Tuesday, 10 October 2023

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO OKTOBA 11,2023

Share:

KAMISHNA WAKULYAMBA: HONGERENI TANAPA KWA UHIFADHI ULIOTUKUKA NA USIO NA MAWAA.


Na. Jacob Kasiri- Kitulo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Benedict Wakulyamba amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa uhifadhi uliotukuka na usio na mashaka kwa taifa.

Kamishna Wakulyamba ameyasema hayo leo tarehe 10.10. 2023 alipotembelea Hifadhi ya Taifa Kitulo iliyopo wilayani Makete katika mkoa wa Njombe.

Ndani ya hifadhi hiyo Kamishna Wakulyamba alitembelea Lango la Mwakipembo, Uwanda wa Maua, Maporomoko ya maji ya Mwakilema na Mwakipembo.

Baada ya kuviona vivutio hivyo na baadhi ya mamalia wachache walioonekana kwa muda huo, hakusita kuonesha furaha yake alipotazama upande wa Mashariki na kuona mandhari nzuri iliyonakshiwa kwa safu za milima  ya Livingstone na tambarare iliyotaradadi kwa maua yenye rangi tofauti mithili ya zulia.

"Nimeridhishwa na kazi nzuri za uhifadhi mnazozifanya maafisa na askari wa TANAPA. Hongereni  kwa kuendelea kuhifadhi rasilimali zetu, serikali na wizara inatambua kazi nzuri mnayoifanya ya uhifadhi kwani mnajituma usiku na mchana.”

Kwa tafsiri isiyo rasmi mwanamapinduzi kutoka nchini India Mahatma Gandhi aliwahi kusema, Utajiri wa taifa lolote lile duniani unategemeana na jinsi taifa hilo linavyoheshimu na kulinda wanyamapori wake. Hivyo wanachokifanya TANAPA ni kuendeleza falsafa hiyo.

Aidha, Kamishna Wakulyamba alisisitiza  maelekezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angela Kairuki (Mb) kutekelezwa, kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mdogo wa ndege karibu na Hifadhi ya Taifa Kitulo ambao utakuwa chachu ya kukuza utalii na kufungua fursa za uwekezaji kwa wananchi wa maeneo jirani.

" Kufanya kazi kwa uadilifu ndio msisitizo namba moja, msijihusishe na vitendo vinavyokinzana na maadili ya kazi kama vile rushwa na ujangili," aliongeza Kamishna Wakulyamba.

Kamishna Wakulyamba pia, aliwataka maafisa na askari kujiendeleza kielimu alisema, "mnapopata nafasi msisite kujiendeleza katika fani ya uhifadhi au fani nyingine kulingana na matakwa ya taasisi, mnaposoma hakikisheni hamuathiri utendaji kazi wa shirika."

Aidha, Kamishna Wakulyamba alifanikiwa kutembelea Ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Kusini yaliyopo Rujewa Wilayani Mbarali, na kuwapongeza TANAPA  kwa ujenzi wa ofisi kubwa na yenye hadhi ya Kanda.

Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini Steria Ndaga, akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo alisema, "Kanda ya kusini ina jumla ya maafisa na askari 17, kati yao wawili ni wa kike na 15 ni jinsia ya kiume".

"Lengo la uanzishwaji wa kanda hii ni kuratibu na kusimamia shughuli za Uhifadhi, Utalii na mwenendo mzima wa Ikolojia katika Hifadhi za Taifa Ruaha, Kitulo na Katavi" alisema Kamishna Ndaga.

Kanda ya Kusini - TANAPA ilianzishwa mwezi mei, 2019 baada ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania lenye makao makuu yake jijini Arusha kufanya ughatuzi wa madaraka uliopelekea  kuanzishwa kwa kanda nne.


Share:

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAONESHA UBABE MASHINDANO YA RIADHA SHIMIWI



Na. Mwandishi Wetu, Iringa

Wizara ya Maliasili na  Utalii imeendelea kuonesha ubabe wake kwenye mbio
ambapo kwa upande wa wanaume imeibuka kinara  kwenye mbio za mita 1500 na  mshindi wa pili kwenye mbio za mita 400 huku  kwa upande wa wanawake  imeibuka   mshindi wa tatu kwenye mbio za mita 1500 katika Mashindano ya 37 ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea Mkoani Iringa .

Akizungumza leo mkoani humo mara baada ya ushindi huo Bw. Elibariki Buko ambaye ndiye mshindi wa mbio namba moja wa mita 1500 na namba  mbili za mita 400,  amesema ushindi huo ni matokeo ya  uongozi makini wa Menejimenti ya  Wizara ya Maliasili na Utalii

" Ushindi huu  sio wa kwangu mimi  bali ni ushindi wa Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wamekuwa msaada mkubwa  kwetu kuanzia maandalizi hadi hatua hii. Niwashukuru sana Mimi pamoja na watumishi wenzangu kwa  kuendelea kutuwezesha kushiriki katika  michezo hii.

Ametumia fursa hiyo  kuihakikishia Menejimenti ya Wizara hiyo kuwa yeye pamoja na wenzake watatumia michezo hiyo kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini huku akiomba kuendelea kupewa nafasi zaidi katika kushiriki katika mashindano mengine  ili waweze kukidhi ndoto na maono aliyonayo Rais Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya utalii kitaifa na kimataifa.


, ‘’Tumeanza kutangaza utalii na vivutio vya utalii vilivyopo maeneo haya kama Hifadhi ya  Ruaha na hata vivutio vingine kama Hifadhi ya Taifa ya Nyerere." amesema Buko.

Ameongeza,’’ imetusaidia pia  kujenga ushirikiano na afya kwani  nina uhakika mara tukaporudi katika maeneo yetu ya kazi umakini na uhodari katika kuhudumia watanzania utaongezeka’’ 

Kwa upande wake Jehovaness Sarakikye ambaye ndio mshindi wa tatu kwenye mbio za mita 1500 kwa wanawake amesema, aliamini atashinda mbio hizo mara baada ya kufanya maandalizi ya kutosha huku akiwapongeza Walimu kwa kuwaandaa vzuri kwa ajili na shindano huo

‘’Tulijiandaa vizuri, haikuwa rahisi lakini nawashukuru sana Walimu wetu walifanya kazi nzuri ya kutuandaa kwa ajili mchezo huu’’ Alisema Sarakikye

Naye Mratibu wa Timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Leodger Kiwia   ametumia fursa hiyo kuwapongeza washindi hao kwa kuipatia ushindi Wizara huku akisisitiza kuwa Wizara itahakikisha inaendelea kupambana ili kushinda michezo iliyobakia na hatimaye kubeba vikombe vyote.

" Nawapongeza sana Washiriki wetu wote ikiwemo na hawa wa Riadha, ushindani ulikua mkali sana lakini hatimaye wameiletea Wizara yetu furaha. Sisi kama Viongozi tutaendelea kusaidia wachezaji hawa kwa namna yeyote ile ili watuletee ushindi na hatimaye tupeleke vikombe nyumbani’’ Amesema Kiwia

Share:

TAFIRI KUFANYA TAFITI ZAIDI YA MCHANGO WA SEKTA YA UVUVI



Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga akizungumza wakati wa kufungua rasmi warsha ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa. Warsha hiyo inafanyika jijini Dar es Salaam ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani.


Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utafiti pamoja na Uratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Mary Kishe akibainisha umuhimu wa tafiti na kuainisha mafanikio ya taasisi hiyo ambapo mwaka huu inafikisha miaka 40, wakati wa warsha ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini. Warsha hiyo inafanyika jijini Dar es Salaam ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani.


Picha ya pamoja ya washiriki wa warsha ya kufanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa. Warsha hiyo inafanyika kwa siku tano jijini Dar es Salaam ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani ambapo wanafanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Na. Edward Kondela



Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ikishirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani inafanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Akizungumza (09.10.2023) kando ya warsha hiyo baada ya kuifungua rasmi, inayoendelea jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga amesema tafiti hizo zitaibua taarifa za maeneo ambayo sehemu ya maziwa na Bahari ya Hindi iliyopo nchini kuweka taarifa zake sahihi kulingana na idadi ya watu ambao wamekuwa wakinufaika kupitia rasilimali zilizopo katika maji hayo.

Bw. Lukanga ameongeza kuwa kwa sasa idadi ya watu nchini imeongezeka na kufikia zaidi ya milioni sitini ila bado taarifa zilizopo kwenye sekta ya uvuvi zinatolewa kulingana na idadi ya watu iliyokuwepo zamani ya zaidi ya milioni 40 ambayo imekuwa ikibainisha watu wanaojishughulisha moja kwa moja katika sekta ya uvuvi ni milioni 4.5.

Aidha, amesema warsha hiyo imeanzishwa na wanasayansi na watafiti kutoka nchi zaidi ya 58 kuhakikisha rasilimali ambazo hazijionyeshi kwa uwazi ziweze kuonekana hususan kwenye uvuvi mdogo ili kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utafiti pamoja na Uratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Mary Kishe amesema taasisi hiyo ambayo mwaka huu inafikisha miaka 40 imekuwa ikikusanya na kutafiti masuala mbalimbali ya sekta ya uvuvi lakini bado haijaangalia mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa na mtu mmoja mmoja.

Amesema kupitia warsha hiyo inayoendelea jijini Dar es Salaam, ambapo TAFIRI inashirikiana na FAO pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani wataweza kuunganisha taarifa za zamani na kuziweka pamoja na kuona umuhimu wa takwimu hizo kwa maendeleo endelevu ya sekta ya uvuvi kwa kuwa kuna taarifa ambazo zimejificha ambazo hazionyeshi usahihi juu ya sekta hiyo.

Pia, amesema warsha hiyo ni muhimu ambapo watafiti watapata fursa ya kutoa mapendekezo yao ya namna ya kusimamia rasilimali za uvuvi ili kuweza kufikia lengo la sekta ya uvuvi kuongeza mchango zaidi katika pato la taifa.

Naye Afisa Mkuu kutoka FAO, Bw. Nicolas Gutierrez na Afisa Mipango Mtafiti kutoka FAO Bi. Nicole Franz wakizungumza kando ya warsha hiyo wamesema uwepo wa taarifa sahihi ni muhimu katika kuendeleza sekta ya uvuvi nchini pamoja na kutoa elimu kwa wavuvi wa umuhimu wa taarifa hizo pamoja na kulinda rasilimali za uvuvi.

Wamebainisha pia uwepo wa taarifa sahihi ya sekta ya uvuvi utawezesha kubadili maisha ya watu wanaojishughulisha na uvuvi hususan wavuvi wadogo kwa kuangalia namna wanavyochangia katika sekta hiyo kwa kuwa ni sekta ambayo inachangia katika ongezeko la chakula duniani.

Warsha hiyo ambayo ni muhimu katika kuangalia mchango wa sekta ya uvuvi nchini inafanyika kwa siku tano jijini Dar es Salaam ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani ambapo wanafanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.
Share:

TAASISI YA MWALIMU NYERERE KUZINDUA MRADI WA KITAIFA WA MAADILI NA UZALENDO




Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) Joseph Butiku alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Babati Mkoani Manyara.

Na. Jawadu Kinyobwa, Babati + Manyara

Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) inatarajia kuzindua mradi wa Kitaifa wa Maadili na uzalendo Oktoba 14, 2023 katika kilele cha Maadhimisho ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mkoani Manyara unaolenga kuzuia mmomonyoko wa maadili.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) Joseph Butiku Oktoba 9, 2023 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Babati Mkoani Manyara.

Amesema kwa mujibu wa Tafiti zilizofanyika hivi karibuni, zimebainisha kuporomoka kwa maadili na uzalendo hali inayo pelekea vitendo viovu katika jamii ikiwemo ukatili wa kijinsia, wizi, ulevi na matendo mengine ambayo ni kunyume na maadili ya kitanzania.

Butiku amesema ustawi wa Taifa lolote unahitaji Amani, Umoja na Maendeleo ya watu wake na nguzo kuu ya mambo hayo ni imani na maisha yanayozingatia usawa wa binadamu wote na haki sawa kwa wote.

“Amani ndio msingi wa kila jambo, Amani ni msingi wa umoja na maendeleo ya ustawi bora wa Taifa. Umoja ni nguvu, umoja ni uzalendo, Hakuna lolote kubwa linaloweza kufanyika bila umoja au kushikamana kwa jamii husika, iwe ndogo au kubwa, kabila au Taifa” amesema Butiku

Aidha, amesema kumomonyoka kwa maadili ya watanzania kunasababishwa na uwepo wa mitandao ya kijamii inayoruhusu upatikanaji wa habari ambazo hazina manufaa kwa Taifa na changamoto za Maisha zinazo wasahaurisha wazazi na walezi malezi bora ya watoto wao.
Share:

UJENZI WA BANDARI YA LAGOSA WAFIKIA 90%


Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa bandari ya Lagosa iliyopo katika Kijiji cha Mgambo wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amesema ujenzi huo unaogharimu shilingi bilioni kumi na Tano tayari umefikia asilimia tisini na sita na kusisitiza ifikapo mwezi Aprili mwaka 2024 mradi huo uwe umekamilika .

Aidha Prof.Mbarawa amesema uwepo wa bandari hiyo utachagiza ufanisi wa shughuli za kiuchumi hasa kilimo ,uvuvi na biashara kwa wakazi wa mwambao wa ziwa Tanganyika ambao kupitia bandari hiyo wataweza kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwenda nje ya nchi.

Kwa upande wake naibu mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania TPA mhandisi Juma Kijavara amesema TPA imejipanga kukamilisha ujenzi huo haraka ili bandari hiyo ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Naye mkuu wa wilaya ya uvinza Dina Masamani ameishukuru serikali kwa kujenga bandari hiyo akisisitiza kuwa itawezesha wakazi kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo kusafirisha bidhaa kwenda nchi Jirani ya Congo ambayo ipo umbali wa Kilometa themanini na nane kutoka bandarini hapo.

Share:

KATIBU MKUU CCM AWEKA WAZI NEEMA KUMALIZA ADHA YA USAFIRI ZIWA TANGANYIKA, MBOLEA NA MALIPO YA WAKULIMA WA MAHINDI


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Komredi Daniel Godfrey Chongolo ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025, kwa vitendo, kuboresha huduma za uchukuzi, usafiri na usafirishaji katika Ziwa Tanganyika, ambapo kufikia mwezi Disemba, 2023, wananchi wataanza kupata nafuu, kuelekea kumalizika kwa adha kubwa iliyopo sasa.

Unafuu huo utatokana na kukamilika kwa matengenezo ya moja ya meli, kati ya mbili zilizopo sasa, Mv Mwongozo na Mv Liemba, ambazo zote zinafanyiwa matengenezo, ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu, pamoja na kutengeneza meli mpya, kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na wananchi kwa ujumla, ambazo hatimae zitaondoa na kumaliza kabisa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika, kuunganisha hadi nchi jirani za DR Congo na Zambia.

Katibu Mkuu wa CCM, Komredi Chongolo ametangaza mikakati hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kalambo, Jumatatu Oktoba 9, 2023, ambapo anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Rukwa, yenye malengo ya kuhamasisha uhai wa CCM, kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 – 2025, kwa kutembelea miradi ya maendeleo.

“Wote ni mashahidi hizi meli (Mv Liemb ana Mv Mwongozo) zimetengenezwa miaka mingi, ingawa Mwongozo sio ya miaka mingi sana kama Liemba. Juzi nikiwa Katavi nimezungumza na Waziri wa Uchukuzi, tumekubaliana mambo kadhaa ikiwa ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM na maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.”

“Kuhakikisha wanachukua hatua za haraka ili MV Mwongozo au MV Liemba mojawapo ianze kazi wakati nyingine inaendelea kufanyiwa marekebisho. Makubaliano tuliyokubaliana tayari wameanza kuyatekekeleza. Sasa hivi tunavyoongea meli ya Mwongozo imewekwa kwenye chelezo pale Kigoma mjini,” amesema Chongolo.

Ndugu Chongolo amesema kuwa kwa sasa meli hiyo inakaguliwa kwa ajili ya kuona matengenezo yanayotakiwa kufanyika ikifika Desemba mwaka huu iwe tayari kurudishwa kwenye maji Ziwa Tanganyika ili ianze kufanya safari, huku akiongeza kuwa kwa upande wa MV Liemba ambayo yenyewe inahitaji matengenezo makubwa zaidi kutokana na ukongwe wake, tayari wizara yenye dhamana imetangaza mkandarasi wa kuifanyia marekebisho.

“Kwa sababu meli hii imeshafanya kazi zaidi ya miaka 100, hivyo itafanyiwa marekebisho makubwa na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya kufanya kazi hiyo na uhakika wa kufanya hivyo ni asilimia 100,” amesema Chongolo.

Aidha amesema Serikali imejenga bandari za mwambao wa Ziwa Tanganyika, ambapo kuna Bandari ya Kabwe, Bandari ya Kasanga zilizoko mkoani Rukwa, Bandari ya Karema ambayo iko Katavi, pamoja na Bandari ya Kigoma, huku akibainisha kuwa hata bandari zingine ndogo ndogo zinawekewa mipango ili zifanye kazi ya kurahisisha shughuli za usafiri, usafirishaji na uchukuzi ili wananchi wajitafutie maendeleo yatakayoboresha maisha yao na kuwawezesha wananchi kujitengenezea uchumi wao.

“Ili zifanye kazi Serikali imefanya uamuzi tayari. Wiki hii tuliyonayo, pale Kigoma watasaini mkataba na mkandarasi atayejenga karakana ya meli Kigoma na kwa maana hiyo kabla ya mwaka huu kuisha mkandarasi atakuwa ameshakusanya vifaa vyake kwa ajili ya kujenga karakana na hiyo karakana itakuwa ya kudumu.

“Lengo ni kwamba karakana hiyo ikikamilika itajengwa meli ya mizigo zaidi ya tani 3500 ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba magari marefu (malori) 100 kwa wakati mmoja. Maana yake muda si mrefu watu watakuwa na njia mbadala na kuepuka kwa msongamano wa njia ya Tunduma kwenda DRC (Congo) kwa kulazimika kupitia Zambia.

Amesema kuwa wasafiri na wote wanaohusika na shughuli za usafirishaji na uchukuzi wataweza kutumia njia ya Kasanga, watavuka kwa meli kwenda upande wa pili, ambako pia meli zitakuwa zinasafirisha watu na mizigo kuja upande mwingine, akiweka wazi kuwa maneno hayo yatawekwa katika vitendo vinavyoendelea kutafsiri dhamira ya dhati ya CCM kuendelea kuongoza nchi na kuwatumikia wananchi, kwa kuisimamia Serikali ili iweze kutengeneza mazingira na fursa za wananchi kujikwamua kimaisha na kubadili hali zao, kupitia shughuli za kiuchumi.

Kuhusu upatikanaji wa mbolea kwa msimu ujao wa kilimo na malipo ya fedha za mahindi waliyouza msimu huu, Katibu Mkuu Chongolo, akizungumza katika maeneo hayo, ikiwemo Singiwe, Kasanga, Kisumba, Chisenga na Matai, amesema kuwa wanakwenda kuielekeza Serikali, kupitia Wizara ya Kilimo, kuhakikisha inaondoa hofu ya wananchi, kwa kuhakikisha mbolea inauzwa kwa bei elekezi kama ambavyo Serkali imeelekeza na ipatikane kwa wingi na ihakikishe wakulima wanalipwa malipo yao haraka.

Kuhusu ujenzi wa Barabara ya Matai – Kasesya yenye kilometa 50, Ndugu Chongolo amesema kuwa mradi huo wa kimkakati utakuwa mkombozi mwingine katika kufanya biashara na kuyafikia masoko ya nchi jirani ambapo ikikamilika magari, yakiwemo malori yanayokwenda nchi jirani yataweza kuchagua ama kupitia Tunduma au Rukwa, Kalambo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Josephat Kandege mbali ya kumuomba Katibu Mkuu Chongolo awafikishie salaam za shukrani kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo Serikali anayoiongoza inavyoshirikiana na wakazi wa jimbo hilo kutengeneza mazingira mazuri ya wananchi kupata huduma na kujitafutia maendeleo kutokana na miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa jimboni humo, pia alizungumzia uwepo wa Skimu ya Umwagiliaji ya Singiwe, ambao umetengewa fedha za kuuboresha ili uongeze manufaa kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo mengine, katika kilimo.

Amesisitiza mradi huo ni mkubwa lakini unahitaji maboresho kidogo ili uweze kufanya kazi vizuri huku akitumia nafasi hiyo kueleza kuna kila sababu ya Wilaya ya Kalambo kufufua zao la Kahawa ambalo miaka ya zamani lililimwa kwa wingi na kahawa yake ilikuwa bora.

Katika ziara yake wilayani Kalambo Ndugu Chongolo alishiriki Mkutano wa Shina Namba 6, Singiwe, kutembelea na kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya, kutembelea na kukagua Bandari ya Kasanga, kukagua ujenzi wa Barabara ya Matai – Kasesya na kuzungumza na wananchi katika maeneo yote hayo, ikiwemo na Kisumba.


Share:

PROF. MKENDA: VYUO VIKUU VIJIKITE KWENYE TAFITI ILI KUTATUA CHANGAMOTO MBALIMBALI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametoa wito kwa vyuo vikuu kuzingatia ufanyaji wa tafiti zenye tija nchini ili kuchochea na kuleta ushindani katika gunduzi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Prof. Mkenda, ametoa wito huo leo Oktoba 9, 2023, wakati akilizindua baraza jipya la chuo Kikuu Huria cha Tanzania la 2023/2026 katika kituo cha chuo hicho mkoa wa Dodoma kilichopo jijini Dodoma.

“Vyuo vikuu havipimwi kwa wingi wa wanafunzi na wingi wa mapato, kuna vipengele vingi vya upimaji ubora wa elimu ya chuo kikuu mojawapo ni ufanyaji wa tafiti zenye kuleta gunduzi, kukuza maarifa na ujuzi katika jamii. Lazima chuo kikuu kiwe chemchem ya kuvumbua na kutafuta majibu ya kutatua matatizo ya wanachi kwa kufanya tafiti na kuja na majawabu. Chuo Kikuu ni mahali pa kuzalisha wataalamu na wabobezi ambao wakitoka wanakwenda kufanya kazi za kutoa huduma kwa wananchi na kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali.” Amesema Prof. Mkenda.

Aidha, aliendelea kusema kuwa tafiti zinazofanywa na vyuo vyetu ni vyema zikashindanishwa kimataifa ili ziweze kuwa na viwango vya ubora zaidi katika nyanja za kimataifa ili kuvifanya vyuo vyetu viwe na uwezo wa kufanya kazi na watu wa mataifa mbalimbali duniani. Ameeleza kwamba hivi karibuni wizara imetoa tuzo na fedha kwa watafiti ambao wamechapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida ya kimataifa kama motisha lakini pia kuwafanya watafiti wa Tanzania kushindana kimataifa. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimepongezwa kwa kazi nzuri ya kuendelea kuzalisha wataalamu na pia kufanya tafiti mbalimbali ambapo katika tuzo hizo mhadhiri mmoja kutoka Chuoni hapo alipata tuzo hizo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Joseph Kuzilwa, amemuhakikishia mhe. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwa baraza jipya lililoteuliwa ni la watu wenye taaluma na ujuzi wa kutosha kuweza kulisongesha mbele gurudumu la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

“Timu hii ya wajumbe itakuwa ni chachu kubwa katika kuchangia ufanisi wa baraza kwenye kusimamia chuo kwa mujibu wa majukumu yaliyoainishwa katika hati idhini ya chuo ya mwaka 2007, sheria ya vyuo vikuu ya mwaka 2005 na waraka namba moja wa msajili wa hazina wa mwaka 2023. Ufanisi katika usimamiaji wa mpango mkakati mpya wa chuo wa miaka mitatu 2023/24 hadi 2025/26 itakuwa ni moja ya kipimo cha baraza hili kwa kipindi chake cha miaka mitatu.” Amesema Prof. Kuzilwa.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema baraza hili jipya limepata fursa ya kupata mafunzo ya siku tatu ambapo wawezeshaji watatoa mada mbalimbali zitakazowawezesha wajumbe kujenga uwezo zaidi ili waweze kufanya kazi na kutimiza wajibu wao vizuri.

“Utendaji wa baraza hili utapimwa na ofisi ya msajili wa hazina kila mwisho wa mwaka, ndiyo maana tumekaa pamoja ili wajumbe waweze kujua vizuri wajibu, taratibu, haki na mamlaka waliyonayo ili waweze kufanya kazi kwa kukidhi matakwa ya sheria na kanuni zilizopo kuhusu utendaji wa bodi na mabaraza yaliyoko chini ya serikali.” Amesema Prof. Bisanda.

Akitoa historia ya Baraza hilo, Mwanasheria wa Chuo ambaye pia ni Katibu wa Baraza Wakili Nelly Moshi, amesema baraza hili lilianzishwa rasmi mwaka 1994 chini ya uenyekiti wa hayati Basil Mramba kama mwanzilishi na kufuatiwa na wenyeviti wengine kadhaa na mwaka 2022 chuo kiliweza kumpata Mwenyekiti wa sasa Prof. Joseph Kuzilwa kufuatia uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wajumbe wa Baraza jipya la chuo wanaendelea na mafunzo mpaka tarehe Oktoba 11, 2023 katika kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mkoa wa Dodoma.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger