Thursday, 18 February 2021

SHIRECU YAKAMATA SHEHENA YA CHOROKO MJINI SHINYANGA

...

Shehena ya choroko

Na Suzy Luhende   - Shinyanga

Chama cha Ushirika mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) kimekamata shehena ya choroko zaidi ya tani 200 katika mtaa wa Viwandani Mjini Shinyanga ambazo ambazo zilinunuliwa kwa wakulima kwa bei ndogo isiyoeleweka na kampuni ya Impex mjini Shinyanga.

Shehena hizo zimekamatwa juzi baada ya baadhi ya wakulima kutoa taarifa kwa viongozi wa Chama cha Ushirika kuwa kuna wafanyabiashara  wananunua choroko kinyume na utaratibu uliokubaliwa wa kuuza kwa kupitia stakabadhi gharani ambapo wananunua kwa bei ndogo isiyoeleweka.

Akizungumza na waandishi wa habari  Kaimu Meneja wa Chama cha Ushirika mkoa wa Shinyanga (Shirecu) Hansi Msuya amesema walipata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kuna magari yanasomba choroko yanapeleka maeneo ya viwandani, ndipo walianza ziara ya kushitukiza katika maeneo ya viwandani na kufanikiwa kukamata Shehena hizo.

"Katika ziara zetu za kufanya upekuzi katika maeneo ya viwanda tulifanikiwa kukamata mzigo wa choroko zaidi ya tani 200 kwa Wakala wa Impex Company ambaye ni mnunuzi wa zao la choroko hata hivyo tumekubaliana na mnunuzi choroko hizi zitaingizwa kwenye mfumo wa kuuzwa katika zitakabadhi gharani hapa hapa zilipo", alisema Msuya.

Kwa upande wake Mrajisi Msaidizi mkoa wa Shinyanga Hilda  Boniface , amesema mfanyabiashara huyo hakufuata makubaliano yaliyowekwa na mkuu wa mkoa Zainab Telack wa kununua kwa kutumia stakabadhi gharani hivyo shehena hizo zitauzwa upya ndani ya ghara hili kwa mfumo wa stakabadhi gharani.

"Zinapouzwa kinyemela hivi mkulima anapunjwa lakini zikiuzwa kwa stakabadhi gharani mkulima ana haki ya kukataa kuwa mnada uahirishwe bei iko chini na inawezekana, sisi tutasimamia haki ya mkulima apate haki yake, na walitupigia wakulima wao wenyewe, mfumo huu ulipitishwa na mkoa hivyo haitakiwi kuupuuza nami ndiye msimamizi wa huu mfumo",alisema Hilda.

Baadhi ya wakulima James Mussa na Wande wakazi wa kijiji cha Pandagichiza wilaya ya Shinyanga wamesema wameshangaa kuona magari yanabeba choroko walijua labda zinaenda kuuzwa kwenye mfumo wa stakabadhi gharani kumbe tayari zimeshanunuliwa kwa bei ya ndogo ya kunyongwa.

Kaimu Meneja wa Chama cha Ushirika mkoa wa Shinyanga (Shirecu) Hansi Msuya akizungumza
Hilda Boniface mrajisi msaidizi mkoa wa Shinyanga
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger