Monday 23 November 2020

SERIKALI YA TANZANIA YASEMA IMEONGEZA UWEZO WA KUGUNDUA WAGONJWA WAPYA WA KIFUA KIKUU

...

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akigawa cheti cha pongezi kwa Uongozi wa Afya wa Mkoa wa Manyara kupitia Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Damas Kayera mara baada ya kushika nafasi ya kwanza ngazi ya mikoa kwa kufanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa afua za kupambana na kifua kikuu na ukoma.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akisema jambo kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi akisema jambo kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe akisema jambo kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Jijini Dodoma.
Wajumbe wa Mkutano wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma wakisikiliza mada zinazotolewa kwenye mkutano.
Wajumbe wa Mkutano wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma wakiwa katika picha ya pamoja.
***


Na Englibert Kayombo WAMJW - Dodoma
Serikali ya Tanzania imeazimia kutokomeza kabisa ugonjwa wa kifua kikuu kwa kuongeza uwezo wa ugunduzi wa wagonjwa wapya wa kifua kikuu na kuwaweka kwenye matibabu.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu an Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.

“Uwezo wa nchi kugundua wagonjwa wapya na kuwaweka kwenye matibabu umeongezeka kutoka wagonjwa 62,908 (33%) mwaka 2015 na kwa sasa kufikia wagonjwa 82,166 (59%)” amesema Prof. Makubi

Kufuatia hatua hiyo Prof. Makubi amesema kuwa maisha ya wananchi takribani 300,000 ikiwemo ya watoto 45,000 yameponywa kwa kupatiwa dawa kwa wakati na kufuatiliwa kwa usahihi kuanzia mwaka 2015 hadi sasa.

Juhudi hizo pia zimeweka kupunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na kifua kikuu kwa 33%. “Mwaka 2015 kulikuwa na vifo 30,000 hivi sasa vimepungua hadi kufikia vifo 20,000” amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi amesema kuwa mafanikio hayo ya ongezeko la kasi ya ugunduzi wa wagonjwa wapya yametokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma ikiwemo kuboresha huduma za ugunduzi wa TB na kutoa kipaumbele kwa makundi yaliyoathirika zaidi kama vile kaya zenye wagonjwa, wanaoishi kwenye kaya duni, gerezani, wachimbaji wadogo wadogo na kwa waathirika wa madawa ya kulevya.

“Aidha tumewekeza katika afua bunifu mbalimbali za matumizi ya teknolojia mpya za molekyula za kubaini TB kwa usahihi na kwa haraka” amesisitiza Prof. Makubi.

Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi amesema Wizara imefanya vizuri kwenye kwa kufikia malengo waliyoyaweka kwenye Mpango mkakati ambao unamalizika mwaka huu 2020.

“Malengo ambayo tulijiwekea ya kupunguza vifo vitokanavyo na kifua kikuu tumeweza kuyafikia pamoja na kupunguza madhaa yanayotokana na ugonjwa huo” amesema Dkt. Subi

Amesema kuwa Serikali imefanikiwa kuongeza vituo vya upimaji wa kifua kikuu sugu kutoka kituo 1 mwaka 2015 hadi kufika vituo 145 hivyo kuongeza wigo wa huduma za matibabu ya ugonjwa huo

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa ofisi yake kwa kushirikiana Wizara ya Afya katika kipindi cha miaka 5 ijayo imejiwekea mikakati ya kuwawezesha watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya ili wawe na ujuzi na uwezo wa kutambua na kutoa huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger