Na. Saidina Msangi na Sandra Charles, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, wamekubaliana kutatua changamoto za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kufanya kazi kwa kushirikiana ili kukuza uchumi wa Taifa.
Mawaziri hao wamekutana jijini Dodoma katika kikao kazi kilicholenga kuangalia masuala yaliyokuwa na changamoto wakati wa bunge la bajeti na Sheria ya Bajeti pamoja na masuala yanayohusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Dkt. Nchemba alisema kuwa kikao hicho kimekuwa cha mafanikio ambapo mengi yamefikia hatua nzuri na kuongeza wigo wa ushirikishwaji hasa katika kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mipya ya kipaumbele iliyoko katika Bajeti Kuu ya Serikali.
“Katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo tunaangalia uwezeshaji na utekelezaji wa miradi inayoendelea na miradi mipya, na mengi tuliyojadili tumefikia hatua nzuri,” alisema Dkt. Nchemba.
Waziri Nchemba aliwaagiza wataalamu wa pande zote kuendelea kufanyia kazi maeneo ya changamoto yaliyosalia ikiwemo uboreshaji wa Sheria ya Usajili wa Vyombo vya Moto.
“Niwasihi msiishie kwenye Sheria ya Vyombo vya Moto ila muangalie na waendeshaji wa vyombo vya moto haipendezi mtu kuwa na leseni mbili wakati nchi ni moja”, alisisitiza Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, alisema kuwa kikao kati yake na mwenzake Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kimetoa njia ya namna ya kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo hususani za miradi.
Alisema kuwa wamejadili namna ya kufanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati iliyopo upande wa Zanzibar, jambo ambalo lina tija kwa wananchi wa Zanzibar.
“Hili ni jambo muhimu tunashukuru uwepo wa kikao hiki ambacho kinatoa mwanga wa namna miradi ya kimkakati Zanzibar itatekelezwa na uwezeshaji wake,” alisema Mhe. Jamal Kassim Ali.
Aidha ameushukuru uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango upande wa bara kwa kikao hicho na kueleza kuwa kikao hicho ni vema kikawepo angalau kila baada ya miezi miwili ili kuona mambo mapya yatakayoibuka yanatatuliwa na kufanya ufuatiliaji wa makubaliano yaliyopita jambo ambalo lililidhiwa na pande zote.
0 comments:
Post a Comment