Friday 1 November 2019

Ahukumiwa Kifungo Cha Maisha Jela Kwa Kumbaka na Kumpa Mimba Mtoto wake wa Kumzaa

...
Mahakama ya  Wilaya ya  Mpanda  Mkoani  Katavi  imemuhukumu  Lazaro  Charles (35)  Mkazi    wa Mtaa wa  Mji   Mwema katika  Manispaa ya   Mpanda Mkoa wa  Katavi kutumikia jela kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kumpa mimba mtoto wake wa kumzaa  mwenye (14) ambaye ni, mwanafunzi wa  darasa la  saba shule ya msingi  Majengo Manispaa ya  Mpanda.

Hukumu  hiyo iliyovuta hisia za wakazi  wengi  wa  Manispaa ya Mpanda, ilitolewa na Hakimu Mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Gosper Luoga baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa Mahakamani na upande wa mashtaka.

Awali katika kesi hiyo Mwanasheria wa Serikali Gregory  Muhangwa aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti hapo Januari 1 mwaka 2017 na April 29, 2019.

Mshtakiwa huyo alikuwa akitenda kosa hilo huko nyumbani kwake wakati mke wake ambaye ni mama  mzazi wa mtoto huyo alipokuwa amesafiri ndipo alipokuwa akiingia kwenye chumba alichokuwa akilala mtoto wake huyo na kumbaka kwa nguvu.

Mwendesha mashtaka huyo alieleza kuwa baada ya kuwa anambaka  alikuwa akimwekea majani kwenye sehemu zake za siri kama dawa ya kienyeji  ya  kumwondolea maumivu.

Hakimu Luoga amemtaka mshtakiwa kama atakuwa na sababu yoyote ile ya msingi ambayo inaweza kuifanya mahakama iweze kushawishika ili kumpunguzia adhabu basi inatoa nafasi kujijitetea.

Lazaro Charles ameiomba mahakama  impatie nakala ya hukumu ya mwenendo wa kesi hiyo tu kwani hana utetezi wowote ule.

Baada ya ombi hilo la mshtakiwa mwanasheria wa Serikali Gregory Muhangwa aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia kama hiyo.

Hakimu Luoga baada ya kusikiliza pande hizo mbili alisoma hukumu na kuiambia Mahakama kuwa mshtakiwa amepatikana na kosa la kifungu cha sheria Namba 158 (1) (a ) SURA YA 16 ya marejeo 2002, hivyo Mahakama inamuhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela kuanzia leo Novemba 1, 2019.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger