Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Jenerali (Mstaafu) George Mwita Waitara ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja wa gofu ambao umebeba jina la SERENGETI NATIONAL PARK GOLF COURSE wa kipekee duniani katika eneo la Fort Ikoma Wilayani Serengeti Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi na uzinduzi wa kampuni ya uwekezaji ya TANAPA – Tanapa Investment Ltd, Waitara ambaye ni mtaalam na mbobevu katika mchezo huo alisema dhumuni kubwa la kuanzisha zao hili la utalii ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni tano na mapato ya dola za kimarekani kufikia bilioni sita ifikapo mwaka 2025.
“Ni Dhahiri kwamba kutokana na umaarufu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti tuna kila sababu ya kuamini kwamba zao hili jipya la utalii litakuwa kivutio kikubwa na chachu ya kuongeza mapato yatokanayo na utalii katika shirika letu na Taifa kwa ujumla”, alisema Waitara.
Akifafanua zaidi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo alisema kwamba sehemu ya kwanza ya mradi huo imekamailika ambapo mashimo mawili na sehemu ya mazoezi (range) yamekamilika na kwamba mtandao wa mashimo mengine 16 pia umekamilika.
Aidha, Waitara ametoa wito kwa wawekezaji na wafanyabiashara ya utalii kutambua uwepo wa zao hili, kulitangaza na hatimaye kuleta wachezaji wa golf ambao pia watatalii katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Akizungumza katika taarifa yake juu ya mradi huu, Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilma wa TANAPA amebainisha kuwa mradi huu unatekelezwa na kampuni ya Uwekezaji ya shirika TANAPA INVESTMENT LIMITED ambayo imeanzishwa kwa maelekezo ya Serikali ili kutekeleza shughuli mbalimbali za ujenzi ndani nan je ya Shirika.
“Kukamilika kwa mradi huu kunategemea kuwavutia wacheza golf zaidi ya 3,000 kwa mwaka kutoka ndani nan je na shirikila linatarajia kupata TZs bilioni 2 kwa mwaka.” Alisema Kamishna Mwakilema.
Akiwasilisha salamu za kihandisi, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa wahandisi (ERB), Mhandisi Wakili, Menye Manga aliahidi kufanya kazi kwa karibu na kampuni ya TANAPA Investment Ltd na kupongeza uanzishwaji wa kampuni hiyo ambayo ina wataalam wa kutosha na vifaa vya kutekeleza kazi mbalimbali za kihandisi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha gofu nchini, Gilman Kasiga aliishukuru TANAPA na hasa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kwa kuendeleza michezo nchini hususan mchezo huu wa gofu na kuahidi kuleta mashindano makubwa ya kimataifa katika kiwanja hicho kwani kinakidhi viwango vya kimataifa.
Ujenzi wa uwanja huu wa golf unatarajiwa kugharimu jumla ya shilling bilioni 7.5 mpaka kitakapokamilika.
0 comments:
Post a Comment