Saturday, 12 January 2019
SINGIDA UNITED YASAJILI MAKOCHA WAWILI KUTOKA SERBIA
Uongozi wa klabu ya Singida United umeamua kuvunja benki kwa kuwasajili Makocha wawili kutoka Serbia kwa ajili ya kuifundisha timu hiyo.
Popadic Dragan ambaye ni Kocha Mkuu ameamua kuja na mwenzake ambaye atakuwa Msaidizi, Dusan Momcilovic.
Usajili wa makocha hawa umefanikiwa ikiwa ni baada ya klabu hiyo kutokuwa na Kocha Mkuu tangu kuondoka kwa Hans Van Der Plujim ambaye alitimkia Yanga.
Pengine Singida wameamua kuboresha benchi la ufnudi kwa ajili ya michuano ya SportsPesa Super CUP itakayokuja hivi karibuni.
KIUNGO WA CHELSEA AJIUNGA MONACO

Kiungo wa klabu ya Chelsea, Cesc Fabregas, amejiunga na klabu ya Monaco, kwa mkataba wa miaka mitatu na nusu.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 amejiunga na timu hiyo kuungana na nyota mwenzake wa zamani wa klabu ya Arsenal, Thienry Henry, ambaye kwa sasa ndio kocha wa Monaco.
Kiungo huyo tangu awasili Maurizio Sarri, katika klabu ya Chelsea, amekuwa na mgumu sana kupata nafasi tayari msimu huu ameanza michezo sita tu kwenye ligi kuu England.
Fabregas, ameshinda mataji mawili ya ligi kuu England ,na kombe la FA Cup mara mbili.
SIMBA QUEENS , YANGA PRINCESS KUCHUANA VIKALI LIGI KUU YA SOKA LA WANAWAKE “SERENGETI LITE”
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Wanawake, Amina Karuma akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani ) wakati wa kutangaza mchuano wa ligi kuu ya soka la wanawake ya SERENGETI LITE kati ya Klabu za Simba Queens na Yanga Princess ambazo zinatarajia kukutana kwenye mchezo utakaochezwa Jumapili, Januari 13,2019.Kushoto kwake ni Afisa masoko wa kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Bw. George Mango na kulia kwake ni Kocha wa Yanga Princess Hamis Kinonda.
Afisa masoko wa kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza mchuano wa ligi kuu ya soka la wanawake ya SERENGETI LITE kati ya Klabu za Simba Queens na Yanga Princess ambazo zinatarajia kukutana kwenye mchezo utakaochezwa Jumapili, Januari 13,2019.Kulia kwake Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Wanawake, Amina Karuma na kushoto kwake ni Kocha wa Simba Queens Omari Mbweze.
Nahodha wa Simba Queens Mwanahamis Omar akiongea na waandishi wa habari jinsi walivyojiandaa na Mchezo huo wa watani wa jadi hapa nchini Klabu za Simba na Yanga zinatarajia kukutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite utakaochezwa Jumapili, Januari 13,2019
Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la Wanawake hapa nchini Klabu za Simba na Yanga zinatarajia kukutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite utakaochezwa Jumapili, Januari 13,2019.
Mchezo huo utachezwa saa 10 Jioni katika Uwanja wa Karume, Ilala makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Ligi kuu ya wanawake inadhaminiwa na kinywaji cha Serengeti Premium Lite kwa msimu wa pili mfululizo.
Katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa, kiingilio kitakuwa shilingi 2,000. Mashabiki wanahakikishiwa usalama huku vyombo husika vikihakikisha mchezo salama bila bughudha ya aina yoyote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Wanawake, Amina Karuma, akizungumza kuelekea mchezo huo amesema msimu huu umeanza kwa msisimko mkubwa na ushindani wa aina yake hivyo ni matarajio yake kuwa mchezo huo wa watani wa jadi utaakisi ubora wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite.
“Mchezo huo unaingia kwenye rekodi za Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite kwa kuwa ndio mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizo tokea kuanza kwa soka la Wanawake hapa nchini,” alisema Amina.
Aidha amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo na kujiona vipaji pamoja na ushindani wa hali ya juu kutoka pande zote za mchezo.
Naye Afisa masoko wa Serengeti Breweries Bw. George Mango amewahakikishia wadau wa soka la wanawake, mashabiki wa mpira wa miguu kuwa kinywaji cha Serengeti Lite kimejidhatiti kuhakikisha wanapata burudani ya hali ya juu kupitia mchezo huo kama ilivyokuwa kwa michezo mingine iliyotangulia.
“Mashabiki wakae tayari kuona namna kinyaji cha Serengeti Lite kilivyo tayari kuwaletea burudani ya hali ya juu kwenye mechi hii ya kusisimua,” amesema Mango.
Serengeti Premium Lite ni bidhaa ya kwanza Tanzania kujitokeza kudhamini ligi ya wanawake, na imejidhatiti kusaidia kupandisha viwango vya ligi hii kupitia kupitia udhamani, matangazo kwenye magazeti pamoja na viwanjani.
Bia ya Serengeti Premium Lite inadhamini Ligi Kuu ya Wanawake kwa kitita cha Shilingi 450 milioni kwa kipindi cha miaka mitatu.
SIKU ZA CAG ZAHESABIKA
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.
Ni siku tisa zimebakia kabla ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kuhojiwa na Kamati ya Maadili, Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kama ambavyo alitakiwa kufanya hivyo na Spika Job Ndugai.
Sababu pekee ambayo inamfanya Mtaalamu huyo wa Uhasibu na Ukaguzi kujieleza kwa kamati hiyo, ni juu ya kauli yake kuwa Bunge halifanyi kazi yake kama linavyotakiwa na hasa kwenye kupambana na ufisaidi.
Akitangaza uamuzi wa kumuita kiongozi huyo Spika Job Ndugai alimtaka kufika Januari 21 Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa na alisema endapo kiongozi huyo hatofika atatafutwa kwa njia yeyote ili afike kwenye kamati hiyo.
Akijibu swali ambalo lilimfanya ajikute kwenye kadhia hiyo ya kuitwa na Bunge Profesa Assad alisema,
“kama tunatoa ripoti na kuna ubadhirifu na hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa lisimamie na kuhakikisha kwamba pale penye matatizo, linahakikisha kuwa hatua zinachukuliwa. Sasa, sisi kazi yetu ni kutoa ripoti tu,”
“Na huo udhaifu, nafikiri ni jambo la kusikitisha, lakini ni jambo ambalo tunaamini muda si mrefu litarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa. Na sitaki kuwa labda nasema jambo hili kwa sababu linahusisha watu fulani, hapana. Lakini nafikiri Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata udhaifu ambao unaonekana, utakwisha.” alisema Assad
Chanzo:Eatv
MATOKEO YA UCHAGUZI DRC KUPINGWA MAHAKAMANI

Mgombea wa upinzani aliyeshindwa katika uchaguzi wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo Martin Fayulu.
Mgombea wa upinzani aliyeshindwa katika uchaguzi wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) uliofanyika Disemba 30 ameapa kuyapinga matokeo mahakamani.
Martin Fayulu ameiambia BBC kuwa raia wa Congo wanastahili kujua ukweli wa uchaguzi, mabao ameutaja kuwa ni "mapinduzi".
Mgombea mwengine wa upinzani Felix Tshisekedi, alitangazwa kuibuka na ushindi katika kinyang'anyiro hicho, lakini kumekuwa na tuhuma kuwa mshindi huyo ameingia makubaliano ya kisiasa na rais aondokaye Joseph Kabila.
Tayari watu kadha wanaripotiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa toka matokeo hayo yalipotangazwa.
Uchaguzi huo unakamilisha safari ya miaka 18 madarakani ya Joseph Kabila.
Matokeo hayo, endapo yatathibitishwa, yataweka historia ya makabidhiano ya amani ya hatamu za uongozi toka nchi hiyo ilipopata uhuru wake toka kwa wakoloni wa Ubelgiji mwaka 1960.
Kanisa lenye ushawishi mkubwa la Katoliki ambalo lilikuwa na waangalizi wa uchaguzi 40,000 limesema matokeo yaliyotangazwa hayaendani na matokeo waliyonayo.
Chanzo:Bbc
MANARA KUJICHANGANYA NA MASHABIKI TAIFA LEO
Afisa Habari wa Simba, Haji Manara.
Afisa Habari wa Simba, Haji Manara ametoa ahadi kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo watakaojitokeza katika Uwanja wa Taifa leo itakapopambana na JS Saoura ya Algeria katika mchezo wa Klabu Bingwa Barani Afrika.
Katika mchezo huo, manara amesema kuwa atajichanganya pamoja na mashabiki katika siti za mzunguko ili kuwahamasisha kuishangilia timu yao ili ipate ushindi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Manara amesema, "watu wangu wa nguvu leo nakaa na nyinyi mzunguko!. Tunachinja mwanzo mwisho!, tunahanikiza wote kwa 'Yes We Can'!. Mniwekee nafasi upande wa kaskazini".
Simba inaanza kampeni yake ya hatua ya makundi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika katika kundi la D, lenye timu za JS Saoura ya Algeria, AS Vita Club ya Congo na Al Ahly ya Misri.
ZANZIBAR WAADHIMISHA KUMBUKUMBU YA SIKU YA MAPINDUZI
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anahutubia taifa leo katika kilele cha miaka 55 ya mapinduzi matukufu kwenye Uwanja wa Gombani uliopo mjini hapa. Hotuba yake inahitimisha sherehe za mapinduzi ambazo zilianza kuadhimishwa tangu Desemba 31 mwaka jana kwa shughuli za kufanya usafi katika Wilaya za Pemba na Unguja huku akipokea maandamano ya wananchi na paredi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Kwa mujibu wa Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed viongozi wa kitaifa na wawakilishi wa nchi mbalimbali wanahudhuria…
PAMOJA NA REKODI HIZI ZA KUTISHA SIMBA SC “YES WE CAN”
Wapinzani wa Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika kundi D, timu ya JS Saoura ya Algeria wanatarajiwa kutua nchini kesho Alhamis tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumamosi kwenye uwanja wa taifa Dar es salaam. Katika mchezo huo, Simba inatakiwa kuutumia vizuri ili kuweza kupata alama 3 muhimu ambazo si rahisi sana kuzipata kwenye mchezo wa marejeano huko mjini Méridja Algeria kutokana na rekodi nzuri ya JS Sauora kwenye uwanja wao wa nyumbani maarufu kama ‘August 20, 1955’. JS Saoura waliweka rekodi ya kucheza mechi 58 kwenye…
RAIS MAGUFULI AAGIZA NDEGE ZA RAIS ZIANZE KUBEBA ABIRIA
Rais Dkt. Magufuli ameagiza kwamba ndege 2 kati ya ndege 3 za Rais, zipakwe rangi ya Air Tanzania na zianze kutumika kusafirisha abiria.
Ametoa agizo hilo jana Ijumaa Januari 11, 2019 wakati wa mapokezi ya ndege ya pili aina ya Airbus A220-300 iliyowasili katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
“Kwa kuwa rais mwenyewe hasafiri hovyo sasa zinakaa kufanya nini na moja ina uwezo wa kubeba watu 50. Hii haitabeba abiria pale tu ambako itakuwa inatumika,” amesema Rais Magufuli.
Akijibu ombi la Askofu mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible fellowship (FGBF) Zachary Kakobe aliyemuomba kuwa na desturi ya kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kama ilivyo kwa viongozi wa dini, Magufuli amesema anaogopa kukutana na watu ambao wanatukana na kutishia kumkatakata.
“Huwezi kukutana na mtu anayekuambia akikushika atakukata halafu ukutane naye kumbe ndiyo siku yako ya kuchinjwa hivyo ni bora umuache akae mwenyewe huko,” amesema Rais Magufuli
Aidha Rais Magufuli ameshwashukuru wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa kuwezesha maendelo hayo kupitia kuunga kwao mkono bajeti inapopelekwa bungeni.
Airbus 220-300 imekuwa ni ndege ya 6 kuwasili nchini miongoni mwa 7 zilizonunuliwa na Serikali huku nyingine moja ikisubiriwa ambapo leo Rais amethibitisha kuwa ndege nyingine ya 8 inanunuliwa.
MAGUFULI : KUMBE MIMI NAFUU KULIKO DKT. BASHIRU,HOTUBA ZAKE ZINASHANGAZA
Rais John Magufuli ameweka wazi kuwa hotuba za Katibu mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally huwa zinamshangaza kwa namna ambavyo anazitoa bila uoga jambo ambalo humfanya yeye ajione ni mpole.Mwenyekiti huyo wa CCM alieleza hilo jana kwenye hotuba yake wakati wa mapokezi ya ndege ya pili aina ya Airbus A220-300 iliyowasili nchini jana mchana Januari 11, 2019 kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
''Dkt. Bashiru amekuwa muwazi, huwa namuangalia kwenye hotuba zake saa nyingine nasema kumbe mimi nafuu bwana kuliko huyu jamaa'', alisema.
Rais alieleza kuwa Katibu wake huyo amekuwa akikemea ufisadi ambao ulikuwa ukishamili siku hadi siku lakini sasa yeye anapingana nao hadharani bila kujali.
Magufuli amewataka viongozi wote wa chama na Serikali kuendelea kuwatumikia wananchi kwa moyo mmoja ili kusaidia maendeleo na siku moja Tanzania itakuwa kama Ulaya.
MAKOSA 12 WALIYOSOMEWA POLISI NA WATUHUMIWA WALIOKUWA WAKITOROSHA DHAHABU MWANZA
Askari polisi wanane wanaotuhumiwa kushiriki mpango wa kutorosha dhahabu kilo 319.59 zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 27 pamoja na wamiliki wa madini hayo, wamefikishwa mahakamani.Washtakiwa hao waliokamatwa Januari 4, mwaka huu, walifikishwa mahakamani kwa makosa 12 likiwemo la uhujumu uchumi.
Walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Gwae Sumaye, na mawakili wa serikali Castuse Ndamgoba, Robert Kidando na Jackline Nyantori.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Januari 4, watuhumiwa wanne ambao ni Sajid Abdallah, Kisabo Nkinda, Emmanuel Kija na Hassan Sadick walitenda kosa la kuwapatia rushwa ya Sh. milioni 700 watuhumiwa wanne ambao ni askari polisi ili kuwasaidia kutorosha madini hayo.
Askari ambao majina yao yalitajwa na mawakili wa serikali ni Koplo Dani Kasara, Koplo Matete Misana na makonstebo Japhet Kuliko, Maingu Sorry, Alex Mkali, Timoth Paul na David Ngelela na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Moris Okinda ambaye alikuwa kiongozi wa askari hao.
Miongoni mwa mashtaka 12 yanayowakabili askari hao ni pamoja na uhujumu uchumi, kuomba na kupokea rushwa ya Sh. milioni 700, kuisababishia hasara serikali na kutakatisha fedha kinyume cha sheria za nchi.
Hakimu Gwae alisema watuhumiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 28, mwaka huu, itakapotajwa.
Askari hao wanane, kabla ya kufikishwa mahakamani, Jeshi la Polisi Tanzania liliwasimamisha kazi Januari jana kutokana na tuhuma za kutenda kosa kinyume cha mwenendo mwema wa jeshi hilo.
ASKARI SABA WA " DHAHABU MWANZA" WASIMAMISHWA KAZI KWA KUOMBA RUSHWA

Jeshi la Polisi Tanzania tarehe 11/01/2019, limewasimamisha kazi askari saba (7) wa vyeo mbalimbali kwa kutenda kosa kinyume na mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi na tayari wamefikishwa mahakamani kusomewa mashitaka yanayo wakabili.
Hatua hii imechukuliwa, baada ya askari hao kuomba rushwa ya bilioni moja na baadae kupokea rushwa ya milioni mia saba toka kwa mfanyabiashara wa dhahabu aitwaye Sajid Abdalah Hassan ambaye walimkamata akiwa na dhahabu kiasi cha kilogramu 319.59, yenye thamani ya mabilioni ya shilingi za kitanzania.
Askari hao waliosimamishwa kazi ni;
- E.4948 CPL Dani Isack Kasala
- F.1331 CPL Matete Maiga Misana
- G.1876 PC Japhet Emmanuel Lukiko
- G.5080 PC Maingu Baithaman Sorrah
- G.6885 PC Alex Elias Nkali
- G.7244 PC Timoth Nzumbi Paul
- H.4060 PC David Kadama Ngelela.
Aidha, kuhusu Afisa SSP: Moris Okinda ambaye alikuwa kiongozi wa askari hao walioomba na kupokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha, mamlaka yake ya kinidhamu tayari imemsimamisha kazi na tayari amefikishwa mahakamani pamoja na askari hao.
Pamoja na askari hao, pia wamefikishwa mahakamani watuhumiwa wengine wa nne waliokamatwa huko Kigongo feri Wilayani Misungwi wakitorosha madini hayo ya dhahabu kutoka Tanzania kwenda Nchi jirani ya Rwanda.
Watuhumiwa waliokamatwa wakitorosha madini hayo ya dhahabu ni;
- Sajid Abadalah Hassan, miaka 28, mfanyabiashara wa dhahabu, mkazi wa Ilala Dar es Salaam na Mwanza mtaa wa pamba ‘A’.
- Kisabo Kija @ Mkinda , miaka 55, mfanyabiashara wa dhahabu, mkazi wa mwatulole –Geita
- Emmanuel Ntemi, miaka 63, dereva, mkazi wa kijiji cha mwatulole –Geita
- Hassan Sadiq Hassan, miaka 28, Mhindi, Raia wa Pakistani, mkazi wa Mwanza mtaa wa Pamba ‘A’, Mfanyakazi wa duka la kuuza vito.
Kufuatia sakata hili, Jeshi la Polisi Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tunaendelea na uchunguzi wa kina ili tuweze kuwakamata watuhumiwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine katika sakata hili.
Imetolewa na;
CP: Robert Boaz
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Tanzania
11 January, 2019.
HABARI KUBWA KWENYE VICHWA VYA MAGAZETI YA TANZANIA JANUARI 12,2019.
Fahamu yote yaliyojiri katika Magazeti ya Tanzania leo Januari 12, 2019. Hapa unapata habari zote zilizopewa uzito katika kurasa za mbele na kurasa za nyuma za habari za michezo na burudani.
Friday, 11 January 2019
UWEKEZAJI BILA SIASA UNAWEZEKANA :ISSA SAMMA
Na Mwandishi wetu -NGARA KAGERA Msemaji wa wawekezaji kutoka Korea Kusini katika wilaya ya Ngara mkoani Kagera Issa Samma amesema wakazi wa wilaya hiyo na viongozi wao wanaweza kukubali au kukataa uwekezaji bila kulumbana kwa kutanguliza siasa, ukanda na ukabila. Samma ametoa kauli hiyo siku chache baada ya mbunge wa jimbo la Ngara Alex Gashaza kunusurika kupigwa na wananchi wa kijiji cha Kazingati akipinga utaratibu uliotumika wa kuwagawia ardhi wawekezaji wa Korea Kusini wilayani Ngara. Amesema wawekezaji walijitokeza kutaka ardhi ya kilimo na kujenga viwanda Kuanza katika kijiji cha Kazingati…
DAKIKA 90 SIMBA, MALINDI HAKUNA MBABE...SIMBA WATOBOA KWA PENATI 3-1

Baada ya timu zote kutunishiana misuli,wameenda kwenye penati ambapo Simba wamepata mabao 3 huku Malindi wakipata bao 1.
Simba SC wametinga Fainali wakicheza na Azam Fc
Simba SC wametinga Fainali wakicheza na Azam Fc
WAFANYABIASHARA WANAOKWEPA KODI WAPEWA SOMO KAGERA
Na Allawi Kaboyo-Bukoba Kagera. Mkuu wa mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewataka wafanyabiashara mkoani humo kuacha tabia ya kufunga maduka yao palea wanapowaona maafisa wa TRA wakija katika maduka yao na kumuagiza meneja TRA wa mkoa huo kujenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara pamoja na kutoa elimu ya kutosha ya umuhimu wa kulipa kodi. Mkuu wa mkoa ametoa agizo hilo katika kikao chake na wadau wa kodi,maafisa wa TRA pamoja na wafanyabiashara kilichofanyika january 11 mwaka huu kwenye ukumbi wa manispaa ya Bukoba kikiwa na lengo la kujua hali ya…



