Rais Mstaafu wa Msumbiji Mhe. Joaqium Alberto Chissano amewasili nchini kushiriki hafla ya utoaji tuzo ya Kitaifa ya Mwl. Nyerere ya Uandishi Bunifu inayotarajiwa kufanyika Aprili 13, 2023 jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia ujio wa Kiongozi huyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Adolf Mkenda amesema Rais Mstaafu Chissano anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika utoaji wa Tuzo hizo ambazo zinatolewa kwa mara ya kwanza nchini.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa Kamati maalum ya Tuzo ilimpendekeza Rais Chissano kuwa mgeni rasmi kutokana na ukweli kwamba ni Rais wa kwanza kuhutubia kutumia lugha ya kiswahili katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika.
"Tunayo furaha kuwa na Mgeni Rasmi Rais Mstaafu wa Msumbiji Mhe. Joaquim Alberto Chissano ambaye mbali na kuongea lugha ya kiswahili vizuri lakini pia ni Mkuu wa nchi wa kwanza kutumia lugha ya kiswahili katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika," amesema Prof. Mkenda
Ameongeza kuwa mshindi wa Tuzo hiyo mbali ya kupata zawadi ya fedha taslimu, vitabu vyake vitachapishwa na kusambazwa katika shule pamoja na maktaba kwa gharama za Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Kitaifa ya Mwl. Nyerere Prof. Penina Mlama amesema Kamati ilipokea miswada 283 ya riwaya na mashairi tuzo ambayo ilishindanishwa na kupata washindi watakaotangazwa Aprili 13, 2023.
Prof. Mlama ameongeza kuwa katika hafla hiyo waandishi nguli na maarufu watashiriki akiwemo Prof. Abdallatif Abdalla, Prof. Farouk Taban, Ida Hadjivayanis na Moyez Vassanji.
Aidha Mwenyekiti huyo amesema kumalizika kwa hafla ya utoaji tuzo za Mwaka 2023 ndio kuanza kwa maandalizi ya tuzo za Mwaka 2024 ambapo Miswada itaanza kupokelewa kuanzia Juni 1, 2023
Tuzo ya Taifa ya Mwl. Nyerere ya Uandishi Bunifu inatolewa kwa lengo la kuhamasisha uandishi Bunifu, usomaji vitabu, kutunza utamaduni ,kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili na kuimarisha Uchapishaji.
0 comments:
Post a Comment