
Na Bora Mustafa, Arusha
Mradi wa Nile Blues Project umeendelea kuwafikia wanafunzi wa shule mbalimbali jijini Arusha kupitia warsha za muziki, sanaa, ubunifu na utamaduni, ukiwa na lengo la kuwajengea vijana ujuzi na kuwapa nafasi ya kugundua na kukuza vipaji vyao.
Mradi huo ambao unalenga kufikia jumla ya shule 10 jijini Arusha, umeendelea na mafunzo yake katika Sekei Secondary School, ambapo wanafunzi wamepata nafasi ya kujifunza kwa vitendo pamoja na kushiriki katika shughuli za ubunifu.
Akizungumza Leo Agosti 26,2026 wakati wa programu hiyo, Lwanda Magere,Meneja wa Mradi wa Nile Blues Project, amesema mafunzo hayo yamekuwa na matokeo mazuri kutokana na mwitikio wa wanafunzi ambao wameweza kutumia maarifa waliyopata kutengeneza na kuonesha ubunifu wao wenyewe.
Pia amesema furaha kubwa kwa timu ya mradi huo ni kuona wanafunzi wakipata ujuzi ambao unaweza kuwasaidia kutambua uwezo wao na kuutumia katika maisha ya sasa na baadaye.
Kwa upande wake, Renalda Masawe, Mratibu wa Programu, amesema Sekei Secondary ni miongoni mwa shule ambazo mradi umefikia katika utekelezaji wa programu hiyo, baada ya awali kutembelea St. Patrick School.
Amesema baada ya Sekei, mpango huo utaendelea katika Kaloleni Primary School na baadaye Arusha Meru, huku lengo likiwa ni kufikisha mafunzo hayo katika shule 10 za Arusha.
Masawe amesema mpango huo utaendelea pia wiki ijayo katika shule nyingine, huku akieleza kuwa baadhi ya shule zimeonesha nia ya kushiriki katika programu hiyo kutokana na umuhimu wake kwa wanafunzi.
Amesema timu ya mradi iko tayari kushirikiana na shule zitakazohitaji programu hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanapata fursa ya kujifunza na kukuza vipaji vyao.
Aidha, amesema lengo si kuwafundisha wanafunzi maarifa ya darasani pekee, bali pia kuwawezesha kutumia ubunifu, sanaa na utamaduni kama sehemu ya kujenga uwezo wao.
Kwa upande wake, Sir Patrick, Mwalimu wa Michezo wa Sekei Secondary School, amesema programu kama hiyo ina umuhimu mkubwa katika kuboresha elimu kwa wanafunzi kwa kuwa inawapa nafasi ya kujifunza kupitia michezo, sanaa na utamaduni.
Amesema ni muhimu shule kuendelea kutoa nafasi kwa shughuli za nje ya darasa ambazo zinaweza kuwasaidia wanafunzi kugundua vipaji na uwezo wao katika maeneo mbalimbali.
Amesema ushirikiano kati ya shule na programu zinazolenga kukuza vipaji unaweza kuwa chachu ya kuwajenga wanafunzi wenye uwezo mpana zaidi, sambamba na masomo yao ya kawaida.
Naye Rose Frank, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Sekei Secondary School, amesema mafunzo hayo yamewapa wanafunzi fursa ya kujifunza mambo mapya ambayo awali hawakuwa na uelewa nayo.
Pia amesema kupitia mafunzo hayo wanafunzi wameweza kupata maarifa mapya na kujifunza kwa vitendo, jambo ambalo limewapa hamasa ya kuendelea kutumia vipaji na ubunifu wao.
Nile Blues Project inaendelea na mpango huo katika shule mbalimbali za Arusha, huku ikilenga kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na kuwapa ujuzi unaohusisha muziki, sanaa, ubunifu na utamaduni.
Programu hiyo pia inaendana na umuhimu wa kuwapa vijana nafasi ya kujifunza kuhusu sanaa na utamaduni wao, huku shughuli za vitendo zikiwasaidia kugeuza maarifa wanayopata kuwa ujuzi unaoweza kutumika katika maisha yao.




0 comments:
Post a Comment