Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema amani na usalama ni msingi mkuu wa maendeleo ya Taifa, akiwataka wananchi kuendelea kulinda tunu hizo ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na mazingira bora ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
Rais Samia amesema hayo leo Jumatatu Julai 20, 2026 mkoani Kigoma wakati akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora hadi Kigoma na uzinduzi wa meli nne za mizigo katika Bandari ya Kigoma.
Amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya usafiri na usafirishaji, lakini mafanikio ya miradi hiyo yanategemea uwepo wa amani na usalama nchini huku akisisitiza kuwa suala hilo ni kipaumbele cha kwanza na halipaswi kupuuzwa kwani maendeleo hayatashamiri endapo amani itavurugwa.
Amewataka wananchi wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kuweka usalama mbele, akisisitiza kuwa maendeleo yanahitaji mazingira yenye utulivu na mshikamano.
Rais Samia pia amewataka wananchi kutokubali kushawishiwa au kutumiwa na watu wenye nia ya kuvuruga amani ya nchi, akieleza kuwa kulinda usalama ni jukumu la kila Mtanzania na kuwataka wote kuwa macho huku wakiepuka kuwa wasaliti na maadui wa nchi yao.
Ameongeza kuwa ulinzi wa amani na usalama utaendelea kuiwezesha Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.

0 comments:
Post a Comment