -JENISTA MHAGAMA

Mgombea nafasi ya Ubunge jimbo la Peramiho Halmashauri ya Songea Vijijini na Waziri wa Afya Jenista Mhagama akiwa amezungukwa na halaiki ya wananchi na wanachama wa chama cha mapinduzi CCM kata ya Muhukuru 

Na Regina Ndumbaro Muhukuru-Peramiho 

Katika muendelezo wa kampeni za kuomba kura kuelekea uchaguzi mkuu nchini Tanzania, Mgombea wa nafasi ya Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, amefanya mkutano wa kampeni katika Kata ya Muhukuru, Jimbo la Peramiho, Halmashauri ya Songea Vijijini, mkoani Ruvuma. 

Akizungumza na wakazi na wanachama wa CCM tarehe 13 Oktoba, Mhagama amesisitiza kuwa eneo la Nakawale linakwenda kuwa lango kuu la uchumi na eneo maalum la kimkakati, likichochewa na nafasi yake ya kijiografia jirani na mpaka wa Tanzania na Msumbiji.

Mhagama amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM umeweka msukumo mkubwa katika kuwajengea uwezo wananchi kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kiuchumi, badala ya kuwa watazamaji. 

Amesisitiza kuwa serikali imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha wananchi wa Nakawale wananufaika na fursa za kibiashara na uwekezaji zitakazoibuka kutokana na miundombinu ya mpaka wa  Mkenda.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kutoa mikopo kwa vijana kuanzisha biashara ndogondogo, kutoa hamasa kwa makundi ya akina mama, vijana na wazee pamoja na kuanzisha viwanda vidogo vya uchakataji wa mazao.

Akiwa kwenye ziara hiyo, Mhagama pia Ameeleza kuwa katika kukuza huduma za kijamii, serikali kupitia Ilani ya CCM imepanga kujenga Kituo cha Afya Nakawale, kukarabati kisima cha maji, pamoja na ujenzi wa shule shikizi katika maeneo ya Mkayukayu na Kaloleni. 

Vilevile, amesema kuwa shule ya msingi Nakawale itaongezewa madarasa na matundu ya vyoo, huku shule ya sekondari ya Muhukuru ikiboreshewa miundombinu kwa kuongeza madarasa, nyumba za walimu na taa za barabarani ili kuruhusu shughuli za mchana na usiku.

Katika upande wa afya, Mhagama ameahidi kuwa huduma bora kwa mama na mtoto zitaendelezwa kwa lengo la kurahisisha uzazi salama, sambamba na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, figo, kisukari na moyo. 

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia huduma za vipimo kwa watu wasiokuwa na uwezo ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki ya huduma bora ya afya bila ubaguzi.

 Jenista Mhagama amewaomba wananchi wa Nakawale na maeneo yote ya Jimbo la Peramiho kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe 29 Oktoba. 

Ameeleza kuwa mwaka huu ni wa kihistoria kwani kwa mara ya kwanza, mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais anatoka mkoa wa Ruvuma. 

Hivyo, amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kudhihirisha mshikamano wao kwa CCM kwa kujitokeza kwa wingi na kupiga kura, kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazoendeshwa na chama hicho.


Share:

Monday, 13 October 2025

VIJANA SASA KUJIFUNZA UFUNDI KWA URAHISI KUPITIA PROGRAMU YA VSOMO YA VETA


Na Mwandishi Wetu,Mbeya

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea kutumia teknolojia ya kisasa kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa VSOMO, unaowawezesha wanafunzi kujifunza kwa kutumia simu janja (smartphone) wakiwa mahali popote nchini.

Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mkoani Mbeya, Ofisa Habari na Uhusiano wa VETA, David Mpondyo, alisema mfumo huo utasaidia kutoa fursa kwa watu wengi kupata mafunzo ya ufundi stadi bila kulazimika kuwepo darasani.

“Mwanafunzi anapakua programu ya VSOMO kupitia Play Store, kisha anaanza kujifunza kwa nadharia kupitia simu yake janja baada ya kukamilisha sehemu ya nadharia, hufanya mafunzo kwa vitendo (practical) katika chuo cha VETA kilicho karibu na anapomaliza hupewa cheti kinachotambulika sawa na wale waliopo darasani,” alisema Mpondyo.

Alibainisha kuwa mfumo huo umetumika kwa zaidi ya miaka tisa na umeendelea kuboreshwa ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha hata sehemu ya vitendo inaweza kufanyika kwa kutumia simu janja.

Aidha, Mpondyo alisema VETA inatumia mfumo mwingine wa elimu kwa masafa uitwao Open and Distance e-Learning (ODeL), unaotumia TEHAMA kuwafikia wanafunzi walioko mbali na vyuo. 

Alisema mfumo huo unahusisha matumizi ya teknolojia mbalimbali za kisasa kama Uhalisia Pepe (Virtual Reality), Vifaa vya kuiga mazingira halisi ya kazi (Simulators), Mechatronics, Roboti (Robotics), Akili Bandia (Artificial Intelligence – AI) na Mtandao wa Vitu (Internet of Things – IoT).

Kwa mujibu wa Mpondyo, Serikali imetumia Shilingi milioni 273 kununua vifaa vya kufundishia vya kuiga mazingira halisi ya kazi (simulators) kwa ajili ya mafunzo ya uchomeleaji na uungaji vyuma, ili kuongeza ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi.

Alisema kuwa mafanikio ya matumizi ya teknolojia hizo yameongeza ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia miongoni mwa wakufunzi, wanafunzi na wahitimu wa vyuo vya VETA, ambao wamekuwa wakibuni suluhisho la changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi kupitia maarifa waliyojifunza.

“Lengo letu ni kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya soko la ajira. Tunaendelea kuboresha mazingira ya mafunzo ili kufikia vijana wengi zaidi na kuwapa maarifa ya kisasa,” alisisitiza Mpondyo.


Share:

MCHENGERWA AMWOMBEA KURA RAIS KWA WANARUFIJI, ASISITIZA UJENZI WA BARABARA MLOKA- MKONGO.


Na Yohana Kidaga- Kipugira

Mgombea wa Ubunge jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kumchagua tena katika kipindi hiki atakwenda kusimamia maendeleo ya wananchi wa Jimbo hili, huku akimwombea kura Mhe Rais Samia.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi katika kata ya Kipugira Mhe. Mchengerwa amesema katika kata hilo endapo atachaguliwa atakwenda kuishawishi Serikali kukamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mloka hadi Mkongo ili ipitike katika kipindi chote cha mwaka.

"Naomba niwahamikishie miaka mitano ijayo tutapambana kufa na kupona kuhakikisha kuwa barabara ya Mloka hadi Mkongo inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami.Najua hiki ndiyo kilio kikubwa cha tarafa ya Mkongo". Amesisitiza Mhe Mohamed Mchengerwa huku akishangiliwa na wananchi wakionyesha kuwa anatambua vema changamoto ya Wanakilugila na Rufiji kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa siasa zake ni za maendeleo ya kwa maana ya kwamba siasa zake zimelenga katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli na siyo ujanja ujanja.

Aidha, amewahimiza wanananchi kufanya kazi kwa bidiii ili kuondokana na umasikini na kuinua hali zao za maisha huku akisisitiza kuwa maendeleo huletwa kwa kufanya kazi.

Mhe. Mchengerwa metumia mkutano huo kutaja mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka kumi cha mabadiliko ya fikra kwa wananchi wa Rufiji.

Baadhi ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hicho ni pamoja na ongezeko kubwa la ujenzi wa miundombinu inayojumuisha madaraja barabara na taa za barabarani, shule za msingi na Sekondari, vituo vya afya na hospitali pia huduma za maji na umeme katika vijiji vyote 38 vya Jimbo hilo.

Leo Mhe Mchengerwa anaendelea na mikutano ya hadhara katika kata nyingine za Jimbo hilo kuomba kura kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa madiwani na kwake mwenyewe ili apewe ridhaa ya kuwaongoza tena katika kipindi hiki.

Mhe Mohamed Mchengerwa ni Mbunge wa tisa wa kuchaguliwa katika jimbo hilo la Rufiji toka lianzishwe na kuongozwa na wabunge kadhaa kuanzia Mhe. Bibi Titi Mohamed ambapo anaelezewa kuwa ni miongoni mwa wabunge walioliletea maendeleo makubwa Jimbo hilo ukilinganisha na wabunge waliotangulia.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger