Mfano wa mchele
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Jofrey Justine (45) anadaiwa kuuawa kwa kunyongwa na watu wasiojulikana wakati akiendelea na kazi ya ulinzi katika mashine ya kusaga na kukoboa nafaka katika kitongoji cha Majengo kijiji cha Didia kata ya Didia wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na Malunde 1 blog, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Jumamosi Septemba 24,2022 ambapo pamoja na kufanya mauaji hayo watu hao wasiojulikana waliondoka na kilo 500 za mchele na kutokomea kusikojulikana.
Akielezea kuhusu tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Didia Mrisho Hamad amesema mlinzi huyo ambaye ni mwenyeji wa Karagwe mkoani Kagera alikutwa ameuawa siku ya Jumamosi asubuhi.
“Nilipigiwa simu majira ya saa 2 asubuhi nikaambiwa kuna mtu amefariki dunia kwenye Mashine ya mzee Richard. Nilifika eneo la tukio tukakuta mwili wa marehemu umelazwa nyuma ya mashine. Hatukuona majeraha ila tuliona tu damu kidogo mdomoni”,ameeleza Mwenyekiti huyo wa kijiji akizungumza na Malunde 1 blog
“Kwenye hiyo mashine tukaona kuna sehemu ilikuwa imetobolewa na kubaini kuwa kuna upotefu wa magunia matano ya mchele yenye kilo 100. Nikawapigia simu polisi wakaja, wakauchukua mwili wa marehemu”,ameongeza Hamad.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanaendelea kufanya upelelezi ili kuwabaini watu waliohusika kwenye tukio hilo la mauaji na wizi wa mchele kilo 500.
0 comments:
Post a Comment