Monday 28 March 2022

TAASISI ZA KIFEDHA ZAOMBWA KUPUNGUZA RIBA ZA MIKOPO KWA WAJASIRIAMALI WADOGO

...
Na Ashura Jumapili, Bukoba.

Baadhi ya wajasiriamali Mkoani Kagera wameziomba taasisi za kifedha zinazotoa mikopo kwa Wafanyabiashara kupunguza riba za mikopo sanjari na kupunguza masharti kama ilivyofanya benki ya CRDB.

Wakiongea kwa nyakati tofauti katika siku ya ( Wellness Day )ya Wafanyakazi wa benki hiyo ya kukutana na kufanya vipimo vya Afya zao kwa magonjwa yasiyoambukiza wajasiriamali hao walisema wanatamani kukopa lakini masharti yanawashinda.

Martine Johansen mjasiriamali kata Kashai Manispaa ya Bukoba ,anajishughulisha na shughuli za kilimo alisema anatamani kuomba mikopo lakini anashindwa kutokana na masharti ya ukopeshaji na riba kuwa juu.

Johansen, alisema kuwa Hali ya Sasa biashara ni ngumu hivyo riba ikiwa juu wanaogopa kukopa.

"Afadhali benki ya CRDB kidogo riba yake ipo chini ukilinganisha na mabenki mengine", alisema.

Mstahiki meya wa Manispaa ya Bukoba Gypson Godson, ambaye alikuwa mgeni rasmi ameiomba benki ya CRDB kupunguza riba kwa Wajasiriamali wadogo kama walivyofanya kwa mikopo ya Kilimo na watumishi,ili na wao waweze kuchangamkia fursa ya mikopo ili waweze kukuza biashara zao na kupanua mitaji.


Godson,alitoa ombi hilo kwenye ( Wellness Day ) iliyoandaliwa na benki hiyo ya CRDB Kwaajili ya Wafanyakazi kushiriki pamoja kupima Afya zao hasa kwa magonjwa yasiyoambukiza na kushiriki michezo mbalimbali.

Alisema benki hiyo imefanya Jambo jema la kutoa mafunzo juu ya Afya kwa Wafanyakazi wake.

"Wakati naingia hapa nilienda kufanya vipimo nilikuwa najua niko salama lakini baada ya kupima urefu na uzito nimejikuta nipo sehemu mbaya kiafya hivyo nalazimika kufanya mazoezi na kupunguza baadhi ya vyakula",alisema Mstahiki Meya.

Alisema ili kufanya kazi kwa weledi ni lazima uwe na nguvu pamoja na Afya njema wakati wote.

Hata hivyo aliwaomba viongozi wa benki hiyo kushiriki katika miradi ya kimkakati ya ujenzi wa soko kuu la Bukoba na stendi kuu la mabasi ili kuiletea Manispaa hiyo maendeleo na Wafanyabiashara waweze kufanya shughuli zao katika mazingira Rafiki.

Pia aliomba kuwepo na michezo kati ya watumishi wa benki hiyo na madiwani wakishirikiana na watumishi wa Manispaa katika uwanja wa kaitaba sanjari na kupima Afya kwa magonjwa yasiyoambukiza.

Kaimu Meneja wa benki ya CRDB Kanda ya Ziwa Japhary Katura, alisema mikopo ya Kilimo imepunguzwa riba kutoka asilimia ( 20-9.9 )na kwa watumishi kutoka asilimia ( 17-13 ).

Alisema kwa Sasa benki ipo kwenye mchakato wa kupunguza riba kwa wajasiriamali wadogo na muda si mrefu watatoa taarifa .

Alisema benki ipo tayari kushirikiana na Manispaa ya Bukoba katika miradi ya kimkakati wanayoendelea kuitekeleza .

Alisema milango iko wazi kwa Manispaa ya Bukoba katika kutekeleza miradi mbalimbali.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger