Sunday, 6 September 2015

Magufuli: Nikiwa Rais Nitachukua Mashamba Yasiyotumika

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameahidi kunyang’any’a mashamba ambayo yamehodhiwa na watu bila kutumiwa kwa ufugaji wala kilimo, na kuyagawa kwa wakulima na wafugaji wasio na maeneo ya kilimo. 
 
Alisema hayo alipozungumza na wananchi wa wilaya za Ulanga na Kilombero mkoani Morogoro jana.

Dk Magufuli alisema akiwa rais, kuna mambo mengi anaweza kufanya, kukabiliana na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na mojawapo ni kutoa ardhi zaidi kwaajili ya wakulima na wafugaji, ili kuondoa uhaba wa ardhi, unaosababisha ugomvi wa maeneo ya kulishia mifugo na kulima.

Alisema kuna watu wanamiliki maelfu ya eka za ardhi bila kulima na kwamba atanyang’any’a mashamba hayo ambayo yamehodhiwa na watu hao bila kutumiwa kwa ufugaji wala kilimo. 
 
Akihutubia maelfu ya wananchi, pia Dk Magufuli alisema kuwa anajivunia uzoefu wa marais wastaafu wa Awamu ya Pili mpaka Awamu ya Nne na wa Zanzibar, kwamba ndio atakaowafuata kwa ushauri akikwama popote.

Alisema hiyo ni moja ya tofauti kubwa kati yake na wagombea wengine wa urais. 
 
“Nitaingia Ikulu nikiwa na washauri wazuri, nikikwama mahali nitakwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, nikikwama nitaenda kwa mzee Benjamin Mkapa, nikikwama tena nakwenda kwa mzee Ali Hasan Mwinyi.

“Wako wengi, upo ushauri nitauchukua kutoka kwa mzee Salmin Amour (Rais Mstaafu wa Zanzibar), Dk Ali Mohamed Shein na kwa Amani Abeid Karume,” alisema. 
 
Kutokana na fursa hiyo ya kiuongozi aliyonayo ndani ya Chama Cha Mapinduzi, Dk Magufuli aliomba Watanzania wote bila kujali vyama vya siasa, makabila wala dini kumpa kura kwa wingi kwa kuwa atakuwa na washauri wazuri wenye uzoefu.

Alisema wagombea wengine, akiwemo wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa, hawataweza kupata ushauri wa washauri hao kama ilivyo rahisi kwake.

Kutokana na uhakika huo wa washauri wazoefu, Dk Magufuli alisema ndio maana baadhi ya wagombea hao wanaweza kuja na ahadi za uongo, ikiwemo ya kuondoa nyumba za tembe na za nyasi.

Aliwataka wananchi kuwapima wagombea hao katika ahadi zao, kwa kuwa baadhi walikuwepo ndani ya Serikali kwa muda mrefu, lakini walishindwa kuondoa nyumba hizo katika majimbo walikotokea.

Dk Magufuli alisema yeye hataahidi kuondoa nyumba hizo, bali anaahidi kushusha bei ya vifaa vya ujenzi hasa saruji, mabati na misumari, ili wananchi wanaofanya kazi wajenge nyumba bora.

Katika kuongeza idadi ya Watanzania wanaofanya kazi ili kufikia lengo hilo, Dk Magufuli alisema katika kila mtaa na kijiji, serikali yake itatoa Sh milioni 50 kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara ndogo za wanawake na vijana.

Alisema atataka kila anayefanya kazi apate kipato kizuri kitakachomsaidia kukabiliana na mahitaji ya maisha yake, ikiwemo kujenga nyumba bora kutokana na kushushwa kwa bei za bidhaa za ujenzi. 
 
Kwa wakulima, alisema atahakikisha pembejeo sahihi zinatolewa kwa wakati na mazao yatakayovunwa, itakuwa marufuku kwa Serikali kukopa mazao yao.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger