Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib, amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuonesha dhamira ya dhati katika mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya kupitia maridhiano, mazungumzo, na ushirikishwaji mpana wa wadau mbalimbali wa kitaifa.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia mkutano uliozikutanisha jumla ya vyama vya siasa 19 vilivyohudhuria Ikulu jijini Dar es Salaam, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikikosekana baada ya kususia mazungumzo hayo.
Khatib amesisitiza kuwa mchakato wa kupata katiba mpya hauwezi kufikiwa kwa misimamo mikali au kugomea mikutano ya mashauriano, bali unahitaji nia njema na utayari wa kusikiliza mawazo ya wengine kupitia utekelezaji wa falsafa ya 4R inayosisitiza umoja, mshikamano, na ustahimilivu.
Amemuunga mkono Rais Samia kufuatia mipango ya kuunda tume maalumu ya kuchunguza na kutatua masuala ya vurugu za kisiasa zilizopita kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande, sambamba na kuimarisha misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kupitia makubaliano ya hivi karibuni kati ya CCM na ACT Wazalendo huko Zanzibar. Vilevile, serikali imeweka mikakati thabiti kupitia sera za ajira, ujasiriamali, na sekta ya kilimo ili kuwaondoa vijana katika hatari ya kutumiwa kwenye migogoro ya kisiasa na kuwashirikisha kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
Viongozi wengine mbalimbali wakiwemo Katibu wa Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir, mgombea wa zamani wa urais wa Zanzibar kupitia NCCR-Mageuzi, Lela Rajab Khamis, na Makamu Mwenyekiti wa UWT, Zainab Shomari, wamempongeza Rais Samia kwa uongozi wake unaojumuisha makundi yote katika ujenzi wa taifa na kuimarisha misingi ya demokrasia na maridhiano nchini

0 comments:
Post a Comment