Polisi huko kaunti ya Meru wamemkamata mwanaume anayetuhumiwa kumnyonga mwanawe wa miaka saba kwa madai ya kuharibu simu ya rununu 'Smartphone' huku jamaa akikanusha madai kwamba alimuua mvulana huyo akisema kwamba alikuwa anamtia tu adabu.
Mwanamume huyo, kulingana na ripoti ya polisi, alimkaba koo mwanawe ndani ya nyumba yao huku akimtandika huku majirani wakifika katika boma hilo kumwokoa mtoto huyo.
Mwanamume huyo, aliyetambulika kama Evans Mutwiri, aliripotiwa kuwafukuza majirani hao akiwakaripia kwa kuingilia mambo ya boma lake.
Hata hivyo majirani hao walikataa kuondoka hadi pale ambapo polisi walifika na walipowasili walimkuta mvulana huyo akiwa amepoteza fahamu.
“Polisi walipofika alijaribu kuwazuia kuingia ndani ya boma. Alijibu kwa jeuri na kuwaambia kwamba mvulana huyo alikuwa amelala. Polisi walilazimika kuingia ndani ya nyumba hiyo kwa nguvu na kumkuta kijana huyo akiwa amezirai, ” jirani, Florence Mwende, alisema.
Kamanda wa kituo cha polisi cha Laare Ezra Zambu, alithibitisha kukamatwa kwa mshukiwa huyo. Zambu alisema mvulana huyo alipoteza maisha yake akipelekwa katika hospitali ya Meru Level V kwani vituo vya afya vya eneo hilo havikuwa na uwezo wa kutibu kiwango cha majeraha aliyopata.
Mshukiwa hata hivyo alikanusha madai kwamba alimuua mvulana huyo akisema kwamba alikuwa anamtia tu adabu.
Mamaake mtoto huyo alisema kuwa alisikia kutoka kwa watu waliokuwa katika kituo hicho cha polisi ambapo anafanya kazi kwamba kuliletwa mshukiwa aliyekuwa amemuua mtoto.
Alipofuatilia ndiposa akabaini kuwa mshukiwa alikuwa ni mumewe.
"Nilisikia kwamba kuna mtu amemuua mtoto. Na kwa sababu ninafanya kazi katika kituo hicho cha polisi kuwapa washukiwa chakula niliulizia na ndiposa nikabaini mtuhumiwa alikuwa mume wangu," alidokeza.
Zambu aliwaonya wazazi dhidi ya kutumia nguvu kupita kiasi wakati wanapowaadhibu watoto akiongeza kwamba yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kuwadhulumu watoto ataadhibiwa vikali kisheria. Alifichua kwamba mwili wa mtoto huyo utafanyiwa upasuaji kubaini kilichomuua.
Chanzo - Tuko News
0 comments:
Post a Comment