Monday, 31 July 2023

AUAWA KWA KUKATWA KICHWA AKICHUMA MBOGA

...


MKAZI wa Kijiji cha Mgongola A Kata ya Kwamgwe wilayani Handeni mkoani Tanga, ameuawa kwa kukatwa kichwa na watu wasiojulikana wakati akichuma mboga shambani.

Akizungumzia tukio hilo lililotokea juzi Julai 29, 2023 kijijini hapo Diwani wa Kwamgwe, Sharifa Abebe amesema mwanamke huyo wa kabila la Kimang’ati alikuwa akichuma mboga ndipo alipouawa kwa kukatwa shingo huku akiwa na mtoto mdogo wa mwezi mmoja na nusu mgongoni.

“Kichwa mpaka sasa hakijajulikana kilipo lakini juhudi za polisi zinaendelea. Ukweli ni kwamba hatujajua nini kilisababisha mauaji haya kwa kweli,” ameeleza Abebe.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya, Albert Msando aliyefika eneo la tukio kwa pikipiki, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kueleza kuwa hadi sasa watu watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi huku juhudi ya kutafuta kichwa cha marehemu zikiendelea.

“Mpaka sasa hivi chanzo cha mauaji hayo hatujajua ni nini na Jeshi la Polisi tangu juzi linaendelea na upelelezi,” amesema.

Alisema kwa ujumla hali ya usalama katika kijiji hicho ni nzuri japokuwa juzi wanakijiji hao walikusanyika wakiwa na silaha za jadi na kufanya vurugu hali ambayo hata hivyo ilitulizwa.

Msando alisema pia watuhumiwa hao watano wanaendelea kuhojiwa na polisi ili kuona kama kuna lolote linaloweza kubainika kuhusu mauaji hayo.

Baba mkwe wa marehemu, Dingo Shauri amesema hata wao hawafahamu chanzo cha tukio hilo.

“Taratibu za mazishi bado tunasubiria askari waseme na tumepanga wakituruhusu tutamzika hapa hapa Kwamgwe hata kama hatujapata kichwa, mwili tunao tutazika tu tutafanyaje sasa,” ameeleza.

Mkazi wa eneo hilo Malick Mohamed aliomba serikali kuingilia kati na kushughulikia mauaji hayo kutokana na wakazi wa eneo hilo kuingiwa na hofu.

“Hali ya amani ni tete. Tumeishi na hawa wafugaji Wamang’ati kwa takribani miaka 10 sasa, pametokea matukio mbalimbali na inapotokea tukio lolote hata kama ni mtu kakwazwa shamba lake limelishiwa akamchapa viboko hawa wenzetu wana tabia ya kulipiza visasi,” amesema Mohamed.
Amesema kutokana na hali hiyo eneo hilo limekuwa na matukio ya mauaji zaidi ya moja.


Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger