MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ya kufutiwa mashitaka ya
uchochezi yanayomkabili na wenzake watatu.
Hakimu
Mkazi Mkuu, Emillius Mchauru alitoa uamuzi huo jana baada ya kukubali
pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri waliodai mashitaka hayo
yasifutwe kwa kuwa hati ya mashitaka haina makosa.
Mbali
ya Lissu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni mwandishi wa gazeti
la Mawio, Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na
Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob. Hata hivyo, uamuzi huo
ulitolewa jana bila Lissu kufika mahakamani hapo kwa kuwa anaumwa.
Akiieleza
mahakama, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai Lissu ameshindwa
kufika mahakamani kwa kuwa anaumwa, lakini wadhamini wake akiwemo
Ibrahim Ahmed wamefika mahakamani na kueleza kuwa Lissu anaumwa malaria.
Aidha, ilielezwa kuwa mshtakiwa Idrissa anaumwa na yupo Zanzibar kwa
ajili ya matibabu.
Katika
maombi yao, washitakiwa kupitia kwa Wakili Kibatala waliiomba mahakama
ifute mashitaka hayo kwa kuwa hati ya mashitaka imekosewa kwa
kutokueleza makosa hayo wametenda wapi na pia mahakama hiyo haina
mamlaka ya kusikiliza masuala yanayohusu Zanzibar.
Akisoma
uamuzi, Hakimu Simba alisema baada ya mahakama kupitia hoja za pande
zote mbili katika kesi hiyo imejiridhisha kuwa hati ya mashitaka haina
makosa.
Aidha,
alisema mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa
makosa yaliyofanyika yanahusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivi
karibuni, mahakama ilifuta mashitaka mawili ya uchochezi kati ya matano
yanayowakabili washitakiwa hao, baada ya upande wa jamhuri kuyaondoa
katika hati kwa kuwa hayana kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Katika
mashitaka yao inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016, Dar es Salaam
washitakiwa walichapisha taarifa ya uchochezi yenye kichwa cha habari ‘
Machafuko yaja Zanzibar’.
Pia
inadaiwa Januari 14, 2016 Dar es Salaam walichapisha habari hizo ili
kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar. Inaendelea kudaiwa siku hiyo
hiyo, Lissu na wenzake bila ya kuwa na mamlaka yoyote yale waliwatisha
na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ili wasikubali kuingia kwenye
marudio ya Uchaguzi Mkuu.
0 comments:
Post a Comment