Sunday, 9 April 2023

CAG AFICHUA SERIKALI YA MAGUFULI ILIVYOLISABABISHIA TAIFA HASARA YA SH 1.7 TRILIONI MRADI WA SGR

...

👉Ripoti mpya ya CAG iliyotolewa Aprili 6, 2023, yasema Serikali ya Awamu ya 5 ilivunja sheria ya nchi kwenye utoaji wa kandarasi ya reli

 ðŸ‘‰Ilikubali masharti mabovu ya Benki ya StanChart kuwapa kandarasi Waturuki kwa gharama ya juu bila tenda ya wazi ya ushindani

Na Waandishi Wetu

SERIKALI ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli iliingizia taifa hasara ya Dola za Marekani milioni 742.4 (zaidi ya Shilingi trilioni 1.7) kwenye ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR baada ya kukubali masharti mabovu ya mkopo wa benki ya Standard Chartered.

Ripoti Kuu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo 2021/22 iliyotolewa juzi na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilisema kuwa hasara hiyo kwa taifa ilitokana na Serikali ya Magufuli kukubali masharti ya ajabu ya mkopo wa kibiashara wa Dola za Marekani Bilioni 1.46 kutoka kwa Benki ya Standard Chartered Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa SGR uliotolewa mwaka 2020.

Moja ya masharti ya mkopo huo ni kuwa Serikali ivunje Sheria ya Manunuzi ya Umma kwa kutoa kandarasi mbili za ujenzi wa reli ya SGR kwa kampuni ya Kituruki ya Yapi Merkezi Insaat VE Sanayi As bila zabuni ya wazi ya kushindanisha kampuni nyingine.

Serikali ya Magufuli ilikubali masharti hayo ya ajabu kwa kutoa kandarasi kwa Waturuki kinyume na sheria za nchi.

CAG alibaini kuwa gharama za ujenzi wa kipande cha reli ya Makutupora-Tabora (Lot 3) iliongezeka kwa Dola za Marekani milioni 1.3 (zaidi ya Shilingi Bilioni 3) kwa kila kilomita wakati gharama ya ujenzi wa kipande cha reli ya Tabora-Isaka (Lot 4) iliongezeka kwa Dola milioni 1.6 (Shilingi Bilioni 3.74) kwa kila kilomita.

"Shirika la Reli Tanzania (TRC) halikutumia njia ya ununuzi ya ushindani katika ujenzi wa reli ya kisasa kwa kipande cha tatu na cha nne na kusababisha kuongezeka kwa Dola za Kimarekani milioni 1.3 na milioni 1.6 kwa kilomita mtawalia ikilinganishwa na mikataba ya awali,," alisema CAG.

Reli ya Makutupora-Tabora yenye urefu wa kilomita 368 inajengwa kwa gharama ya Dola za Marekani Bilioni 1.9, wakati kipande cha Tabora-Isaka chenye urefu wa kilomita 165, kinajengwa kwa gharama za Dola za Marekani milioni 900.

Maana yake ni kuwa taifa limeingia jumla ya hasara ya Dola za Marekani 742.4 (zaidi ya Shilingi trilioni 1.7) kwenye vipande hivyo viwili vya reli.

"Mapitio yangu ya njia za ununuzi zilizotumika katika ununuzi wa mkandarasi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha 3 na 4 yalibainisha kuwa Benki ya Standard Chartered ambako Serikali ilipata mkopo iliweka masharti kwamba ingekubali jukumu la kuwa Mratibu wa 
Kimataifa, na Wakala Kiongozi Aliye na Mamlaka kupanga ufadhili na mkopo kwa Wizara ya Fedha na Mipango (MoFP) tu kwa masharti kwamba kampuni ya Yapi Markezi iteuliwe kama Mkandarasi," alisema CAG kwenye ripoti hiyo.

"Wizara 
ya Fedha na Mipango (MOFP) ilikubali mkopo huo kwa masharti yasiyofaa kutoka Benki ya Standard Chartered kupitia barua yenye kumbukumbu namba PST/GEN/2021/01/55."

Wakati barua hiyo inaandikwa, Doto James ndiye aliyekua Katibu Mkuu wa Hazina (PST) kwenye Wizara ya Fedha na Mipango.

CAG amebaini zaidi kuwa TRC iliamua kuchagua njia ya kutoa zabuni kwa njia 
mzabuni mmoja licha ya ushauri uliotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Bodi ya Zabuni, ambayo iliishia kuigharimu serikali fedha zaidi, ambayo ingeweza kuepukwa.

"Ni maoni yangu kwamba, hakuna mfadhili anayeweza kuitaka Serikali ya Tanzania kumpa mkataba mkandarasi pasipo kuwa na uwazi, ushindani, usawa na haki kwa wakandarasi wote wenye sifa na wanaostahili katika mchakato wa ununuzi," alisema CAG.

Ripoti ya CAG ilibaini kuwa baada ya Serikali ya Magufuli kukubali masharti yasiyofaa ya kuwapa kandarasi ya Lot 3 na Lot 4 kwa Yapi Merkezi bila tenda ya wazi ya ushindani, Waturuki hao wakaongeza gharama ya ujenzi kuliko kawaida na kuliingizia taifa hasara kubwa.

Wakati vipande vingine vya reli ya SGR ya Tanzania vinajengwa kwa gharama ya kati ya Dola za Marekani milioni 3.9 na Dola la Marekani milioni 4.6 kwa kila kilomita, kipande cha Lot 3 walichopewa Waturuki bila ya tenda ya wazi wanakijenga kwa gharama ya juu ya Dola milioni 5.2 kwa kila kilomita.

Vile vile, kipande cha Lot 4 walichopewa Waturuki hao hao bila ya tenda ya wazi (single source) wanakijenga kwa gharama kubwa mno ya Dola Marekani milioni 5.5 kwa kila kilomita.

"Kulingana na tofauti hiyo, hapakuwa na faida ya kiuchumi kwa TRC kwa kutoa kandarasi kupitia njia ya chanzo kimoja kwa M/S Yapi Merkezi. Hii ni kwa sababu gharama awali za miradi mingine zilikuwa chini ikilinganishwa na mkataba aliopewa mkandarasi wa kipande cha 3 na 4," alisema CAG.

"Zaidi ya hayo, niligundua kuwa mawanda ya kazi kwa kipande cha 3 na 4 ya mradi ulikuwa mdogo na ulikuwa na miundombinu michache kuliko ile ya kipande cha 1, 2, na 5, na miundo mikuu zaidi."

CAG amependekeza kuwa menejimenti ya TRC iweke kipaumbele katika matumizi ya mbinu shindani ya ununuzi katika shughuli za manunuzi za siku zijazo ili kuepuka upotevu wa fedha za walipa 
kodi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger