Friday, 10 July 2020

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa July 10



















Share:

Thursday, 9 July 2020

Breaking : RAIS MAGUFULI AMEFANYA UTEUZI MWINGINE USIKU HUU LEO ALHAMIS



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Julai 9,2020 amefanya uteuzi wa Mkuu wa wilaya mmoja na Mkurugenzi Mtendaji mmoja kama ifuatavyo.


Rais Magufuli amemteua Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Advera Bulimba kuwa mkuu wa wilaya ya Nzega mkoani Tabora huku akimteua Solomon Isack Shati kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hanang mkoani Manyara.


Wakati huo huo, Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kept, (Mst) George Huruma Mkuchika kwa mamlaka aliyokasimiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya uteuzi wa Makatibu Tawala wa wilaya 2 kama ifuatavyo.


Mkuchika amemteua Omary Mwanga kuwa katibu tawala wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi huku akimteua Saitot Zelothe Stephen kuwa katibu tawala wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya.




Share:

RAIS MAGUFULI AOMBOLEZA KIFO CHA BALOZI JOB LUSINDE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiandika kwenye kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Waziri katika Baraza la kwanza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere Marehemu Balozi Job Lusinde aliyefariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Msemaji wa Familia ya Marehemu Balozi Job Lusinde, Waziri Mkuu Mstaafu John Samweli Malecela wakati alipokwenda kutoa pole nyumbani kwa Marehemu Balozi Lusinde Uzunguni jijini Dodoma leo tarehe 09 Julai 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na mke wa Marehemu Balozi Job Lusinde, Mama Sara Lusinde aliyekaa katikati mwenye kilemba cheupe mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kutoa pole nyumbani kwa Marehemu Balozi Lusinde Uzunguni jijini Dodoma.PICHA NA IKULU
Share:

DKT. EDMUND MNDOLWA ATAKA USHINDI MNONO KWA CCM UCHAGUZI MKUU

 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Edmund Mndolwa (wa pili kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Wilaya ya Manyoni, Robert Chalamaganza (kushoto) moja ya mzinga wa nyuki kati ya 20 yenye zaidi ya sh.milioni 1.2 ililiyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka jana kwa ajili ya kuanzisha mradi waufugaji nyuki katika Shule ya Sekondari ya Mkwese. Wengine ni Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Manyoni.
 Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Manyoni, Leah Gervas (kulia) akimvika skafu  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Edmund Mndolwa mara baada ya kuwasili kwa ziara ya siku moja wilayani humo mkoani Singida jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mkoa wa Singida, Mwalimu Ephraim Kolimba.
  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Edmund Mndolwa (kushoto) akisalimiana na Katibu wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Manyoni, Ally Omary.
Mwekezaji wa shule hiyo, Askofu Williams Wilson Yindi, akielezea historia fupi ya shule hiyo.

 Viongozi wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Manyoni wakijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mkoa wa Singida, Mwalimu Ephraim Kolimba (wa pili kuli)
 Mkutano ukiendelea.
  Mjumbe wa Mkutano Mkuu Wazazi Taifa, Focus Mushi, akizungumza. 
 Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka, akizungumza.
Katibu wa UVCCM, Mkoa wa Singida, George Silindu akizungumza.
 Katibu wa CCM Wilaya ya Manyoni, Dafroza Lucas, akizungumza. 
 Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Alexandrina Katabi, akizungumza.
 Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa, akizungumza. 
 Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mkwese wakiwa shuleni wakimsubiri kumpokeea Dkt. Mndolwa.
 Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida, Dkt. Denis Nyiraha, akizungumza. 
 Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, Yahaya Masere, akizungumza.
   Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Edmund Mndolwa, akipokea zawadi.
 Zawadi ya asali ikipokelewa.
 Zawadi ya asali ikipokelewa.
 Katibu wa UVCCM Wilaya ya Manyoni, Igembya Wambura, akimkaribisha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Edmund Mndolwa.
Vijana wa UVCCM Wilaya ya Manyoni wakifanya gwaride kabla ya kuvalishwa Skafu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Edmund Mndolwa.



NA DottoMwaibale, Manyoni

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Edmund Mndolwa amewataka wanachama wa jumuiya hiyo, kuhakikisha wanakipa ushindi CCM, wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba mwaka huu.

Mndolwa alitoa ombi hilo jana wakati akizungumza na wanachama wa jumuiya hiyo wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida katika ziara yake ya kikazi ya siku moja.

“Rais wetu Dkt.John Magufuli amefanya kazi kubwa ya kutuletea maendeleo hivyo zawadi kubwa ya kumpa ni kuhakikisha tunampa kura nyingi za kutosha wakiwemo wabunge na madiwani” alisema Mndolwa.

Alisema kujiandikisha katika daftari la wapiga kura hakutoshi kinachotakiwa ni siku ikiwadia ya kupiga kura kujitokeza kwa wingi kuanzia wakina mama, vijana nawanaume.

Katika ziara hiyo Mndolwa alikabidhi mizinga 20 ya nyuki aliyoitoa Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Daniel Mtuka kwa ajili ya kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki katika Shule ya Sekondari ya Mkwese yenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 1.2.

Pamoja na mambo mengine Mndolwa alizindua luninga iliyonunuliwa na mbunge huyo kwa ajili ya kuangalia wanafunzi wa shule hiyo, lengo likiwa ni kujifunza vipindi mbalimbali.

Katika hatua nyingine Dkt. Mndolwa amemhakikishia Mwekezaji wa shule hiyo, Askofu Williams Yindi atapewa mkataba wa kuindesha shule hiyo, inayomilikiwa na jumuiya ya Wazazi.

“Nikuhakikishie kuwa hadi ifikapo Augosti 15 mwaka huu kama hakutakuwa na hatua yoyote iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kupata mkataba wa uendeshaji wa shule hii baina yetu na wewe naomba nipigwe risasi ya kichwani” alisema Mndolwa.

Hatua ya Dkt.Mndolwa kutoa agizo hilo ilikuja baada ya mwekezaji wa sekondari hiyo kueleza kuwa ameboresha miundombinu ya shule ambayo ilikuwa imeharika, ikiwa ni pamoja na kuchimba visima vya maji, kuweka umeme, ukarabati wa majengo zikiwemo nyumba za walimu, madarasa, mashine ya kusaga, ununuzi wa vifaa vya kufundishia, kununua vifaa vya maabara na zana zingine.

“Mhe.Mwenyekiti uwekezaji nilioufanya katika shule hii unafika zaidi ya sh.milioni 80 lakini hadi leo hii sina mkataba wowote kati yangu na jumuiya ya wazazi, ambao ndio wamiliki wa shule.” AlisemaYindi.

Yindi aliongeza kuwa waliipokea shule hiyo januari 2019 ikiwanawanafunzi 40 na wafanyakazi 10 hadi kufia Machi, 2019 waliongeza wanafunzi 37 nakufikia 77, huku idadi ya wafanyakazi ikifikia 17, na mwaka huu wameongeza wanafunzi hadi kufikia 103 na wanatarajia kupata wanafunzi wengi zaidi kadri watakavyo zidi kuimarisha miundombinu ya shule na taaluma.

Aidha, Mndolwa aliomba wanachama wa jumuiya hiyo kujenga tabia ya kulipia kadi zao ili fedha zitakazo patikana zisaidie katika shughuliza za uendeshaji wa jumuiya hiyo ambayo haina vyanzo vingi vya mapato.




Share:

SERIKALI YAKUTANA NA WADAU KUTATUA CHANGAMOTO KATIKA KILIMO CHA MKONGE

strong>
Naibu Waziri Kilimo Mhe. Omari Mgumba,akizungumza na wadau wa Tasnia ya mkonge katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Royal Village Jijini Dodoma

Mwenyekiti wa Bodi ya Mkonge Bi Mariamu Mkumbi wakati akihutubia wadau wa Tasnia ya mkonge katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Royal Village Jijini Dodoma
Wakuu wa Mikoa mbalimbali wakisikiliza mawasilisho mbalimbali katika mkutano wa wadau wa tasnia ya mkonge uliofanyika leo Jijini Dodoma.

Naibu Waziri Kilimo Mhe. Omari Mgumba (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya wakifuatilia mjadala wakati wa mkutano wa wadau wa tasnia ya mkonge uliofanyika leo Jijini Dodoma.


Na.Alex Sonna, Dodoma

Serikali yakutana na wadau wa Mkonge nchini ili kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili tasnia ya hiyo ili kuongeza tija katika uzalishaji, ajira na kukuza sekta ya viwanda, pato la mkulima na Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo imebainishwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary wakati wa kufungua mkutano wa wadau wa mkonge nchini.

Aidha Mhe. Mgumba amesema kuwa serikali imeanda mikakati katika zao la mkonge ili kuongeza tija na uzalishaji kwa kuanzisha vitalu vya mbegu ya mkonge katika Halmashauri zote amabako zao la mkonge linastawi.

Mhe. Mgumba amesema kuwa kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Mlingano uzalishaji wa mbegu bora umeanza ili ziweze kuzalishwa kwa wingi.

Mhe. Mguma ameeleza kuwa serikali inafanya uhakiki wa mashamba ya Mkonge yaliyobinafsishwa ili yaweze kuzalisha mkonge kama ilivyokubaliwa kwenye mikataba.

Pia amesema kuwa selikari imejipanga Kutoa elimu kwa maafisa ugani katika vijiji na kata kwenye maeeo yanayolima mkonge ili kuwajengea uwezo wa kuwahudumia wanachi katika kulima zao la mkonge.

“serikali itaongeza Bajeti nakuwezesha Kituo cha Utafiti Mlingano kufanya utafiti wa aina mbalimbali za mbegu ya mkonge na kuzisambaza kwa wakulima bila kusahau Kulinda ardhi ya kilimo ili isibadilishwe matumizi ambapo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeshaanza kufanya maboresho katika Sera na Sheria zake”, ameweka wazi Mhe. Mgumba.

Mhe. Mgumba ameongeza kuwa watahakikisha wanahimiza na kushawishi wawekezaji kuwekeza mnyororo wa thamani wa Tasnia ya Mkonge hususan kwenye viwanda na teknolojia bora za uzalishaji wa bidhaa za mkonge ikiwemo magunia, mazuria, matofali, mapambo, n.k ili kupanua soko la ndani na nje.

Hata hivyo Mhe. Mgumba amesema kuwa watanzania kwa kushirikiana na serikali wanatakiwa kulinda viwanda vya ndani kwa kuongeza tozo na kodi kwa bidhaa mbadala wa mkonge zinazoingizwa hapa nchini kutoka nje ya nchi.

Naye Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Evarist Ndikilo ametoa wito kwa wadau wa mkonge kuwa wawazi katika mkutano huo ili baada ya kikao hicho basi wakatekeleze yale yatakayo kuwa yameamuliwa katika mkutano huo ili kufufua kilimo cha mkonge nchini na shabaha kubwa ikiwa ni kurudisha taswira ya zao hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mkonge Tanzania, Bi. Mariam Mkumbi amesema kuwa kutokana na zao la mkonge kuwa moja kati ya mazao saba ya kimkakati hapa nchini Pamoja na maelekezo ya serikali ya kuongeza uzalishaji wa zao la mkonge kutoka tani 36,000 mwaka 2019 na kufikia tani 120,000 mwaka 2025.

“Bodi ya Mkonge Tanzania imeandaamkakati wa kurudisha hadhi ya zao la mkonge kama ilivyo kuwa katika miaka ya 1960 ambapo Tanzania ilikuwa inaongoza kwa uzalishaji na ubora wa mkonge duniani”, ameeleza Bi. Mkumbi.

Bi. Mkumbi ameongeza kuwa uzalishaji huo unalenga kuhusisha takribani tani 62,331 kutoka kwa wazalishaji waliopo katika mashamba makubwa na tani 60,256.9 na zaidi ya hapo kutoka kwa wakulima wadogo katika mikoa 16 ndani ya kanda sita zilizoainishwa katika mpango huo wa ndani ya Tanzania Bara ambao watahamasishwa kpitia mpango huo.

Itakumbukwa kuwa zao la mkonge lina historia ndefu nchini kwani mwaka 1964 Tanzania iliweza kuzalisha jumla ya Tani 230,000 na kuongoza Duniani kwa uzalishaji wa zao la mkonge. Kipindi hicho mkonge ulikuwa unachangia asilimia 65% ya fedha za kigeni nchini.
Share:

MWALIMU WA KIKE ALIYEZUA GUMZO KUFANYA MAPENZI NA MWANAFUNZI WAKE WA DARASA LA 6 AFARIKI DUNIA


Aliyekuwa mwalimu katika jimbo la Washington ambaye uhusiano wake na mwanafunzi ulifanya akafungwa gerezani na kukashifiwa kote duniani ameaga dunia kwa ugonjwa wa saratani akiwa na umri wa miaka 58.

Mary Kay Letourneau alipatikana na hatia ya mauaji ya daraja la pili ya kubaka mtoto mwaka 1997 baada ya kupata ujauzito na Vili Fualaau alipokuwa na umri wa 12 au 13 na yeye alikuwa na umri wa miaka 34.

Alijifungua mtoto wao wa pili akiwa gerezani 1998.

Baada ya kumaliza kifungo chake, wanandoa hao walioana 2005, hatahivyo, walitengana baada ya miaka 12.

Waliki wa Bi. Letourneau, David Gehrke ameviambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba Bi. Letourneau amekufa nyumbani kwake akiwa na watoto wake na Bwana Fualaau.

Bi. Letourneau alikuwa mama aliyeolewa na watoto wanne wanaoishi Seattle alipoanza uhusiano na mwanafunzi wake wa darasa la sita.

Awali, alihudumia kifungo cha miezi kadhaa tu gerezani lakini baada ya kuachiliwa huru alipatikana akifanya ngono tena na kijana huyo huyo mdogo.

Mama huyo aliyekuwa mwalimu alirejeshwa tena gerezani na kuhudumia kifungo cha miaka saba. Binti zake wawili aliopata na kijana Fualaau awali walitunzwa na familia ya mume wake.

Inasemekana kwamba mama huyo amekuwa mgonjwa kwa miezi sita kabla ya kutokea kwa kifo chake.

Mama huyo alikuwa mkatoliki na ni binti ya aliyekuwa mbunge wa Republican, John G. Schmitz. Lakini taaluma ya baba yake kisiasa ilifikia ukingoni baada ya kujitokeza kwa kashfa ya kwamba alikuwa na watoto wawili nje ya ndoa.

 Chanzo - BBC Swahili
Share:

BENKI YA 1&M TANZANIA YATIA FORA SABASABA

Kutoka kushoto ni Mkuu wa Huduma za Rejareja wa Benki ya I&M Tanzania, Lilian Mtali, Meneja Masoko na Mawasiliano, Anitha Pallangyo, Ofisa Mauzo, Beatrice Fusi, Meneja Mwandamizi (Madeni na Maendeleo ya Bidhaa), Deepali Ramaiya, Meneja wa Tawi la Nyerere, Said Gagu na Ofisa Masoko na Mawasiliano, Debora Mwakyoma wakiwa katika Maonyesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, Dar es Salaam.
 
Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

BENKI ya I&M Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, lakini inang’ara kwa kutoa bidhaa na huduma za kipekee ambazo zinakidhi mahitaji yote ya mteja katika soko.

I&M Tanzania ilitambulisha akaunti mpya ya wanawake ya Tunaweza inayotoa suluhisho kwa wanawake wa ngazi zote kuanzia mmoja mmoja, wajasiriamali hadi kikundi au taasisi.

Akaunti hiyo inajitofautisha kwa kutoa huduma bila malipo yoyote, haina makato ya kila mwezi na viwango vyake vya riba vinavutia kwenye akiba.



Akizungumza leo jijini Dar es Salaa, katika maonyesho hayo, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Benki ya I&M, Anitha Pallangyo, alisema kuwa bidhaa hiyo mpya imeunganishwa kwenye mtandao wa benki wa kidijitali ili kuwapa wateja huduma bora na endelevu wakati wowote wanapohitaji.

Amesema I&M Tanzania ni sehemu ya I&M Holdings Kenya iliyoanzishwa mwaka 1974 kama kampuni ya huduma za kifedha kabla baadaye kubadilishwa kuwa benki ya biashara.

“Mwaka huu inasherehekea miaka kumi ya huduma zetu katika soko la Tanzania. Tunafurahi kuendelea kuhudumia wateja wetu na wateja wapya, pia tunashukuru wateja wetu na washikadau wote walioshiriki katikakuiletea benki mafanikio makubwa kwa kipindi chote cha miaka kumi kwenye soko.”

“Tunatoa huduma kadhaa za kifedha ikiwa ni pamoja na akaunti ya akiba, current akaunti kwa madhumuni ya biashara, mikopo ya biashara, huduma za kubadili fedha, uhamishaji fedha kitaifa na kimataifa, huduma za kidijitali ambazo hutoa fursa kwa mteja kupata huduma za benki kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *150*32# au kupitia iClick- huduma ya benki kwa njia ya mtandao inayopatikana bila kikomo kwa saa 24,” amesema Anitha

Meneja Masoko na Mawasiliano huyo wa benki hiyo, amesema kuwa pia benki yao wanatoa unafuu na urahisi wa kupata mikopo na huduma nyingine kadhaa ambazo ziliwafanya watu waliotembelea banda lake kwenye maonyesho ya Sabasaba lililopo ukumbi wa Karume, upande wa kulia wa lango la kuingilia kuhamasika na kutaka kujua zaidi kuhusu benki hiyo.

“I&M inafungua milango kwa Watanzania wote kwenda kujiunga na benki inayojali mahitaji yao, iliyo tayari kuwapa huduma za kipekee za kifedha kupitia wafanyakazi wake wenye uzoefu zaidi katika kutoa huduma bora kwa wateja.

“Mbali na kushiriki katika maonyesho ya Sabasaba, benki hiyo inatoa huduma zake bora kupitia mtandao wa matawi yake yaliyoko maeneo ya Maktaba, Indira Gandhi, Nyerere, Kariakoo, Oysterbay pamoja na mikoani ikiwa ni pamoja na Moshi, Arusha na Mwanza,” amesema


 Timu ya wafanyakazi wa mauzo na idara ya masoko wa benki hiyo kutoka matawi yake ya Dar es Salaam inayoongozwa na Meneja Masoko na Mawasiliano wa Benki ya I&M, Anitha Pallangyo na Ofisa Masoko na Mawasiliano, Debora Mwakyoma wapo kwenye maonyesho hayo ili kuwapa wageni na wale ambao wanataka kuwekeza katika benki inayoaminika na salama ikiwa na huduma za ATM zinazopatikana kwa saa 24.
Share:

Serikali Yaanzisha Kanda Mpya Ya Wakala Wa Taifa Wa Hifadhi Ya Chakula (Nfra) Songwe -Waziri Hasunga Abainisha Sababu

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Serikali imetangaza kuanzisha Kanda mpya ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula-NFRA katika mkoa wa Songwe itakayohudumia mikoa ya Songwe na Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika eneo la Vwawa Mkoani Songwe jana tarehe 8 Julai 2020 Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amasema kuwa Mkoa wa Songwe ulishika nafasi ya tatu Kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya chakula nchini katika msimu wa 2018/19 hivyo Kutokana na uzalishaji huo mkubwa wa chakula, Serikali imeona ipo haja ya kuanzisha Kanda ya NFRA katika Mkoa wa Songwe, tofauti na hapo awali ambapo katika eneo la Vwawa kulikuwa na Kituo kidogo cha NFRA ambacho kilikuwa chini ya Kanda ya NFRA Makambako.

Waziri Hasunga amesema kuwa Kanda ya NFRA Songwe imeanzishwa rasmi tarehe 01 Julai, 2020 ambapo Kuanzishwa kwa Kanda hiyo kumetokana na hali ya uzalishaji mkubwa wa chakula katika Mikoa ya Songwe na Mbeya, pamoja na kujengwa kwa Maghala na Vihenge vya Kisasa ambavyo vitaongeza uwezo wa uhifadhi kutoka tani 17,000 za awali na kufikia tani 37,000.

Akizungumzia kuhusu msimu wa ununuzi wa kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Waziri huyo Japhet Hasunga anayehudumu katika serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli akihudumia sekta ya kilimo amesema kuwa katika Kituo cha Vwawa, zoezi la ununuzi wa mahindi limeanza rasmi tarehe 06 Julai, 2020.

Ameongeza kuwa kwa sasa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula-NFRA umeanza na ununuzi wa tani 10,000 na utanunua kwa bei ya Tsh 550 kwa kilo.

Kadhalika, amesema kuwa Wakala utaendelea kuongeza kiasi cha ununuzi kadri utakavyopata fedha kutoka Serikalini. Ambapo hata hivyo amesema mtu yeyote anaruhusiwa kuuza mahindi NFRA bila kujali upendeleo wowote ilimradi mahindi hayo yawe na ubora unaotakiwa.

MWISHO


Share:

CCM YAANIKA MAJINA YA WANACHAMA 10 WALIOTIA NIA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA SHINYANGA MJINI


Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Ahmedi Bwanga

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga Mjini kimetangaza majina ya Wanachama 10 wa CCM waliotia nia ya kugombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM.

Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Ahmedi Bwanga  amesema hadi leo asubuhi Alhamis Julai 9,2020 jumla ya Wanachama wa CCM 10 wamejitokeza kutia nia kugombea kiti cha Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini na kueleza kuwa zoezi la kuchukua Fomu kugombea ubunge litafanyika Julai 14,2020 hadi Julai 17,2020.

Bwanga amewataja waliojitokeza kutia nia ya kuwania ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kuwa ni Stephen Julius Masele, Dotto Joshua, Erasto Kwilasa, Bandora Salum Mrambo, Wilbert Masanja, Severine Luhende Kilulya, Jonathan Manyama, Lydia Winga Pius, Mary Izengo na Eunice Jackson.
Share:

Breaking News : CCM SHINYANGA MJINI YAWASIMAMISHA UONGOZI MAKADA 12 WA CCM WALIOKAMATWA NA TAKUKURU



Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Ahmedi Bwanga akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamis Julai 9,2020  kuhusu kusimamishwa uongozi Viongozi 12 wa UWT/CCM kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Ahmedi Bwanga akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamis Julai 9,2020  kuhusu kusimamishwa uongozi Viongozi 12 wa UWT kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga Mjini kimewasimamisha uongozi Viongozi 12 wa CCM kwa tuhuma ya kujihusisha na vitendo vya rushwa  kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamis Julai 9,2020, Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Ahmedi Bwanga amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha kamati ya siasa ya wilaya ya Shinyanga Mjini kilichoketi Julai 8,2020 kutoa mapendekezo na maazimio mbalimbali. 

“Chama Cha Mapinduzi kimepokea taarifa mbalimbali kutoka vyombo vya dola ambazo zinatusikitisha za baadhi ya viongozi wetu wa Chama wamekiuka sheria na taratibu zetu za chama tulizojiwekea kwa kujihusisha na masuala ya rushwa. CCM imechukua hatua kali ili iwe fundisho kwa wale wengine ambao hawataki kubadilika”,ameeleza Bwanga.

“Katika kikao chetu cha kamati ya siasa ya wilaya ya Shinyanga Mjini kilichoketi Julai 8,2020 kilitoa mapendekezo na kuazimia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha uongozi/nyadhifa zao zote wale wote waliohusishwa na vitendo vya rushwa katika kata ya Ngokolo,waliokamatwa na TAKUKURU mpaka pale tutakapopata taarifa ya uchunguzi kamili kutoka vyombo vya dola itakayoeleza kuwa hawana makosa na baadae kitajua nini cha kufanya”,amefafanua Bwanga.

Amewataja viongozi wa UWT/ CCM waliosimamishwa uongozi kuwa ni Hulda Malsaba (Mwenyekiti wa UWT Kata ya Ngokolo), Pendo Mhapa (Katibu wa UWT Kata ya Ngokolo), Zulfa Hassan (Mwenezi kata ya Ngokolo), Jackline Isaro (Mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UWT wilaya ya Shinyanga Mjini) na Asha Mwandu (Mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM taifa na Mjumbe wa kamati ya utekelezaji Wazazi mkoa wa Shinyanga).

Wengine ni Moshi Ndugulile (Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji UWT wilaya ya Shinyanga Mjini), Elizabeth Hange (Katibu wa UWT tawi la Ngokolo), Tabu Shaban (Katibu UWT tawi la Ngokolo), Tabu Said (Mwenyekiti tawi la Majengo Mapya),Happy Chikala (Katibu UWT tawi la Mwadui),Elizabeth Buzwizwi (Mwenyekiti UWT tawi la Majengo Mapya) na Elizabeth Benjamini (Mwenyekiti UWT tawi la Mwadui).

Julai 1,2020 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga ilitoa taarifa kwa vyombo ya habari kuhusu kumshikilia Mjumbe wa CCM Mkutano Mkuu Taifa CCM, Asha Mwandu Makwaiya Mkazi wa Majengo Mapya Mjini Shinyanga Juni 28,2020 kwa kosa la kutoa rushwa kwa wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT). 

TAKUKURU ilieleza kumkamata Bi. Asha Mwandu Makwaiya ambaye ni mkazi wa Majengo Mapya Shinyanga Mjini na Mjumbe wa CCM Mkutano Mkuu Taifa akiwa nyumbani kwa Elizabeth Donald Itete ‘Mama Buzwizwi’ ambaye ni Katibu wa UWT tawi la Mshikamano pamoja na wajumbe wengine 10 ambao ni viongozi wa UWT kata ya Ngokolo. 

“Bi. Aisha Mwandu Makwaiya alitaka kugawa mashuka 10, kitenge kimoja, ndala 11 kwa wajumbe 11 wa umoja wa Jumuiya ya Wanawake CCM (UWT) kata ya Ngokolo kama kishawishi cha yeye kuchaguliwa au kuchaguliwa kwa aliyemtuma”,alisema Mkuu huyo wa TAKUKURU.


Share:

Waziri Mkuu wa Ivory Coast afariki dunia ghafla

Waziri Mkuu wa Ivory Coast, Amadou Gon Coulibaly, amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia leo Alhamisi akiwa na umri wa miaka 61.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kumnukuu Rais Alassane Ouattara wa Kodivaa akitangaza jana usiku kwamba Ivory Coast imeingia kwenye msiba wa kuondokewa ghafla na Coulibaly.

Aidha amesema, Waziri Mkuu Coulibaly alishiriki kwenye kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri la serikali ya Kodivaa, hali yake ikawa mbaya na amefariki dunia hospitalini.

Mwezi Machi mwaka huu, Coulibaly aliteuliwa na chama tawala wa Ivory Coast kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho ili kumrithi Rais Alassane Ouattara.
 
Waziri Mkuu huyo alirejea nchini Kodivaa tarehe pili mwezi huu wa Julai baada ya kupitisha muda mrefu wa matibabu nchini Ufaransa. Aliwahi kufanyiwa operesheni ya moyo mwaka 2012.

Ouattara amemtaja Colibaly kwamba alikuwa mtu wake wake wa karibu mno katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Haikuweza kujulikana haraka ni nani atateuliwa kushika nafasi yake ya kugombea urais wa tiketi ya chama tawala katika nchi hiyo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa cocoa duniani.


Share:

Watiania Ubunge Wa CCM Mkoa Wa Iringa Waonywa Kuzingatia Sheria Na Kanuni Za Chama

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.
KAMATI ya siasa ya chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Iringa imewata watiania na wanachama kuheshimu kanuni na sheria za uchaguzi zilizowekwa ndani ya chama ili kuepuka panga linaloweza kujitokeza pindi watakapo kiuka taratibu za chama.

Mwenyekiti wa kamati ya siasa Mkoa wa Iringa Abel Nyamahanga ameyasema hayo wakati akizungumza na wandishi wa habari katika ukumbi wa ccm mkoa wa Iringa na kusema kuwa watia nia wanatakiwa kupita ofisi za wasimamizi wa uchaguzi ili kupewa taratibu za uchaguzi.

Nyamahanga alisema chama hakitasita kumchukulia hatua mwanachama na mtia nia ambaye atakiuka sheria na taratibu za uchaguzi.

Alisema kuwa kila kitu kinachofanywa na chama cha mapinduzi kipo kwenye kanuni za uchaguzi za chama hicho hivyo watia nia kwenye ngazi za udiwani na ubunge wanatakiwa kufuata kanuni hizo ili waweze kutia nia bila kuwa na kashfa.

“Tunacho kizungumza hapa kila kitu kipo kwenye miongozo na kanuni za chama chetu cha mapinduzi (CCM) ndio maana tunawataka watia nia wote kufuta kanuni na taratibu za chama wakati wa nia yake ya kutafuta nafasi ya kuwatumiakia wananchi” alisema Nyamahanga

Nyamahanga aliwataka wanachama na watia nia wote kuheshimu kanuni za uchaguzi ndani ya chama cha mapinduzi ili kuondokana na tatizo la rushwa ambalo miaka mingi kipindi cha uchaguzi ndio huaribu taswiara ya chama cha mapinduzi.

Aidha Nyamahanga aliwataka watia nia waache mara moja kupita kwenye kata na matawi kwa lengo la kukutana au kuwasalimia wapiga kura badala yake wanatakiwa kupita katika ofis za wasimamizi wa uchaguzi ili wapate taratibu na mwenendo wa uchaguzi unaokubarika ndani wa chama hicho.

 Alisema wapo baadhi ya watia nia wamekuwa wakiwakusanya  wapiga kura kutoa maeneo mbalimbali kwa kisingio cha kuwasalimia,kujitambulisha  na kuwapa nauli ikithibitika kwa mgombea yoyote yule ataondolewa kwenye orodha ya wagombea kwa mujibu wa ibara ya 35 kifungu kidogo cha kumi na sita.

Kwa upande wake mjumbe wa halmashauri kuu (CCM) Taifa Salim Asas alisema kuwa serikali ya chama cha mapinduzi imeleta maendeleo kwa wananchi hivyo wanauhakika wa ushindi katika uchaguzi mkuu.

Alisema kuwa chama cha mapinduzi mkoa wa Iringa kitashinda kwa kishindo majimbo yote hata jimbo la Iringa mjini ambalo lipo upinzani nalo watashinda kwa kuwa chama hicho kimejipanga vilivyo kuhakikisha hakuna makundi ili kuhakikisha kwenye uchaguzi mkuu wanaenda kwenye uchaguzi wakiwa wamoja.

Aliongeza kuwa wananchi wa manispaa ya Iringa wamekuwa na imani na utendaji wa kazi wa chama cha mapinduzi hivyo itakuwa kazi nyepesi kushinda kwa kuwa wanauhakika wa kumpata mgombea mwenye uwezo wa kupeperusha pendera ya chama hicho.


Share:

Waziri Kairuki Ahamasisha Kilimo Cha Pamoja Same

Na Dixon Busagaga ,Same.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angela Kairuki,ameutaka uongozi  wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, kuhamasisha wananchi kulima kilimo cha pamoja,hususani yale mazao yenye uhitaji mkubwa katika viwanda, ili kuwezesha kilimo chenye tija na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Kairuki ametoa Rai hiyo jana, wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo, ambapo alisema kilimo cha pamoja kina manufaa makubwa kwa wakulima kwa kuwa wawekezaji wataweza kukununua mazao mengi kwa pamoja, na hivyo kuinua uchumi.

Kairuki alisema, yapo mazao yenye uhitaji mkubwa katika viwanda mbalimbali nchini, akitolea mfano wa  zao la Mtama, ambapo alisema kampuni ya Kilimanjaro Biochem (KBL) iliyopo wilayani Mwanga, ina mahitaji ya zaidi ya Tani 6,000 hivyo ni dhahiri , kuwa soko la uhakika litapatikana, endapo wakulima watalima kilimo cha pamoja na kuzalisha zao hilo kwa wingi.

“Wilaya ya Same ina fursa nyingi za Kilimo, kutokana na ardhi yake kuweza kustawisha mazao ya aina nyingi tofauti na maeneo mengine, kwani yapo maeneo ya umwagiliaji ambapo wanaweza kulima kilimo cha umwagiliaji na maeneo mengine makubwa ya kilimo kingine, hivyo hamasisheni kilimo cha pamoja chenye tija”alisema Kairuki

Mbali na hilo,  Kairuki  alitaka pia Wilaya hiyo,  kujenga makumbusho ya Madini, ambayo watalii pamoja na wananchi watatembelea na kujionea madini mbalimbali ambayo yanapatikana wilayani humo.

“Fursa ya madini ni kubwa katika Wilaya hii, sasa wekeni mkazo kwenye utafiti ikiwezekana iwe kijiji kwa kijiji na kuwepo na maduka ya kuuzia vifaa vya uchimbaji ikiwemo baruti”

Aidha katika kupanua wigo wa uwekezaji, Katika wilaya hiyo,Kairuki alisema ipo haja ya kuangaliwa uwezekano wa kuanzishwa kwa machinjio ya kisasa, katika Wilaya hiyo,akieleza kuwa ipo mifugo mingi na endapo itaanzishwa machinjio, itakuwa fursa nzuri ya uwekezaji katika Halmashauri hiyo.

“Suala la kuanzisha machinjio, liende sambamba na upatikanaji wa mbegu bora za mifugo, pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa machinjio ili kuwawezesha kuitumia na kuleta tija kwa Wilaya”alisema Kairuki.

Katika hatua nyingine,Kairuki aliutaka pia uongizi wa Wilaya hiyo, kushughulikia migogoro ya Ardhi hususani ile inayohusu wananchi na wawekezaji kwa haraka, ili kuweza kutoa muafaka na kuwezesha uwekezaji kuendelea kwa tija.

“Mwekezaji anapofika mahali akakutana na migogoro, inamchelewesha kuanza kazi zake, lakini pia inakwamisha kasi ya uwekezaji, hivyo hakikisheni mnashughulikia migogoro kwa haraka iwezekanavyo, ili kupanua wigo wa uwekezaji”

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule,alisema wakulima kulima zao moja katika eneo moja, itawarahisishia wanunuzi kupata mazao wanayohitaji kwa wingi, na hivyo kuwa na masoko ya uhakika.

“Wakulima wanapolima mmojamoja  au mazao ya aina tofauti katika eneo moja,hayana tija kwao wenyewe na pia kwa serikali, pindi inapotarajia kuuza zao moja kwa Wingi kwa wakati mmoja, lakini inapotokea tukasema kata fulani ni ya zao fulani, wanaweza kukusanya mazao yakauzwa kwa pamoja na kuleta Tija”alisema Senyamule.


Share:

Nafasi za Ajira katika Shirika la Kazi Duniani




Share:

SERIKALI KUJENGA KITUO KIKUBWA CHA UKUZAJI VIUMBE MAJI CHATO


Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Charles Kabeho akizungumza na ujumbe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi ya ujenzi ya Corporation sol uliofika ofisini kwake muda mfupi kabla ya kuelekea kijiji cha Rubambangwe ambako kitajengwa kituo kikubwa cha kukuzia viumbe Maji.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dokta Rashid Tamatamah (Kulia) akionesha mipaka ya eneo kinapotarajiwa kujengwa kituo cha kukuzia viumbe hai katika kijiji cha Rubambangwe wilayani Chato muda mfupi kabla ya kukabidhi eneo hilo kwa mkandarasi (Corporation Sol) ili aweze kuanza ujenzi wa kituo hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dokta Rashid Tamatamah (kulia) akikabidhi mkataba na michoro ya majengo ya kituo cha kukuzia viumbe maji kwa Meneja wa Kampuni ya Corporation Sol Bw. Simeo Machibya Wilayani Chato (Geita).


Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia sekta ya Uvuvi imeikabidhi kampuni ya ukandarasi ya Serikali ya Corporation Sol eneo naf mkataba wa Ujenzi wa Kituo kikubwa cha Ukuzaji wa Viumbe Maji ili kazi hiyo ianze mara moja.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika leo (08.07.2020) katika kijiji cha Rubambangwe kilichopo Wilaya ya Chato mkoani Geita yalifanywa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dokta Rashid Tamatamah ambaye mbali na kubainisha kuwa mradi huo utakuwa ni mkubwa kuliko yote hapa nchini, pia alielezea maeneo kadhaa yatakayohusiana na mradi huo.

Dokta Tamatamah alisema kuwa mradi huo utajumuisha ujenzi wa mabwawa yatakayokuwa na uwezo wa kutoa zaidi ya tani 10 kwa mwaka, jengo la vitotoleshi vya samaki ambalo litakuwa na uwezo wa kutoa vifaranga zaidi ya milioni mbili kwa mwaka, jengo dogo la kutengeneza chakula cha samaki na eneo la kuhifadhia samaki hao.

Aliongezea kuwa mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.8 mpaka kukamilika kwake na tayari Wizara ilishalipa fidia ya shilingi milioni 42 kwa wakazi waliokuwa wakifanya shughuli zao za kiuchumi katika maeneo hayo yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 28.

“Lakini pia hapa litajengwa darasa, bweni na ukumbi wa chakula kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wakuzaji viumbe maji wanaohitaji kujifunza au kuongeza ujuzi wa taaluma hiyo kwa kozi fupi za wiki mbili au tatu” Alisistiza Dokta Tamatamah.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe Maji ambao ndio wasimamizi wakuu wa kituo hicho pindi kitakapoanza kufanya kazi, Bw. Nazaeli Madala alisema kuwa kituof hicho kitakuwa ni ufumbuzi wa changamoto ya uchache wa samaki wanaopatikana kwenye vyanzo vya asili.

“Kituo hiki kitahudumia mikoa yote inayozunguka kanda ya ziwa na maeneo jirani na ukanda huo na tutawafundisha wafugaji wa samaki, maafisa ugani wa fani ya ufugaji wa samaki na pia kitatumika kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma katika ngazi mbalimbali huko vyuoni” Aliongeza Madala.

Madala alibainisha kuwa kituo hicho kitawasaidia kupata muongozo wa kujenga vituo vingine katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika, Nyasa na maeneo ya Pwani lengo likiwa ni kuhakikisha viwanda vyote vya samaki vilivyopo nchini havikosi malighafi.

Naye Afisa Mtendaji wa kijiji cha Rubambangwe Bi. Restituta Majura alisema kuwa mradi huo utawanufaisha sana wakazi wa kijiji hicho kwani mbali na kutoa ajira kwa wananchi watakaoshiriki kwenye hatua ya ujenzi, pia wanatarajia kunufaika na uwepo wa barabara itakayoelekea eneo la mradi kwani pia itawasaidia kufika kwenye zahanati ya kijiji inayoendelea kujengwa hivi sasa.

Kabla ya kuelekea kwenye eneo la ujenzi wa kituo hicho, Dokta Tamatamah akiwa na timu yake ya wataalam kutoka Wizarani walifika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Charles Kabeho ambaye aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kupeleka mradi huo kwenye Wilaya yake na kuahidi kufuatilia kwa ukaribu hatua zote za ujenzi wa kituo hicho hadi kitakapokamilika mnamo mwezi Oktoba mwaka huu.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger