Tuesday 25 July 2023

VIFAA VYA MAWASILIANO 108,395 VYAFUNGWA

...

Na Mwandishi Wetu - Dodoma

JUMLA ya simu na vifaa vingine vya mawasiliano 108,395 vimezuiliwa kupokea na kutoa mawasiliano katika kipindi cha mwaka mmoja, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kujihusisha na ulaghai, vitendo vya udanganyifu, kuibiwa, wizi, na kuripotiwa kuibiwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dodoma wiki iliyopita kuwa, TCRA imekuwa macho katika kutambua vifaa vya mawasiliano vinavyotumiwa nchini kwa kuhakikisha vinatumika katika huduma za mawasiliano kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.


“TCRA imesimamia zoezi la kuzuia matumizi ya simu zilizoripotiwa kuibiwa, kupotea au kuharibika pamoja na kuzuia matumizi ya simu zisizokuwa na viwango. Usimamizi huu unawezesha kubaini na kufungia namba tambulishi za vifaa vya Mawasiliano zilizonakiliwa (Duplicate International Mobile Equipment Identity-IMEIs), namba tambulishi za vifaa vilivyotumika kwenye udanganyifu pamoja na namba tambulishi zilizotolewa taarifa ya kupotea au kuibiwa,” alisisitiza Dkt Jabiri katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma.


Alisisitiza kuwa, kuanzia Julai 2022 hadi Juni 2023 jumla ya namba tambulishi zilizofungiwa na mfumo wa utambuzi wa namba hizo ni 108,395 ambazo ziliripotiwa kupotea, kuibiwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu, hivyo kuwezesha kupunguza matukio ya wizi na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya Mawasiliano vyenye ubora kwenye soko.


Kuhusu kubainisha simu za ulaghai Mkurugenzi Mkuu Jabiri alisema kuwa, TCRA imeendelea kubaini simu za ulaghai zinazoingia hapa nchini na hatua stahiki zimekuwa zikichukuliwa. “Kutokana na hatua hiyo, idadi ya simu za udanganyifu imeendelea kupungua kuanzia mwaka 2020 hadi Juni 2023. Hata hivyo, tulibaini matukio machache ya simu za ulaghai yalitokea mwezi Septemba, 2022 kama inavyoonekana kwenye Jedwali hapo chini,” alisema.


Kuhusu Usimamizi wa simu za ndani na kimataifa Jabiri alisema Idadi ya dakika za simu za kimataifa zinazoingia nchini (International Incoming) zimepungua kutoka dakika 3,136,692 mwezi Julai 2022 hadi kufikia 2,900,165 mwezi Juni 2023 ambayo ni sawa na asilimia 7.54%, idadi ya dakika za simu za kimataifa zinazotoka nchini (International Outgoing) zimepungua kutoka dakika 2,405,522 mwezi Julai 2022 hadi kufikia dakika 2,226,071 mwezi Juni 2023 ambayo ni sawa na asilimia 7.46%.


“Kupungua kwa simu za kimataifa kunasababishwa na mabadiliko ya teknolojia na upatikanaji wa chaguzi mbadala za kupiga simu kupitia mitandao ya intaneti kama vile Whatsap, Facebook, Telegram, Zoom nakadhalika,” alibainisha.


Alibainisha kuwa idadi ya dakika za simu za kitaifa ndani ya mtandao mmoja (onnet) zimeongezeka kutoka dakika 6,172,696,579 mwezi Julai 2022 hadi dakika 7,012,574,045 mwezi Juni 2023 ambayo ni sawa na 13.61%.


“Hivyo hivyo idadi ya dakika za simu za kitaifa nje ya mtandao mmoja (offnet) zimeongezeka kutoka dakika 4,879,102,325 mwezi Julai 2022 hadi kufikia dakika 5,064,800,480 kufikia mwezi Juni 2023 ambayo ni sawa na 3.81%. Ongezeko la simu za kitaifa linasababishwa na ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini,” aliongeza.


Mamlaka hiyo yenye jukumu la kusimamia huduma za mawasiliano nchini ilianzishwa mwaka 2003 kwa Sheria namba 12 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania, ikianzishwa baada ya kuunganishwa kwa zilizokuwa Tume ya Mawasiliano na Tume ya Utangazaji nchini. TCRA inasimamia sekta ndogo za simu na Intaneti, huduma za Utangazaji na Posta, ambapo hutoa taarifa ya mwenendo wa sekta kila Robo ya Mwaka wa Fedha na Mwaka mzima ambapo zamu hii Mkurugenzi Mkuu Bakari alikuwa akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya Usimamizi wa Sekta ya Mawasiliano nchini kwa mwaka mmoja uliopita yaani 2022/2023.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger