Thursday, 3 September 2020

Takukuru yarejesha fedha za wakulima wa zao la pamba.

...
Samirah Yusuph
Maswa. WAKULIMA wa zao la pamba katika kijiji cha Gula wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru)kwa kuweza kuokoa kiasi cha fedha sh Milioni 6.2 walizouza zao hilo kwa musimu huu wa kilimo 2019/2020

Wakulima hao ambao ni wanachama wa Kilimo hai cha pamba katika kijiji hicho chini ya Kampuni ya ununuzi wa zao hilo ya S.M Holiding ya Jijini Mwanza fedha zao hizo zilikuwa zimepotezwa na Mhasibu wa kampuni hiyo,Paul Simba baada ya kufanya udanganyifu.

Wametoa pongezi hizo wakati wakikabidhiwa pesa hizo na Mwenyekiti wa Kilimo Hai Maswa,Laurence Chonjo chini ya usimamizi wa  Afisa wa Takukuru wilaya ya Maswa,Greyson Chogo katika ghala la kuuzia zao hilo lililoko maeneo ya misheni katika kijiji hicho.

Walisema kuwa wao wanalima kilimo hai cha zao hilo chini ya kampuni hiyo ambayo imekuwa ikiwawezesha pembejeo kwa masharti ya kuwauzia pamba lakini walifanyiwa vitendo vya hujuma na kudhulumiwa pesa zao.

Walisema kuwa licha ya kufuata maelekezo ya serikali kuwa fedha zao watalipwa kupitia akaunti zao za benki au simu lakini walichobaini namba za simu zilizoandikwa hazikuwa zao bali ni za mhasibu huyo aliyekuwa akinunua pamba katika kituo hicho.

"Tulielezwa kwa musimu huu hakuna mkulima atakayelipwa pesa taslimu atakapouza pamba yake hivyo tulio wengi tuliandika namba za simu ili pesa iingie huko lakini cha kushangaza tulipoona muda mrefu umepita tuliona tufuatilie tuone malipo yetu yameishia wapi tukagundua mhasibu aliweka namba zake za simu na pesa zetu zikaingia kwake,"alisema Njile Waziri.

Waliendelea kueleza kuwa baada ya kubaini hali hiyo walitoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya kijiji na baadaye walikwenda kutoa taarifa kwa taasisi hiyo na ndipo walipolifanyia kazi na hatimaye wameweza kupata fedha zao kwani awali walikuwa wamekata tamaa kuziipata.

“Niipongeze Takukuru katika wilaya yetu ya Maswa kwa kufanikisha kuipata fedha yetu ambayo tulifanyiwa mchezo mchafu na huyu mhasibu kwa kufanikisha  kuokoa pesa zetu ambazo tulishakata tamaa kuzipata lakini wamepambana hadi leo hii tumekabidhiwa,” alisema Peter Jinasa.

Naye Afisa wa Takukuru,Greyson aliyeshuhudia wakulima hao wakipokea fedha hizo alisema kuwa ni vizuri makampuni hayo ya ununuzi wa mazao ya wakulima wakaajili wafanyakazi ambao ni waaminifu sambamba na kuwafanyia ukaguzi wa mara kwa mara ili kuepusha wakulima kupoteza haki zao baada ya kuuza mazao yao.

"Takukuru tulipopata malalamiko haya ya wakulima wapatao 10 na tuliamua kuyafanyia kazi haraka ili kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao hivyo ni vizuri haya makampuni yakatoa ajira kwa wafanyakazi waaminifu na wafanyiwe ukaguzi wa mara kwa mara ili kuondoa matatizo kama haya,"alisema.

MWISHO.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger