
Meneja Msaidizi Huduma kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Shinyanga Ramadhan Sengo


Na Stella Herman,Shinyanga
Wafanyabiashara Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kuongeza uelewa kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi ili waweze kutekeleza ipasavyo wajibu wao wa kikodi na kuepuka makosa yanayoweza kusababisha migogoro au adhabu.
Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga kwa wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa marekebisho ya sheria za kodi yaliyoanza kutumika Juni 30, 2026.
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wafanyabiashara kufahamu mabadiliko yaliyofanyika, kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa kodi pamoja na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa walipa kodi na namna ya kushirikiana na TRA katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika leo Agost 19, 2026, Meneja Msaidizi Huduma kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Shinyanga Ramadhan Sengo, amesema TRA imeamua kuwashirikisha wafanyabiashara moja kwa moja ili kuwapa nafasi ya kuelewa mabadiliko hayo na kupata majibu ya maswali yanayohusu shughuli zao.
Sengo amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha mfumo wa ulipaji na ukusanyaji wa kodi unakuwa na ufanisi.
“Kwa pamoja, mafunzo haya ni muhimu katika kuongeza jitihada za wafanyabiashara na taasisi kwa pamoja ili kusaidia Taifa letu kuwa na uwezo wa kukusanya kodi kwa ajili ya maendeleo. Tumieni fursa hii kuuliza maswali yatakayotupa uelewa na kutusaidia kujua mambo mbalimbali kupitia wataalamu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania,” amesema Sengo.

Katika mafunzo hayo, Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi kutoka TRA Mkoa wa Dar es Salaam, Abdalah Seif, alitoa ufafanuzi kuhusu maeneo mbalimbali yaliyofanyiwa marekebisho katika sheria za kodi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) Mkoa wa Shinyanga, Hatibu Mgeja, amesema sekta binafsi ni sehemu muhimu katika kukuza uchumi na hivyo Serikali na wafanyabiashara wanapaswa kuendelea kushirikiana.
Mgeja alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutoa elimu kuhusu mabadiliko ya mfumo wa kodi, hatua ambayo amesema itasaidia wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao kwa uelewa zaidi.
“Tunashukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika mfumo wa kodi kwa wafanyabiashara, hatua ambayo inalenga kusaidia ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya maendeleo ya Taifa,” amesema Mgeja.
Wafanyabiashara walitumia pia fursa hiyo kuiomba TRA kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusiana na shughuli zao, ikiwemo TANROADS, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), TARURA na Halmashauri, katika kutoa elimu ya pamoja kuhusu kodi na majukumu mbalimbali yanayowahusu.
Wamesema ushirikishwaji wa taasisi hizo utasaidia kupunguza mkanganyiko unaoweza kujitokeza wakati wafanyabiashara wanapotekeleza majukumu yao ya kikodi na majukumu mengine yanayohusiana na uendeshaji wa biashara.
Mkurugenzi wa Lyakale Civil Engineering, Christopher Ringo, ameomba TRA Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa watumishi wa TANROADS na TARURA, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya kikodi kwa wakandarasi, hususan kutokana na kuchelewa kwa malipo.
Mabadiliko ya sheria za kodi yaliyofafanuliwa katika mafunzo hayo yanahusu maeneo mbalimbali, yakiwemo uuzaji wa mali, mazao ya misitu, ushuru wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, uendeshaji wa kampuni za madini, viwango vya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), wajibu wa waajiri kuzingatia Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), mirahaba ya malipo kwa timu za mpira wa miguu, biashara zinazofanyika kupitia mitandao, kodi kwa vyombo vya usafiri wa abiria, wajibu wa kulipa kodi pamoja na kodi zinazohusiana na michezo ya bahati nasibu.


Meneja Msaidizi Huduma kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Shinyanga Ramadhan Sengo












0 comments:
Post a Comment