Thursday, 10 January 2019

AMRI SAIDI APEWA HESHIMA YA UKOCHA BORA


Dismas Ten na Amri Said
'Huwezi kukataa, Amri Said ni kocha mzuri na bora lakini pia ameongeza kitu ndani ya Biashara United'', maneno ya Dismas Ten msemaji wa Yanga baada ya timu yake kupangwa na Biashara kwenye mchezo wa raundi ya 4 ya kombe la shirikisho.

Dismas amempa heshima hiyo Amri Said ambaye katika mchezo wake wa kwanza tu tangu awe kocha wa Biashara United alishinda 2-1 dhidi ya Mbeya City, hivyo Ten amekiri kuwa Amri Said ameibadilisha timu hiyo.

''Tumepangwa kucheza nyumbani dhidi ya Biashara United, mchezo utakuwa mgumu ukizingatia mabadiliko ya benchi la ufundi ambayo wamefanya Biashara lakini pia lazima uzingatie kuwa waliifunga timu gani'', ameongeza Dismas.

Yanga ambao ni mabingwa wa michuano hiyo msimu wa 2015/16 wametinga raundi ya 4 baada ya kuwatoa Tukuyu Stars ya Mbeya kwa mabao 4-0 huku Amisi Tambwe akifunga Hat-trick.

Amri Said aliifundisha Lipuli FC msimu wa 2017/18 na kuisaidia kumaliza katika nafasi ya 7 ikiwa na alama 38. Msimu huu aliuanza na Mbao FC kabla ya kuachana nayo mwezi Desemba na kujiunga na Biashara United.
Via >>EATV
Share:

STAND UNITED MATUMIZI MAKUBWA KULIKO MAPATO

Timu ya Stand United maarufu kwa jina la chama la wana inayofadhiliwa baadhi ya huduma na kampuni ya vinywaji ya Jambo products,imeelezwa kukabiliwa na changamoto ya kuwa na matumizi makubwa tofauti na mapato hali inayoisababisha timu hiyo kujikongoja kwenye michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara. 

Timu hiyo ambayo imecheza michezo 20 na kupata alama 22 ikiwa nafasi ya 11 kati ya timu 20 zinazoshiriki ligi kuu soka Tanzania bara. 

Mwenyekiti wa timu hiyo dokta Ellyson Maeja alisema timu hiyo katika mzunguko wa kwanza msimu huu wamepata fedha kutoka wadhamini mbalimbali jumla ya kiasi cha shilingi milioni 53.6 (Azam milioni 27,BIKO milioni 13,viingilio mechi za nyumbani milioni 3.6). 

Maeja aliongeza kwamba bajeti ya mishara ya wachezaji na benchi la ufundi imekuwa ikishuka kila wakati na hali inayowanja moyo. 

“Bajeti ya mishara mwezi Agosti 2018 ilikuwa milioni 16.3 kwa mwezi,lakini imeshuka kufikia milioni 14, na tunaendelea kushusha ingawaje kubana mkaa sana napo ni shida”, Alisema Maeja. 

Kampuni ya vinywaji ya Jambo Products inaifadhili timu hiyo huduma ya usafiri ndani na nje ya mkoa, chakula pindi timu inapokuwa ndani ya mkoa wa Shinyanga,  huduma ya maji ya kunywa na jezi za wachezaji. 

Wadau wa soka mkoai Shinyanga wamemuomba mfadhili huyo kufadhili mambo ambayo ni changamoto kwa timu hiyo kama vile fedha ya mishahara pamoja na usajili kwa wachezaji. 

Wadau hao wa soka wanakutana januari 10 2019 kujadili na kuweka mikakati ya kuinusuru timu hiyo na hali mbaya ya kiuchumi na kuleta ushindani katika ligi kuu soka Tanzania bara nakuendlea kuwanufaisha wakazi wa mkoa wa shinyanga kiuchumi. 

Na Malaki Philipo - Malunde1 blog


Share:

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU SHULE BINAFSI KUFUKUZA WANAFUNZI WASIOLIPA ADA


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amepiga marufuku wanafunzi wa shule binafsi ambao hawajamaliza ada kusimamishwa au kufukuzwa shule.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamisi Januari 10, 2019, jijini Dar es Salaam, Waitara amesema kuanzia kesho Ijumaa ataanza kupokea taarifa kutoka kwa katibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri na wadhibiti ubora wa shule ambazo zimewafukuza au kuwarudisha wanafunzi.

Amesema ni marufuku mwanafunzi kusimamishwa au kufukuzwa shule kwa sababu ya kutolipa ada bila kujali anasoma shule ya umma au binafsi.

Waitara amesema jambo jingine ambalo Serikali haikubaliani nalo ni la wazazi kulazimishwa kulipa ada kwa mkupuo na iwapo hawajafanya hivyo wanafunzi hawataendelea na masomo hata kama mwaka uliopita walifanya hivyo.

"Nina sms (ujumbe mfupi wa maandishi) nilizotumiwa na wazazi wa shule ambazo zimerudisha wanafunzi nyumbani kwa kukosa ada na malipo mengine ya kiholela kama vile kulazimishwa kununua sare za shule shuleni, for figer, rim na madaftari ya ganda gumu (counter book),” amesema Waitara.

“Nataka maofisa elimu, wakurugenzi na makatibu tarafa kwenda kwenye hizi shule (anazitaja shule) hadi kufikia kesho niwe na majibu yanayoonyesha kupatikana ufumbuzi."

Waitara pia amewataka wazazi ambao watoto wao wamerudishwa kwa ajili ya kutolipa au kukamilisha ada wafike kwenye ofisi alizozitaja au Tamisemi kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

Naibu waziri huyo amesema kuna haja ya kurudisha mjadala wa ada elekezi.

"Nafanya utaratibu kurudisha mjadala wa kuangalia namna ambavyo Serikali itatoa msimamo wa ada elekezi kwa sababu kuna shule zinatoza kuanzia Sh1.5 milioni hadi Sh6 milioni na zinasema zinatoa huduma," amesema Waitara.

Na Kalunde Jamal, Mwananchi
Share:

KIKONGWE AUWAWA KIKATILI NA KUKATWA SEHEMU ZA SIRI

Na Allawi Kaboyo-Bukoba Kagera. Watu wawili wamepoteza maisha katika mauaji tofauti Mkoani Kagera akiwemo Laurian Kakoto(80)mkazi wa Kijiji cha Ihunga Kata ya Kishanda aliyeuawa na kuzikwa kwa kutanguliza kichwa akiwa amekatwa koromeo na kuondolewa sehemu za siri. Akifafanua matukio hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Revocatus Malimi amesema tukio la kwanza lilitokea mnamo tarehe 08/01/2019 linahusishwa na imaani za ushirikina ambapo mwili wa marehemu Kakoto ulikutwa umefukiwa kwenye shimo la mita moja kwenye shamba la mahindi. Kamanda Malimi amesema marehemu aliondoka nyumbani kwake tarehe 7,Januari,2019 kwenda kununua mchele na…

Source

Share:

TETESI ZA SOKA ULAYA 10.01 2019,AARON RAMSEY AMEKUBALI KUJIUNGA NA JUVENTUS MWEZI JUNI

Kiungo wa kati wa Arsenal na Wales Aaron Ramsey, 28, amekubali kujiunga Juventus mwezi Juni mwaka huu. (Guardian)

Atletico Madrid imeingia katika kinyang'anyiro cha kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Uhispania Alvaro Morata, 26.

Kuna tetesi kuwa Morata huenda akajiunga na Sevilla. (Goal)

Real Madrid wanajiandaa kutoa ofa ya euro milioni 9 kumenyana na mahasimu wao Manchester United katika juhudi za kumnunua mlinzi wa Napoli na Senegal Kalidou Koulibaly, 27. (Il Mattino, via Talksport)

Azma ya United ya kumnunua mlinzi wa Fiorentina na Serbia Nikola Milenkovic, 21, huenda imefifia baada ya Jose Mourinho kutimuliwa kutoka klabu hiyo. (ESPN)

Burnley wanakadiria kuwa thamani ya mlinzi wa England James Tarkowski, 26 ni euro milioni 50 japo Liverpool wanapania kumchukua kiungo huyo kwa mkopo. (Sun)

Mchambuliaji wa Southampton, mtaliano Manolo Gabbiadini, 27, amekubali kujiunga tena na Sampdoria kwa kima cha euro milioni 11.7. (Guardian)

Share:

MGOMBEA WA URAIS DRC MARTIN FAYULU APINGA MATOKEO YA UCHAGUZI WA URAIS CONGO

Martin Fayulu, mgombea urais wa upinzani DRC aliyeibuka wa pili, ameyakataa matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) yanaonesha Felix Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na anatangazwa mshindi mteule wa urais.

Bw Tshisekedi alipata zaidi ya kura 7 milioni naye Bw Fayulu akapata kura takriban 6.4 milioni, huku mgombea wa serikali Emmanuel Ramazani Shadary akimaliza wa tatu akiwa na takriban kura 4.4 milioni.


Bw Fayulu ameambia Idhaa ya Kifaransa ya BBC kuwa: "Hii ni kashfa mbaya sana. Matokeo haya hayana uhusiano hata kidogo na ukweli halisi. Raia wa Congo hawataukubali utapeli kama huu daima. Felix Tshisekedi hakupata kura 7 milioni, haiwezekani. Alizitoa wapi?"

Chanzo:Bbc
Share:

JPM ASOMA SMS ZA WATEULE WAKE " ENDELEENI KUGOMBANA TU...MTAGOMBANIA VIJIJINI SIKU MOJA'


Rais John Magufuli jana alieleza jinsi alivyosoma meseji za watendaji wake serikalini na kubaini baadhi yao wanagombana badala ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika maeneo yao.

Alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua.

Alitoa mfano jinsi alivyosoma meseji za majibizano kati ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, (Tamisemi), Zainabu Chaula ambaye jana aliapishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya.

“Nilikuwa nazisoma meseji; meseji ya Waziri wa Afya na meseji ya Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, wanajibizana wee na wote wanatoka Tanga. Huyu mwingine anakaa kimya, huyu mwingine anashindilia maneno, nikaona nani anashindiliwa maneno zaidi, nikasema hawa njia ya kuwakomesha niwaweke wizara moja,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wote wawili wanafanya kazi vizuri, hivyo ameona bora wakae wizara moja. Alimpongeza Chaula kwa jitihada zake za kusimamia ujenzi wa hospitali zaidi ya 300 ndani ya miaka mitatu.

Mbali ya viongozi hao, Rais Magufuli pia alisema anafahamu jinsi watendaji katika baadhi ya halmashauri wanavyogombana. Alitolea mfano Halmashauri ya Nyasa ambako alisema mkurugenzi na mkuu wa wilaya hawaivi.

Alitaja mgogoro mwingine kuwa uko Gairo ambako alisema mbunge wa anagombana na mkuu wa wilaya. Mbunge wa Gairo ni Mbunge wa jimbo hilo Ahmed Shabiby (CCM), na Mkuu wa Wilaya ni Siriel Mchembe.

Alisema mbunge amefikia hatua ya kutuma maneno ya kumtukana DC na kusema anashindwa kuelewa kwamba kuna kamati za nidhamu za CCM ambazo zinaweza kumfanya apoteze ubunge. 

“Nimewaangalia tu, I hope (natumai- mbunge) atafika siku moja aombe msamaha kwenye Bunge,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Pale Dodoma, mkurugenzi wa Jiji na DC walikuwa wanagombana, nika-send message (nikatuma ujumbe) kwamba ‘endeleeni kugombana tu, mtagombania vijijini siku moja. Wamenyamaza naona yameisha,”

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ni Godwin Kunambi na DC ni Patrobas Katambi.


Na Peter Elias, Mwananchi
Share:

RAIS TRUMP AONDOKA KWA HASIRA KWENYE MKUTANO NA WANADEMOCRATICS

Rais Trump wa Marekani anaelekea katika mpaka na Mexico ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kujenga ukuta,siku moja baada ya kutoka katika mkutano wa majadiliano wakati wapinzani wa ujenzi huo kutoka chama cha Democratic 

Donald Trump alivurumuka na kutoka katika mkutano na viongozi wa mabaraza ya bunge la Marekani " nilisema kwaheri," aliandika katika ukurasa wa Twitter muda mfupi baada ya mkutano huo, wakati juhudi za kumaliza kufungwa kwa sehemu shughuli za serikali, ziliingia katika mparaganyiko mkubwa. 

Mamia kwa maelfu ya wafanmyakazi wa serikali wanakabiliwa sasa na kukosa mishahara hadi kesho Ijumaa.


Wakati atakaposimama kwa muda leo mjini McAllen , Texas , Trump atafanya ziara katika kituo cha mpakani cha doria kwa ajili ya mazungumzo kuhusiana na uhamiaji na usalama wa mpakani, na kupata maelezo kuhusu usalama wa mpaka.

 Lakini Trump ameelezea shaka shaka yake kwamba kujitokeza kwake pamoja na matamshi hayatabadilisha mawazo ya mtu yeyote, wakati akitafuta kupata dola bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta ambao umekuwa ni ahadi yake kuu tangu alipokuwa akifanya kampeni ya urais.

Mazungumzo hayo yalizusha uvumi zaidi juu ya iwapo Trump atatangaza dharura ya kitaifa na kujaribu kuidhinisha ujenzi wa ukuta huo binafsi iwapo baraza la Congress halitaidhinisha fedha anazotaka.

Chanzo:DW
Share:

RAIS TRUMP AKAZIA UJENZI WA UKUTA, ALITAKA BUNGE KUIDHINISHA DOLA BILIONI 5.7

                     Rais wa Marekani Donald Trump.

 Rais wa Marekani Donald Trump wanawake na watoto ni waathirika wakubwa wa mfumo ulioharibika kukabiliana na usafirishaji haramu wa watu akisema idara za doria mpakani hazina tena nyumba za kuwapatia hifadhi wahamiaji na haziwezi kuendelea na utaratibu kwa watu wanaotafuta hifadhi.

Trump anasema kuna mzozo wa kibinadamu na usalama unaoendelea kuwa mkubwa kwenye mpaka wa Marekani na Mexico akiueleza kuwa ni mzozo wa moyo na kiroho.

Katika hotuba yake ya kwanza ya kitaifa kutoka chumba cha Oval Office ndani ya White House Rais Trump alifafanua hoja yake ya kujenga ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico lakini hakutangaza hali ya dharura ya kitaifa ambayo itamruhusu kujenga ukuta bila idhini ya bunge.


Alisema wakati wamarekani wanaumizwa kutokana na kile alichokieleza kutodhibitiwa wahamiaji haramu Rais Trump alisema wamarekani wenye asili ya Kiafrika na asili ya Amerika Kusini wanaathirika zaidi kwa sababu fursa za ajira zimechukuliwa na wahamiaji.


Trump alisema wanawake na watoto ni waathirika wakubwa wa mfumo ulioharibika kukabiliana na usafirishaji haramu wa watu akisema idara za doria mpakani hazina tena nyumba za kuwapatia hifadhi wahamiaji na haziwezi kuendelea na utaratibu wote kwa watu wanaotafuta hifadhi.

Chanzo:Voa


Share:

WENGER KUREJEA KWENYE UKOCHA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA 2022

Arsene Wenger.

Meneja wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger anajipanga kurudi katika kazi yake ya ukocha, huku ripoti zikieleza kuwa ataifundisha Timu ya Taifa ya Qatar katika kuelekea michuano ya Kombe la Dunia la 2022.

Wenger amehusishwa na tetesi kadhaa za kufundisha timu mbalimbali zikiwemo PSG, Real Madrid tangu alipoondoka Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita, akisisitiza kuwa anahitaji changamoto mpya na kwamba Qatar inajipanga kuchukua fursa ya hali hiyo na kumvuta mfaransa huyo.

Kwa mujibu wa mtandao wa France Football, Qatar inajipanga kumnyakuwa kocha huyo kwaajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 ambayo itafanyika nchini humo.

Habari za maslahi ya Qatar hutoka kwa Soka la Ufaransa, ambao wanasema kuwa Qatar ni nia ya kurekebisha timu yao ya kitaifa ya kuweka mbele ya Kombe la Dunia ya 2022.

Kocha huyo alinukuliwa miezi kadhaa iliyopita, akisema kuwa anatamani kurejea katika kazi yake mapema mwaka huu 2019 baada ya kuwa amepumzika kwa kipindi cha kutosha.

Arsene Wenger (69) alihudumu miaka 22 na klabu ya Arsenal, akiiongoza klabu hiyo kushinda mataji matatu ya EPL na mataji saba ya FA.
Share:

MANJI KURUDI KIVINGINE YANGA

Mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa klabu ya Yanga, Dr. Jonas Tiboroa amejinasibu kurejesha mfumo wa zamani wa klabu hiyo ambao utaruhusu klabu kuwa na kampuni mbili za kibiashara.


Katika muendelzo wa kampeni zake kuelekea uchaguzi huo, Dr. Tiboroa amesisitiza kuwa klabu ya Yanga itaendelea kuwa ya wanachama huku kukiwa na kampuni mbili, kampuni moja itakuwa inahusika katika uwekezaji na nyingine ambayo itahusika na biashara za klabu.

"Mimi nilipokuwa Katibu Mkuu chini ya Manji tulisema tutahakikisha kuwa Yanga inakuwa klabu ya wanachama na tukaanzisha kampuni mbili, moja inayoshughulikia uwekezaji na nyingine inayoshughulikia biashara za klabu", Alisema Dr. Tiboroa

"Hizi kampunni tulizisajili mwaka 2015, lakini kwa bahati mbaya kizo kampuni zote hazijafanya kazi mpaka sasa, ndiyo maana mimi nimeona kuna haja ya kurudi nikaendeleze yale niliyoyaanza", aliongeza Dr. Tiboroa.

Endapo Dr. Tiboroa atachaguliwa na mpango huo kukamilika, maana yake wawekezaji kama Yusuph Manji na wengine wanaweza kupata nafasi ya nafasi ya kuwekeza katika klabu hiyo bila kuathiri mfumo wake wa uanachama kwakuwa shughuli zote zitaratibiwa chini ya kampuni ya uwekezaji ya klabu.

Uchaguzi wa Yanga unatarajia kufanyika Januari 13, 2019 kwenye ukumbi wa bwalo la maafisa wa polisi Oysterbay Dar es salaa, ambapo nafasi ya Uenyekiti wa klabu inashindaniwa na wagombea wawili, Dr. Jonas Tiboroa na Baraka Igangula.

Chanzo:Eatv
Share:

SAMAKI AUA MTU


Katika mji wa Brooklyn nchini Marekani, kumekumbwa na mkasa wa mama anayedaiwa kupika samaki na harufu iliyotoka, imemuua mwanawe mdogo.

Hadi sasa suala hilo liko katika uchunguzi mikononi mwa mamlaka za kiserikali kupata ukweli wa kifo hicho, kilichoanzia kwa mtoto mhusika mwenye miaka 11 kuugua ghafla, kulegea kwa muda na kupoteza fahamu.

Mtoto Cameron Jean-Pierre, anadaiwa alikuwa na historia ya aleji ya samaki na katika siku ya Mwaka Mpya wiki moja na nusu iliyopita, mama yake alikuwa anaandaa mapishi, harufu ilimfikia mtoto aliyeanguka na kuzimia, mahali hapo anakoishi bibi yake.

Hadi sasa wachunguzi wa kitabibu hawajatoa ufafanuzi kuhusu kilichojiri katika afya ya mtoto huyo ambaye ameshafariki, ingawaje wanafamilia wanakazania chanzo cha kifo hicho ni maradhi ya pumu.

Mama wa mtoto huyo, Jody Pottingr, anasimulia kwamba mwanawe alianza kuugua nyumbani kwa bibi yake, pale binafsi alikuwa alikaanga aina ya samaki hao wa asili.

Mzazi huyo anahisi samaki huyo aliguswa na kitu ambacho kina mtazamo wa sumu kwa samaki wake na ndicho kilicholeta athari inayotajwa na aleji inayotajwa mtoto huyo, iligunduliwa kupitia uchunguzi wa kiafya shuleni, siku moja alivyojisikia vibaya baada ya mlo wa mchana .
Share:

HUYU NDIYE FELIX TSHISEKEDI MSHINDI WA URAIS CONGO

Share:

ANAYEDAIWA KUUA MWALIMU AFIKISHWA MAHAKAMANI


Mtuhumiwa Seif Salimu anayedaiwa kuhusika na mauaji ya mwalimu wa Shule ya Msingi ya Mailisita Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Dinna Lekule, miaka 12 iliyopita amekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hai.

Mwendesha Mashtaka, Meja Lebulu Mbise aliiambia mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Devota Msofe kuwa mshtakiwa Salimu, maarufu kwa jina la Sharifu, alitenda kosa hilo usiku wa Agosti 21, 2007 nyumbani kwa marehemu Mailisita.

Hata hivyo, mshtakiwa ambaye ni mkazi wa kijiji cha Doma Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, hakutakiwa kujibu lo lote katika kesi hiyo, ambayo aliiahirisha hadi Januari 21, mwaka huu itakapotajwa tena.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, mume wa marehemu, Dk Redfan Shao wa Hospitali ya Wilaya ya Hai, alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.

Alisema kutokana na tukio hilo, alikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa miezi 10, akituhumiwa kumuua mkewe.

Alisema, hata hivyo, siku ya tukio hilo alikuwa Handeni katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni kikazi.

Alisema, baada ya tukio hilo alipigiwa simu na kurejea nyumbani Agosti 22 na kujikuta akitiwa mbaroni, akihusishwa na mauaji hayo.

 Dk Shao alisema, baada ya upelelezi Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mahakama, walijiridhisha kuwa hakuhusika na mauaji hayo na kumwachia huru baada ya miezi 10 na sasa anaendelea na kazi katika Hospitali ya Wilaya ya Hai.

Akisimulia kifo cha mkewe, Dk Shao alisema, marehemu alipigwa na kitu chenye ncha kali kichwani, alivunjwa mkono wa kushoto mara mbili na kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani.

Alisema, vitu kadhaa viliibiwa katika nyumba yake ikiwamo televisheni moja aina ya Panasonic, redio, vifaa vya kompyuta na pasi ya umeme.

Na Nakajumo James - Habarileo
Share:

SAKATA LA KUDHALILISHA BUNGE : NDUGAI AMPA BARUA YA WITO CAG..MAALIM SEIF NAYE AKOMAA

 Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema ofisi yake tayari imeshaandika barua ya wito kwenda ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikimtaka kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga na Haki ya Bunge ili kuhojiwa.

Hatua hiyo imekuja siku tatu baada ya Spika Ndugai kumtaka CAG, Profesa Mussa Assad kufika mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli yake kuwa chombo hicho cha kutunga sheria hakitekelezi ipasavyo majukumu yake ya kuisimamia Serikali.

Profesa Assad, ambaye ametakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Januari 21, alitoa kauli hiyo alipohojiwa na idhaa ya Kiswahili ya kituo cha televisheni cha Umoja wa Mataifa (UN), wakati alipokuwa jijini New York, Marekani kuhudhuria mkutano wa jopo la wakaguzi wa nje.

Mbali na CAG, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee naye ameitwa mbele ya kamati hiyo Januari 22 kwa madai ya kutoa kauli iliyounga mkono kilichosemwa na Profesa Assad.

“Tayari tumeshamwandika barua yaani summons (hati ya wito), maana wito wetu unaenda kama wa kimahakama vile,” alisema Ndugai kwa njia ya simu jana, muda mfupi baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa mawaziri wawili na wateule wengine wa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam.

Wakati Ndugai akisema hayo, katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif amemtaka Ndugai kumuomba radhi Profesa Assad akisema kilichofanywa na CAG ni kutimiza wajibu wake na si kulidhalilisha Bunge.


Na Bakari Kiango, Mwananchi 
Share:

LORI LAGONGA TRENI DODOMA

Na.Alex Sonna,Dodoma
Watu wawili wamenusurika kifo baada ya lori aina ya scania walilokuwa wakisafiria kutoka Dodoma kwenda Iringa kuigonga treni ya mizigo katika makutano ya reli na barabara eneo la hazina jijini Dodoma.


Tukio hilo lilitokea jana mchana mara baada ya lori hilo lenye namba za usajili T463 ADW likiwa na tela lenye usajili T483 BLP kuiigonga treni hiyo iliyokuwa ikitoka jijini Dar es salaam kuelekea mikoa ya kanda ya ziwa.


Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wamesema kuwa ajali hiyo imechangiwa na mvua zilizokuwa zikinyesha na kumfanya dereva wa lori kutoona kizuizi cha treni mbele yake.


Mmoja wa mashuhuda hao Ramadhani Rashid Mkazi wa Majengo amesema kuwa ajali hiyo ilichangiwa na dereva wa lori kutaka kukatiza kwa mwendo mkali lakini alikuwa kacheleWa hali iliyosababisha kugongwa na treni hiyo ya
mizigo.


“Dereva wa lori alikuwa katika mwendo mkali wakati akikatiza kivuko cha reli hivyo alishindwa kusimama na treni likawa limekaribia na kumgonga tumetoa watu wawili wakiwa wamejeruhiwa vibaya mwingine mmoja utumbo ukiwa nje”alisema


Kaimu kamanda wa polisi mkoani Dodoma ACP William Mkonda, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema chanzo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi na majeruhi wamelazwa katika hosipitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma
Share:

TUME YA UCHAGUZI YAMTANGAZA TSHISEKEDI KUWA MSHINDI WA URAIS CONGO

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Congo (Ceni) imetangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo yanayoonesha mgombea wa upinzani Felix Tshisekedi ameshinda kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 30 mwaka uliopita.

Tshisekedi amemshinda mgombea mwingine wa upinzani Martin Fayulu, pamoja na mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na serikali ya Rais anayemaliza muda wake, Emmanuel Shadary.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Ceni) Corneille Nangaa, mapema leo Alhamisi amesema kwamba kwamba Bw Tshisekedi amepata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na kumtangaza rasmi kuwa Rais mteule wa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini na mafuta.


Tshisekedi anatokea katika muungano wa kisiasa na aliyekuwa mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation), Vital Kamerhe ambaye atakuwa ni Waziri Mkuu wa serikali yao kwa mujibu wa makubaliano yao.


Ripoti zinaeleza kuwa mshindi wa kwanza (Felix Tshisekedi) amepata kura takriban milioni 7, huku mshindi wa pili (Martin Fayulu akipata kura takriban milioni 6.4 milioni na mgombea wa tatu ambaye anaungwa mkono na Rais Joseph Kabila (Emmanuel Ramazani Shadary) akipata takriban kura millioni 4.4.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger