Friday, 27 December 2019

Iran, Russia na China zaanza mazoezi ya pamoja ya kijeshi kaskazini mwa Bahari ya Hindi

...
Iran, China na Urusi zimeanza mazoezi  ya pamoja ya kijeshi kwenye bahari ya Hindi na ghuba ya Oman katika kile Moscow inachosema ni zoezi lisilotarajiwa la ushirikiano wa majeshi ya majini baina ya mataifa hayo.

Zoezi hilo la siku nne lililofunguliwa katika mji wa bandari wa Chahbahar uliopo kaskazini mashariki ya ghuba ya Oman na karibu na mpaka na Pakistan linanuwia kuimarisha ulinzi katika eneo la bahari ya kanda hiyo.

Eneo la bahari linalozunguka Iran limekuwa kitovu cha mvutano wa kimataifa kufuatia Marekani kuongeza mbinyo dhidi ya mauzo na ushafirishaji wa mafuta ya Iran na kuhimiza biashara nyingine na taifa hilo zisitishwe.

Afisa mmoja wa jeshi la majini la Iran ameiambia televisheni ya taifa ya nchi hiyo kuwa ujumbe wa zoezi hilo ni amani, urafiki na ulinzi na ni ishara kwamba Iran haiwezi kutengwa kimataifa.

Kulingana na televisheni ya Iran, mazoezi hayo yanajumuisha meli za uokozi na mazoezi ya kufyetua makombora.
Luteka kuimarisha uhusiano wa nchi hizo

Hapo jana msemaji wa wizara ya ulinzi ya China Wu Qian alisema mazoezi hayo ya kijeshi yataimarisha mahusiano na ushirikiano wa majeshi ya majini miongoni mwa mataifa hayo matatu.

Kwenye mazoezi hayo China imetuma mfumo wake wa kuharibu makombora uitwao Xining wakati urusi imepeleka meli tatu za kiejshi kutoka kikosi chake cha eneo la Baltiki, mzinga wa kufyetua roketi na boti ya uokozi.

Tehran imekuwa ikitafuta kuimarisha uhusiano wake wa kijeshi na Beijing na Moscow kutokana na kishindo cha vikwazo vya kiuchumi kutoka Marekani.

Luteka hiyo inaonekana kuwa jibu dhidi ya mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa karibuni na Marekani  pamoja na Saudi Arabia ambaye ni mshirika wake katika kanda ya Ghuba.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger