Baadhi washiriki Kampeni ya GGM Kili Challenge 2022 waliopanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kukusanya fedha za mapambano dhidi ya VVU. Mwaka huu jumla ya Sh bilioni 1.1 ilikusanywa na GGML kupitia wadau mbalimbali.
NA MWANDISHI WETU
WAKATI leo ikiwa ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), imesema itaendeleza mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi kutokana na msaada inaoupokea kutoka kwa wadau na kuiwezesha Kampeni ya Kili Challenge kupiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa na GGML miaka 20 iliyopita na inalenga kuongeza uelewa na fedha za kupambana na maambukizi ya VVU. Kili Challenge imekuwa mfuko wa kimataifa wenye kushirikisha wapanda mlima Kilimanjaro na waendesha baiskeli kutoka mabara yote na zaidi ya nchi 20.
Hayo yamebainishwa jana naMakamu wa Rais wa AngloGold Ashanti anayesimamia miradi endelevu, Ghana na Tanzania, Simon Shayo wakati akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa kuelekea kilele cha maadhimisho hayo ya siku ya Ukimwi duniani.
“Tunafurahia mafanikio haya kwa kutuwezesha kuufanya mfuko huu kuwa endelevu katika kutimiza malengo ya Serikali dhidi ya janga hili,” amesema.
Alisema mwaka huu GGML kwa kushirikiana na Tume ya kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) kupitia kampeni hiyo ya Kili Challenge ilifanikiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 1.1 fedha zinazotumika katika kutunisha mfuko wa mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI.
Alisema fedha ambazo zimepatikana hadi sasa zimewezesha taasisi na makundi mbalimbali nchini kuboresha shughuli za mapambano dhidi ya UKIMWI.
Alisema kampeni ya GGM Kili Challenge 2022 iliyoanza Juni 29 na kumalizika Julai 21 mwaka huu, inaunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kufikia malengo ya sifuri tatu.
Sifuri ya kwanza inalenga katika kupunguza asilimia ya maambukizi mapya, sifuri ya pili katika kupunguza unyanyapaa na sifuri ya mwisho ni kupunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na VVU.
“Mathalani katika kampeni ya mwaka huu jumla ya washiriki 52 ambao 24 kati yao walipanda Mlima Kilimanjaro kwa miguu na 28 waliendesha baiskeli kuzunguka mlima huo kuanzia lango la Machame na kumalizia kwenye lango la Mweka,” alisema.
Alisema kwamba kampeni ya mwaka huu ilikuwa ya mafanikio makubwa.
Pia alieleza kuwa kampeni hiyo iliambatana na upimaji wa bure wa VVU na kisukari pamoja na chanjo ya UVIKO-19 kwa wakazi wa Moshi mjini na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
“Ninafuraha kubwa kuwataarifu kuwa katika huduma hizo zilizofanyika Julai 15 hadi 18 mwaka huu jumla ya watu 463 walipimwa VVU na hakuna hata mmoja aliyekutwa na maambukizi. Aidha watu 411 walijitokeza kupima VVU. Hii ni hatua kubwa katika mwitikio wa Watanzania wanaotaka kujua hali zao za kiafya,” alisema Shayo.
Aliongeza kuwa katika utoaji wa chanjo ya UVIKO-19, wataalam hao walifanikiwa kuwachanja watu 822, wakiwemo wanaume 365 na wanawake 427.
Zoezi la kuchangia damu lilikusanya jumla ya uniti 27 za damu, huku kondomu za kiume 9,335 na za kike 200 zikitolewa kwa wananchi waliohudhuria tukio hilo.
“Ili kutoa elimu ya kutosha kwa umma kuhusu VVU, vidonge vya PrEP pia vilisambazwa ili kupunguza makali ya kwa waathirika na kuzuia maambukizi kwa wale waliopima na kukutwa hawana ugonjwa huo, pamoja na vipeperushi 204 kuhusu masuala ya afya ya uzazi,” alisema Shayo.
Aidha, Mkurugenzi wa TACAIDS, Dk Leonard Maboko alisema jumla ya Sh1.1 bilioni zilipatikana wakati wa kampeni hiyo.
Pia alitoa wito kwa wadau wengine kukaa mezani na TACAIDS ili kwa pamoja kutafuta njia mpya za kutafuta fedha zaidi za kukuza mfuko wa VVU nchini.
Mmoja wa wapanda mlima, Lucina Livigha alisema licha ya changamoto za kupanda mlima huo, wanajivunia kuwa sehemu ya kampeni hiyo yenye mafanikio ambayo ni kuokoa maisha ya Watanzania.
0 comments:
Post a Comment