CHAMA
cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka viongozi na watendaji wa
chama hicho kuhakikisha mikataba ya kibiashara wanayofunga inapitiwa na
kuwashirikisha wanasheria ili kuepuka vitendo vya utapeli.
Kimesema
kuwashirikisha wanasheria wakati wa kufunga mikataba ya aina mbali
mbali ya kukodisha Mali za Chama hicho kutasaidia kumaliza kero na
migogoro ya matumizi mabaya ya Rasilimali za CCM.
Hayo
aliyasema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai katika
mwendelezo wa ziara ya kukagua na kuhakiki mali za Chama hicho huko
Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema
matatizo ya matumizi mabaya ya Mali za chama hicho yanayojitokeza
katika maeneo nchini ni kutokana na baadhi ya viongozi na watendaji
kufunga mikataba ama makubaliano na wafanyabiashara bila ya
kuwashirikisha wanasheria ama kupata ushauri kutoka kwa viongozi wa
ngazi za juu hali inayopelekea baadhi ya watu kutumia nafasi hiyo
kujinufaisha wenyewe badala ya kuangalia maslahi ya CCM.
Vuai
alieleza kwamba njia pekee ya kuziweka salama mali mbali mbali za chama
hicho ni uwepo wa maridhiano na makubaliano yanayojali na kuzingatia
matakwa ya kisheria.
“
Naendelea kusisitiza kwamba mali za CCM hazipo kwa ajili ya
kuwanufaisha watu wachache, bali zipo kwa ajili ya kukinufaisha chama
ambacho ni taasisi halali ya watu wengi na jambo lolote la umiliki wa
Rasilimali zake lazima liendeshwe kwa misingi ya uwazi na usawa kupitia
utaratibu halali wa kisheria.
Pia
Mali zote kwa sasa ni lazima zitumike ipasavyo kwa mujibu wa matakwa ya
sera ya CCM ya siasa kwenda sambamba na ukuaji wa uchumi ndani ya chama
chetu.”, alisisitiza Vuai na kuongeza kuwa CCM kwa sasa inaendelea na
mipango ya kuhakikisha Rasilimali zake zinatumika vizuri kuimarisha
uchumi wa Chama hicho badala ya watu wachache wanaojimilikisha mali hizo
kinyume na taratibu.
Alisema
lengo la ziara hiyo ni kuhakiki mali za Chama hicho pamoja na
kuwakumbusha Viongozi na Watendaji wa Chama na Jumuiya kwamba chombo
pekee kinachomiliki mali zote ni Baraza la Wadhamini la Chama hicho
hivyo hakuna chombo kingine tofauti na baraza hilo kinachoweza kutoa
maamuzi ya kuuza mali za Chama.
Aliwaagiza
Viongozi wa Mkoa huo kupitia upya mikataba yote waliyofunga na
wafanyabiashara katika eneo linalomilikiwa na CCM ili kuhakikisha
maslahi yanayopatikana yanaendana na mahitaji ya wakati uliopo sasa
kibiashara.
Aliwasihi
Wana CCM kuendelea na utamaduni wa kuwashirikisha viongozi wa ngazi
mbali mbali za chama hicho pindi panapotokea kasoro za kiutendaji ili
ziweze kutatuliwa kwa kufuata utaratibu wa kinanuni na kimaadili kwa
lengo la kuepuka kauli na malalamiko yasiyofaa ndani ya Chama hicho.
Naibu
Katibu Mkuu huyo alisema kazi iliyopo sasa mbele ya CCM ni kuendelea
kujiimarisha kisiasa huku ikitekeleza ilani ya Uchaguzi ya Mwaka
2015/2020 kwa kasi na kwa ufanisi zaidi ili wananchi waendelee kuiunga
mkono na hatimaye Chama hicho kiweze kuandika historia mpya ya ushindi
wa mwaka 2020.
Alisema
maeneo ya CCM yaliyopo Nungwi ni Rasilimali kubwa kwani yapo katika
ukanda wa Utalii hivyo yanatakiwa kulindwa na kuangaliwa vizuri na
wahusika yasije yakaangukiwa mikononi kwa watu ambalo ni matapeli na
wapinga maendeleo na wakatumia fursa hiyo kupandikiza migogoro na
mipasuko isiyokuwa ya lazima ndani ya Chama.
Pamoja
na hayo alisema endapo uongozi wa Mkoa huo utahitaji msaada wa kisheria
Afisi kuu ipo tayari kuwaunga mkono kwa kuwapa mwanasheria wake ili
aweze kuwashauri na kuwaelekeza njia bora ya kufunga mikataba rasmi
inayotambulikana kisheria.
Nao
Viongozi wa Mkoa huo wameahidi kuzifanyia kazi kwa haraka changamoto
zilizojitokeza katika maeneo yanayomilikiwa na chama hicho ili kwenda
sambamba na matakwa ya sera ya ukuaji wa uchumi ya CCM.
Walisema
licha ya CCM ndani ya mkoa huo kuendelea na harakati za kuimarisha
shughuli za kisiasa, bado wana fursa ya kuhakikisha rasilimali za chama
hicho hasa zilizopo katika maeneo ya uwekezaji katika sekta ya utalii
zinakinufaisha chama badala ya watu wachache wanaojali maslahi binafsi.
0 comments:
Post a Comment