Amewatahadharisha pia watendaji wa halmashauri zote nchini kutotumia fedha za miradi zinazopelekwa na serikali kinyume na malengo kutokana na kuimarishwa kwa mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi yake na thamani ya miradi itakayojengwa.
Aliyasema hayo alipozungumza na watumishi na watendaji wa manispaa hiyo, huku akiweka bayana kwamba halmashauri hiyo inaongoza kwa kuwa na watumishi wa Mikataba, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za utumishi.
Akiendelea na mkutano huo, ghafla Waziri Mkuu alimsimamisha Kaimu Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Zaituni Hassan na kumuuliza idadi ya watumishi wa Mikataba katika halmashauri hiyo ambapo ofisa huyo alijibu kuwepo kwa watumishi 89.
Jibu hilo lilimfanya Waziri Mkuu kuhoji sababu ya kuwepo kwa idadi kubwa hiyo na kujibiwa kuwa hatua hiyo ilitokana na wengi wao kukosa sifa za kuajiriwa huku akisema wengi wao ni madereva.
Zaituni aliendelea kumwambia Waziri Mkuu kwamba mwaka jana Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ilitangaza nafasi za kazi na kuwataka watumishi hao kuomba lakini walishindwa kufikia vigezo vilivyowekwa na kusababisha halmashauri kuendelea kuwatumia bila kuwaajiri.
Pamoja na maelezo hayo, Waziri Mkuu alieleza kushangazwa na hatua ya kutokuwepo kwa madereva waliohitimu Kidato cha Nne ambao wangeweza kuajiriwa, hata hivyo Ofisa Utumishi huyo alimwambia waliopo wana elimu ya Kidato cha Nne lakini hawana vyeti vya mafunzo ya udereva kutoka Chuo cha Elimu na Mafunzo Stadi (VETA).
Majaliwa alieleza kuwa wanaotakiwa kuajiriwa kwa Mikataba ni walimu wa Masomo ya Sayansi na watendaji wa mitaa hivyo kama madereva hao hawana sifa ni vyema wakaondolewa kwa vile wanaziba nafasi za watu wenye sifa za kuajiriwa.
Alisema kutokuajiriwa ni moja ya sababu za kuwepo watumishi hewa hivyo alisema hadi kufikia Julai 30, mwaka huu, Ofisa Utumishi huyo awe amejiridhisha kuhusiana na sifa za watumishi hao ili wasio na sifa waondolewe na wenye sifa waajiriwe huku akisema zoezi hilo lifanyike katika idara zote.
Alimtaka kuanza taratibu za kumuomba Katibu Mkuu wa Utumishi kibali cha kuwaajiri watumishi hao na kusema ametoa nafasi hiyo kwa kuwa watumishi wengi katika halmashauri hawana mwelekeo mzuri kutokana na kutoajiriwa, hivyo wasio na sifa waondoke ili watafutwe wenye nazo.
Akizungumzia fedha zinazopelekwa katika halmashauri, Waziri Mkuu alisema kila fedha inayoingia katika halmashauri itakuwa na maelekezo ya matumizi na Mkurugenzi atalazimika kutoa nakala ya maelezo hayo na kumpatia Mkuu wa Wilaya ili ajue matumizi ya kila shilingi na thamani ya miradi.
Alisema baada ya kumaliza uteuzi wa viongozi mbalimbali, sasa Serikali inaanza kupeleka fedha za maendeleo katika halmashauri zote ili utekelezaji wa shughuli za maendeleo uendelee.