Waziri wa Nishati, Medard Kalemani ametoa onyo kwa mameneja na wakandarasi wanaotoza nguzo za umeme wananchi na kuwataka waachane na tabia hiyo mara moja kwakua serikali imegharimia nguzo hizo kwa asilimia 100.
Waziri Kalemani ametoa kauli hiyo bungeni leo Jumatano Novemba 6, katika kipindi cha maswali na majibu alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Halima Bulembo aliyetaka kujua serikali inazungumzia vipi kadhia ya kulipishwa nguzo za umeme ambayo wananchi wa Mkoa wa Kagera wamekuwa wakikumbana nayo
Akijibu hoja hiyo Waziri Kalemani amesema serikali haitaendeleakufumbia macho suala hilo na kwamba yeyote atakaekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria bila kujali cheo chake.
“Yapo maeneo bado wakandarasi na mameneja wa Tanesco wanaendelea kutoza nguzo wateja, ninaomba nitoe tamko kali sana kwamba ni marufuku kutoza nguzo kwa wateja wote, awe mkandarasi, Meneja wa Tanesco au kibarua na hii ni kwasababu serikali imegharamia kwa asilimia 100,” amesema Dk. Kalemani.
Aidha amesema serikali imekuwa ikipeleka umeme katika maeneo yote hasa vijijini lakini baadhi ya taasisi zimekuwa hazilipiwi na hivyo amewataka wamiliki wa taasisi hizo kuhakikisha wanalipa kiasi cha Sh 27,000 ili taasisi zote zipelekewe umeme.
0 comments:
Post a Comment