Friday 26 July 2024

SHIRIKA LA IUCN LAUNGANA NA SERIKALI KUTEKELEZA MRADI WA 'BAHARI MALI'

...
Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Buriani amesema serikali ina mpango wa kupanda miti aina ya mikoko 250 kila mwezi.

Dkt. Buriani ameyasema hayo leo Julai 26, 2024 wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Mikoko Duniani, ambapo mkoani Tanga imeadhimishwa kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi, eneo la Sahare, jijini Tanga.


Amesema mpango huo utatekelezwa kupitia mradi wa Bahari Mali unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na shirika lisilokuwa la kiserikali la International Union for Conservation Nature (IUCN).


Aidha Dkt. Burian, amesema uboreshaji wa mazingira ya bahari ni muhimu kutokana na mchango wake katika kuzifanya fukwe kuwa nzuri zenye kuvutia. Pia amesema uwepo wa mikoko unatoa uhakika wa mazingira bora ya matumbawe na mazalia kwa viumbe wa baharini hususani samaki.


"Pamoja na kuboresha mazingira ya bahari, mikoko inachangia uzalishaji wa hewa ya ukaa yenye manufaa makubwa kiuchumi na uhifadhi wa mazingira yetu" amesema Dkt. Buriani.


Naye Meneja Mradi wa Uhifadhi wa Bahari wa IUCN, Joseph Olila, amesema mradi huo unatekelezwa katika Wilaya mbili za Pangani na Mjinga, lakini pia unatekelezwa Micheweni katika kisiwa cha Pemba.


"Miongoni mwa manufaa ya mradi huo ni ongezeko la mapato kwa jamii na ukuaji wa uchumi wa bluu, urejeshwaji wa mikoko iliyotoweka, utawala katika sekta ya bahari na kutengeneza mipango ya uvuvi endelevu" amesema.


Akisoma risala kwa niaba ya Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, James Nshale, Mhifadhi Misitu Mkoa wa Tanga , Lawrence Bryson amesema, uwezo wa mikoko katika udhibiti wa hewa chafu ni mara tano zaidi ya misitu iliyopo nchi kavu.


"Lakini pia manufaa ya mikoko yapo kwenye utengenezaji wa asali bora na kupelekea kuibuliwa kwa utalii wa mikoko baharini" amebainisha Mhifadhi huyo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger