Tuesday, 25 August 2026

PROF SHEMDOE, WANANCHI WARIDHISHWA NA UJENZI WA BARABARA ZA AFCON 2027 DAR ES SALAAM

...

Na OWM – TAMISEMI, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara zinazoingia kwenye viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michezo na mazoezi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) jijini Dar es Salaam, huku wananchi wakifurahia hatua hiyo na kuipongeza Serikali kwa ujenzi wa miundombinu  itakayosaidia kutatua changamoto ya usafiri katika maeneo hayo.

Prof. Shemdoe amesema hayo Agosti 24, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, ikiwemo Kigamboni, Uwanja wa Taifa (Benjamin Mkapa), Leaders Club pamoja na eneo la Mbweni kuelekea Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo.

Amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, akieleza kuwa ujenzi wa barabara za Kigamboni umefikia asilimia 75, barabara za Uwanja wa Taifa asilimia 20, Leaders Club asilimia 70, huku barabara za Mbweni kuelekea Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo zikifikia asilimia 20. Kwa ujumla, Prof. Shemdoe amesema utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo umefikia wastani wa asilimia 50.

Prof. Shemdoe amesema ametoa maelekezo kwa wakandarasi katika maeneo yote yanayotekeleza miradi hiyo kuhakikisha wanaongeza kasi ya ujenzi na kufanya kazi kwa saa 24, ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha ifikapo Agosti 30, 2026, utekelezaji unafikia wastani wa zaidi ya asilimia 60. 

Kwa upande wake, Mkazi wa Mbweni jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Malindi Estate, Bi. Maria Bilia, amesema wananchi wa Mbweni wamefarijika kuona ujenzi wa barabara hizo ukiendelea, kwa kuwa utasaidia kupunguza changamoto ya usafiri katika eneo hilo.

Bi. Bilia amemuomba Prof. Shemdoe kufikisha salamu za pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara kuelekea AFCON 2027.

Ameongeza kuwa ameshuhudia wakandarasi wakifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, hatua ambayo amesema inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Malindi Estate, Kata ya Mbweni, Manispaa ya Kinondoni, Bi. Selina Mkonye, amesema wananchi wa eneo hilo wanaunga mkono jitihada za Serikali kwa vitendo, ikiwemo kuwa na mpango mkakati wa miaka mitano wa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 30 kwa kiwango cha lami na kilomita 60 kwa kiwango cha changarawe.

Bi. Mkonye amesema ujenzi wa barabara zinazotekelezwa kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027 umekuja kuchagiza na kuimarisha mpango mkakati huo wa wananchi wa kuboresha miundombinu katika eneo lao.

Ujenzi wa barabara hizo unalenga kuboresha upatikanaji na mtiririko wa usafiri kuelekea viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michezo na mazoezi ya Fainali za AFCON 2027 jijini Dar es Salaam, sambamba na kuboresha miundombinu kwa manufaa ya wananchi.

Kwa sasa, miradi minne (4) inatekelezwa, ambayo ni ujenzi kwa kiwango cha zege wa Barabara ya Taifa yenye urefu wa kilomita 1.3, Litapwasi kilomita 0.43 na Sotele kilomita 0.2; ujenzi kwa kiwango cha zege wa Barabara ya Yanga yenye urefu wa kilomita 0.7; ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Dahomey yenye urefu wa kilomita 0.5; ujenzi wa Barabara ya Mbalizi yenye urefu wa kilomita 0.8, pamoja na uboreshaji wa maegesho ya VVIP katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger