Tuesday 29 September 2020

Watumishi Wizara Ya Kilimo Wapatiwa Mafunzo Ya Uadilifu

...


Watumishi wa Wizara ya Kilimo wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi.


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ametoa wito huo leo (29.09.2020) mjini Morogoro wakati alipofungua mafunzo ya siku nne kwa wakuu wa taasisi, bodi na wakala chini ya wizara kuhusu kamati za kudhibiti uadilifu.


Kusaya amewataka watumishi wote kuwa waadilifu ndani ya mioyo yao ili watende kazi walizokabidhiwa kama dhamana ya kuhudumia umma bila upendeleo na kujiepusha na vitendo vya rushwa.


“Lengo la wizara ya kilimo ni kuwa na watumishi wenye udilifu na maadili mema ndio maana nimetoa kibali mafunzo haya yafanyike na kuwezesha kutimiza malengo ya kazi .Mtumishi mwadilifu atatumikia watanzania muda wote “alisema Kusaya


Mafunzo haya yanawakutanisha wakuu wa taasisi, bodi za mazao na wakala pamoja na kamati za uadilifu toka taasisi zote 23 chini ya wizara ya kilimo ambapo lengo  ni kujifunza namna ya kuishi uadilifu katika kuhakikisha shughuli za serikali zinafikia malengo yaliyowekwa huku watumishi wakizingatia misingi ya uadilifu na maadili .

Katibu Mkuu huyo wa wizara ya kilimo amewaambia watumishi hao kuwa katika utendaji kazi wao wanapimwa kwa matokeo hivyo wajibidiishe kutenda haki kwa wananchi pindi wawapo sehemu za kazi kwa kuepuka vitendo vinavyokiuka misingi ya maadili ikiwemo rushwa, kauli mbaya na matumizi mabaya ya madaraka.


“Tujione tunawiwa kuwahudumia watanzania kwani tumepewa dhamana ya kuwatumikia wenzetu kwa uaminifu na uadilifu “Kusaya alisema


Katika hatua nyingine Kusaya amesema atachukua hatua kali kwa baadhi ya watumishi kwenye taasisi chini ya wizara ambapo amebaini kuwa wanajihusisha na vitendo vibaya vya kuwajibu wananchi kwa kauli mbaya.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala Udhibiti wa Viuatilifu (TPRI) Dkt. Magret Mollel amemshukuru Katibu Mkuu kwa kutoa kibali cha kufanyika mafunzo hayo yenye kulenga kuongeza tija na utendaji kazi wa wizara ya kilimo.


Dkt. Mollel alisema kwa siku nne wajumbe wa kamati za uadilifu toka taasisi zote za wizara watashiriki mafunzo ya uadilifu na maadili toka kwa wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais Utumishi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Wizara ya Kilimo Filbert Lutare alisema mafunzo hayo yanahusisha washiriki 130 toka taasisi 23 chini ya wizara na kuwa wizara itahakikisha baada ya mafunzo haya watumishi kwenye taasisi zote wanaishi uadilifu na kuongeza kiwango cha maadili mema katika kuhudumia umma.


Aliongeza kusema kuwa Kamati za Kudhibiti Uadilifu zinaundwa kwa mujibu wa Waraka  wa Katibu Mkuu Kiongozi  wa mwaka 2017 ukilenga kutekeleza Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa Awamu ya Tatu ili watumishi wa umma washiriki kikamilifu na kwa vitendo kupambana na vitendo vya rushwa.

Mwisho
Imeandaliwa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
MOROGORO
29.09.2020







Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger