Sunday, 8 August 2021

ZITTO KABWE : CHANJO YA CORONA NI SALAMA

...


Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe licha ya kuipongeza Serikali kwa hatua ya kuruhusu chanjo ya corona kuingizwa nchini, lakini amesema kunatakiwa kuwapo na mkakati maalumu wa kuhamasisha wananchi dhidi ya corona ambao utaongozwa na watu wanaoaminika kwenye jamii tofauti na ilivyo sasa.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Agosti 8, 2021 wakati akifungua kikao cha dharura cha kamati kuu ya chama hicho mjini Unguja chenye ajenda moja ya kujadili hali ya kisiasa nchini.

“Napongeza maamuzi sahihi ya Serikali ya kuruhusu chanjo ziingizwe nchini ili kuwapa kinga Watanzania na kuulinda mfumo wetu wa afya dhidi ya wagonjwa wengi ambao bila kinga hautaweza kuhimili. Hata hivyo, bado kuna kazi kubwa zaidi ya kufanya kwenye uhamasishaji wa watu kujitokeza kupata chanjo. Nitoe rai kwa kila mmoja wenu, nikianza na wanachama wa ACT Wazalendo kufuata taratibu na kupata chanjo mapema iwezekanavyo”


“Napenda kuwahakikishia kuwa nimejiridhisha chanjo zilizoruhusiwa kuingia nchini ni salama na mimi pia nimekwisha chanjwa na niko salama salimini. Nipende kuwaasa kuwa kuchanjwa ni suala la hiari lakini tunapoangalia usalama wa wapendwa wetu, jamii yetu na watanzania wenzetu basi hatuna budi kuhakikisha tunafanya maamuzi sahihi”

“Niweke bayana kuwa ni lazima kuwepo na mkakati maalum wa uhamasishaji dhidi ya Korona ambao utaongozwa na watu wanaoaminika kwenye jamii, na sio watu wale wale ambao walituambia kuwa Tanzania imeishinda Korona, ama watu wale wale ambao walituaminisha kunywa malimau na tangawizi ni kutibu Corona.”

“Hatuwezi kuwa na utekelezaji bora wa sera mpya za kupambana na Korona iwapo tutaendelea kuwa na sura zile zile zilizotuaminisha kutumia njia zisizoshauriwa Kisayansi”

“Vile vile niendelee kusisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote ikiwemo kuepuka mikusanyiko, kuvaa barakoa na kunawa kwa maji tiririka na sabuni kila wakati pamoja na kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na maambukizi na pia kuzuia kusambaa kwa maambukizi”

“Kwa upande wa Serikali zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar, hatua madhubuti zichukuliwe kuongeza elimu kwa wananchi kwani kwa mwaka mzima walikuwa wanaambiwa hakuna Korona, hivyo kuwaambia kuwa sasa ipo sio jambo rahisi kueleweka. Jitihada zifanyike kwenye kutoa elimu sahihi kwa Umma” amesema Zitto Kabwe
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger