Tuesday, 26 March 2019

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Yatangaza Kuanza Uboreshaji Daftari la Wapiga Kura

...
Na Margareth Chambiri
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kufanya zoezi la uandikishaji wa Wapiga Kura kwa majaribio katika Kata mbili za Kibuta iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani na Kihonda katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mkoani Morogoro.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage Jijini Dar es Salaam leo (Jumanne Tarehe 26. 03. 2019) imesema Uandikishaji huo wa Majaribio utakaoanza Machi 29, hadi Aprili 04, 2019 utafanyika katika vituo 20 vya kuandikisha Wapiga Kura ikiwa ni vituo 10 katika kila Kata.  

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uandikishaji huo unalenga katika kuvifanyia majaribio vifaa na mfumo wa Uandikishaji Wapiga Kura ili kubaini changamoto kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi hilo.

Imezitaja sifa za watu watakaoandikishwa katika uandikishaji huo kuwa ni raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 au atakayetimiza umri wa miaka 18 siku ya Uchaguzi  Mkuu ujao.
Aidha uandikishaji huo hautawahusu raia walio chini ya kiapo cha utii wa nchi nyingine, aliyebainika kuwa hana akili timamu au yuko kizuizini kama mhalifu mwenye ugonjwa wa akili au yuko kizuizini kwa ridhaa ya Rais.

Taarifa hiyo imeendelea kutaja watu ambao hawatahusika katika majaribio hayo ya uboreshaji kuwa ni mtu aliyehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama au anatumikia kifungo kinachozidi miezi sita pamoja na mtu aliyepoteza sifa za kuandikishwa kuwa Mpiga Kura chini ya Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote inayohusu makosa ya uchaguzi.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi pia inawajulisha wakazi wa Kata hizo zinazofanya Uandikishaji wa Majaribio na ambao walijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2015 kuwa wanaweza kutumia fursa hiyo kuhakiki taarifa zao katika vituo walivyojiandikishia.

Wakati huo huo Tume inatoa fursa kwa Vyama vya Siasa kuweka Wakala mmoja  katika kila kituo cha Kuandikishia Wapiga Kura kwa lengo la kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu zitakazotumika pamoja na changamoto zitakazojitokeza ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kabla ya zoezi rasmi la Uandikishaji.

Tume imevitaka Vyama vyenye nia ya kuweka Mawakala katika uandikishaji huu wa Majaribio kuwasilisha orodha ya majina ya Mawakala na vituo walivyopangiwa kwa Maafisa Waandikishaji wa Halmashauri za Kisarawe na Manispaa ya Morogoro.

Kadhalika Vyama vimetakiwa kuwasilisha nakala mbili za barua za utambulisho zikiwa na picha mbili na nakala mojawapo kati ya Kitambulisho cha Taifa au Kadi ya Mpiga Kura, Pasi ya Kusafiria au Leseni ya Udereva na kwamba kila Chama kitagharamia Wakala wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo wakati wa uandikishaji huo wa majaribio Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatumia runinga, redio, mitandao ya kijamii na magari ya matangazo kwa ajili ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura ili kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika zoezi hilo.

Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Kaijage kupitia taarifa hiyo amewaomba wakazi wa Kata za Kibuta na Kihonda kujitokeza kwa wingi katika Uandikishaji huo wa majaribio na kutoa ushirikiano kwa Tume wakati wote wa utekelezaji wa jukumu hilo muhimu kwa mustakabali wa demokrasia ya Taifa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi hufanya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoipa Tume mamlaka ya kusimamia na kuratibu uandikishaji wa Wapiga Kura katika Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Madiwani kwa Tanzania Bara.

Tume kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292 inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na unaofuata. 


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger