Jeneza lililobeba Mwili wa aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Nkulila
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi ambaye alikuwa rafiki kipenzi wa marehemu David Nkulila akitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Nkulila.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi ambaye ni Diwani Mstaafu wa kata ya Ngokolo katika Manispaa ya Shinyanga na rafiki kipenzi wa Hayati David Mathew Nkulila ameomba barabara ya lami kuanzia Kalogo mpaka Shule ya Msingi Bugoi ipewe jina la 'Nkulila' ili kumuenzi David Nkulila.
Ntobi ametoa ombi hilo Agosti 25,2021 wakati wa Misa ya kuombea mwili wa marehemu David Nkulila iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma Ngokolo Mjini Shinyanga.
Mazishi ya mwili wa marehemu David Nkulila ambaye pia alikuwa Diwani wa kata ya Ndembezi yamefanyika katika makaburi ya Mageuzi Ndembezi Mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na maelfu ya waombolezaji kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga.
Ili kumuenzi David Nkulila , Ntobi aliomba barabara ya kuanzia Shule ya Msingi Bugoi hadi Kalogo ipewe jina la Nkulila
"Kutokana na namna Nkulila alipigania ujenzi wa barabara ya lami ya kuanzia Shule ya Msingi Bugoi hadi Kalogo wakati nami nilipigania ujenzi wa barabara ya Ngokolo. Natoa rai barabara ya Shule ya Msingi Bugoi hadi Kalogo ipewe jina la Nkulila ili kumuenzi", alisema Ntobi huku waombolezaji wakipiga makofi wakati wa misa ya kuombea mwili wa marehemu David Nkulila.
"Kama ikiwezekana pia WDC ya kata ya Ndembezi na Manispaa ya Shinyanga pia mkae muangalie namna ya kumuenzi Nkulila. Naomba mtaa mmoja kwenye kata ya Ndembezi upewe jina la Nkulila kutokana na kuwa ndiye Diwani wa kwanza Ndembezi (Kata ya Ndembezi imeundwa kutoka kata ya Ngokolo) na wa aina yake katika Manispaa ya Shinyanga",aliongeza Ntobi huku akiendelea kupigiwa makofi na waombolezaji ikiwa ni ishara ya kuonesha kuunga mkono hoja ya Ntobi.
"Mimi ni rafiki wa karibu sana wa David Nkulila. Mimi ni Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga lakini nilikuwa ndiyo rafiki yake yeye akiwa ni wa CCM. Urafiki wangu na Nkulila mimi nikiwa diwani wa Kata ya Ngokolo yeye akiwa diwani wa Ndembezi ulitufanya tuonekane kama mapacha kutokana na maono makubwa tuliyokuwa nayo kuhusu maendeleo ya Manispaa ya Shinyanga. Kutokana na urafiki wetu huu ulisababishia misukosuko mingi hadi ikafikia hatua akataka kujiuzulu Udiwani",alisema Ntobi.
Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Nkulila (57) alifariki dunia Agosti 23,2021 kutokana na ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Nkulila amekuwa Diwani wa kata ya Ndembezi tangu mwaka 2010 anafariki dunia Agosti 23,2021 na Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mwaka 2010-2015.
Pia amekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabambasi tangu mwaka 2004 hadi mwaka 2019.
Nkulila alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Novemba 24 Mwaka 2020 na ametumikia nafasi ya Meya kwa kipindi cha miezi 10 hadi umauti ulipomkuta.
David Mathew Nkulila alikuwa na maono ya kuifanya Manispaa ya Shinyanga kuwa Jiji na tayari alikuwa ameanzisha usafiri wa daladal za Hiace kwa njia za Mjini Shinyanga hadi Old Shinyanga, Mjini hadi Kolandoto na Mjini hadi Ishinabulandi.
Nkulila atakumbukwa kwa misimamo yake thabiti katika kutetea wanyonge, asiyekubali kuyumbishwa na kupiga vita rushwa na ufisadi.
Nkulila ameacha mjane watoto watano kati yao watoto watatu ni wa kulea aliachiwa na marehemu ndugu zake.
0 comments:
Post a Comment