Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kuelekea msimu ujao wa pamba serikali itajitahidi kupunguza gharama na kwamba haitaingilia kupanga bei bali watatafuta njia nyingine za kumlinda mkulima na kuhakikisha hapati hasara.
Ametoa kauli hiyo bungeni leo Jumatano Novemba 6, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Busega (CCM), Dk. Raphael Chegeni aliyetaka kupata tamko la serikali kuhusu wakulima wa pamba ambao waliuza pamba tangu Mei mwaka huu lakini hawajalipwa fedha zao.
“Wakulima wa pamba ambao mwaka hadi mwaka wamekuwa wakifanya kazi ya kulima wamekuwa wakipata hasara kwa mfano leo hii wakulima wa Mkoa wa Simiyu hasa wa Wilaya ya Busega wameuza pamba tangu mwezi Mei mpaka leo hawajaliwa fedha zao sasa hauoni kwamba hii ni kuwakatisha tamaa wakulima wasiweze kufanya kilimo kizuri zaidi na nini tamkola serikali juu ya hili,” amehoji.
“Ninakiri kuwa baadhi ya wakulima wa pamba hawajalipwa fedha zao, kwa mwaka huu mpaka sasa hivi jumla ya bilioni 417 zimeshalipwa kwa wakulima wa nchi nzima, ambao hawajalipwa wanadai bilioni 50 kufikia sasa hivi na sababu ya msingi ni lazima tufahamu kwamba asilimia zaidi ya 80 ya pamba inakwenda nje ya nchi, wanunuzi wetu wanakabiliwa na mtikisiko wa bei ambao umewakabili katika soko la dunia na sisi kama nchi tulitoa maelekezo ya bei ya kununulia na haya yalikuwa maamuzi ya serikali kwaajili ya kumlinda mkulima asipate hasara.
“Pamba yote iliyokuwa kwa wakulima imeshakusanywa sasa hivi kilichobaki mikononi mwa wakulima ni tani 5,000 tu ambayo tunaamini msimu unapoanza pamba yote ya wakulima itakuwa imeondoka, tunajitahidi kupunguza gharama msimu huu unaokuja na hatutaingilia kupanga bei, jukumu letu litakuwa ni kuhakikisha mkulima hapati hasara kwa kutafuta njia nyingine za kumlinda kuliko kumuathiri mnunuzi,” amesema Bashe.
0 comments:
Post a Comment