Friday 1 March 2019

AGPAHI YAWAPIGA MSASA WASHAURI WAVIU SIMIYU

...

Afisa wa AGPAHI, Bw. Emmanuel Mashana, akiwezesha mada ya ufuatiliaji wa mahudhurio ya WAVIU CTC katika warsha iliyokutanisha Washauri WAVIU wa mkoa wa Simiyu ili kuwaongezea uweledi katika shughuli zao hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI.
Afisa wa AGPAHI, Bi. Harieth Novat, akiwaonyesha Washauri WAVIU rejesta za miadi ya WAVIU.
Maafisa wa AGPAHI, Harieth Novat (kushoto) na Emmanuel Mashana wakijadiliana jambo wakati wa warsha.
Washiriki wa warsha ya Washauri WAVIU Simiyu wakiendelea na zoezi la kujaza rejesta za miadi ya WAVIU.
Washauri WAVIU wakiwa kwenye kazi za vikundi katika warsha hiyo iliyoandaliwa na AGPAHI.
Washauri WAVIU wakiwa kwenye kazi  ya vikundi katika warsha hiyo iliyojumuisha  Vituo 36 vya kutolea huduma mkoani Simiyu huku wawezeshaji wakikagua ufanisi wa kazi.
Afisa wa AGPAHI, Bw. Emmanuel Mashana akiangalia kazi ya kikundi.

Asasi ya kitaifa inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), imewapiga msasa Washauri WAVIU wa mkoa wa Simiyu ili kuwaongezea uweledi katika shughuli zao hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI.

Mratibu wa AGPAHI mkoa wa Simiyu, Bi. Dafrosa Charles, amesema ili kuwaongezea weledi washauri WAVIU hao hivyo kufanya kazi zao kwa ufanisi, AGPAHI inaendesha warsha ya siku tano mjini Bariadi ili kuwapa stadi na mbinu mbali mbali.

Kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR) chini ya Vituo vya Udhibiti wa Magonjwa na Kinga (CDC), AGPAHI imekuwa ikiisaidia serikali katika kuboresha afya za wananchi hususan wale wanaoishi na VVU. Kwa sasa AGPAHI inafanya kazi katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Mwanza.

Katika warsha hiyo inayojumuisha vituo 36 vya kutolea huduma kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Simiyu (Bariadi DC, Bariadi TC, Maswa DC,Meatu DC na Busega DC) , Washauri WAVIU hao 39 wanakumbushwa kuhusu wajibu na majukumu yao katika kusaidia utendaji wa shughuli kwenye vituo vya kutolea huduma hizo hasa za ufuatiliaji wa watoro katika ngazi ya jamii.

Ili kuweza kufuatilia vyema watu wanaopata huduma za VVU na UKIMWI kwenye vituo vyao, Washauri WAVIU hao wamepimwa uelewa wao kuhusiana na ujazaji wa rejesta ya miadi kwa wateja wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV).

Lengo la zoezi hilo lililoongozwa na Maafisa wa AGPAHI, Bw. Emmanuel Mashana na Herieth Novati, lilikuwa ni kubaini mapungufu katika utumiaji wa rejesta hizo ili kuyashughulikia hivyo kuboresha upatikanaji wa taarifa.

Kufuatia mapungufu yaliyojitokeza maafisa hao kwa kushirikiana na Mratibu wa UKIMWI wa wilaya ya Bariadi, Bi. Joyce Mashauri, waliwaongoza Washauri WAVIU hao katika namna sahihi ya kujaza rejesta hizo kwa ufanisi wa ufuatiliaji wateja.

Aidha Washauri WAVIU hao walipiitishwa kwenye ujazaji rejesta za miadi na ufuatiliaji wa watu wanaotumia huduma za VVU na UKIMWI. “Lengo la mazoezi haya ni kuhakikisha kuwa watakaporejea kwenye vituo vyao, kazi itafanyika kwa ufanisi kwa ufuatiliaji bora wa ufuasi wa huduma na tiba za VVU na upimaji wa wingi wa virusi katika damu,” amesema Bw. Mashana.

Kwa kufahamu kuwa ugonjwa wa kifua kikuu umekuwa ukiwashambulia watu wengi hasa wenye VVU,Washauri WAVIU hao wamefundishwa kuhamasisha matumizi ya dawa za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa usahihi kama kinga kwa wanaostahili.”

Masuala mengine ambayo Washauri WAVIU hao walifundishwa ni pamoja na kuhamasisha upimaji wa familia za wateja wa vituo vya kutolea huduma, vipaumbele katika huduma ya VVU. “Ni matumaini yetu pia kuwa mtawahamasisha wanaume nao kupima, uzoefu unaonyesha ni wanaume wachache tu wenye tabia ya kutafuta huduma za afya,” amesema Bi. Novati.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger