Sunday, 6 September 2015

Dr. Slaa Aishambulia CHADEMA Kwa Mara ya Pili.......Asisitiza Kuwa Lowassa ni Fisadi

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Wilbrod Slaa amejitokeza hadharani kwa mara nyingine na kujibu watu waliojitokeza kuponda hotuba yake, aliyoitoa hivi karibuni kuwa hawana hoja zaidi ya kumtukana.

Akizungumza kupitia kituo kimoja cha Televisheni jijini Dar es Salaam, Dk Slaa alisema madai yote, yaliyotolewa juu yake na baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa Chadema na vyama vinavyounda Ukawa, baada ya hotuba aliyoitoa, hayana msingi wowote na kwamba ni kuishiwa hoja, ndio maana walimtukana badala ya kujibu hoja.

“Nashukuru hoja zangu zote hawajazijibu, sasa wanapiga tu propaganda, hata Rostam Aziz alijaribu kujibu, lakini akatukana tu kama alivyonitukana mwaka 2007 badala ya kujibu hoja na mimi nasema ufisadi ni hoja,” alisema Slaa.

Aidha, Dk Slaa alisema hawezi kumpeleka mahakamani Rostam ambaye ni kada wa CCM, ambaye amemtaka Dk Slaa ampeleke mahakamani kama anao ushahidi kuwa anaunga mkono mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.

Slaa amesema yuko tayari kutoa ushahidi wake pale Jamhuri itakapomfungulia mashitaka. “Wale ambao hawaelewi taratibu za kesi, kuna kesi za madai ambapo mtu binafsi anafungua kesi na kesi za jinai ambazo mtu binafsi hawezi kufungua ila Jamhuri, kesi za Jamhuri mtu huwezi kufungua, wewe ni shahidi… mimi nikiitwa nitakwenda kutoa ushahidi dhidi ya Rostam Aziz,” alisema Dk Slaa.

Aidha, alisema ni kweli vijana wanataka mabadiliko na ni hoja ya msingi na pia wakulima ambao hawafaidiki na kilimo chao, wanataka mabadiliko, vivyo hivyo kwa makundi mengine.
 
 “Nimesema mimi Lowassa hafai, leo, lini ameanza kuwa rafiki wa masikini?

"Lini ameanza kuwa safi?Watanzania waache ushabiki usiofaa wapime kwa vigezo, ushabiki usio na tija utatuangamiza,” alisema Dk Slaa, akijibu hoja mbalimbali ambazo zimejitokeza baada ya hotuba yake hiyo, aliyoitoa mwanzoni mwa wiki hii baada ya kutangaza kuachana na mambo ya siasa na kubaki mshauri wa wananchi.

Akijibu shutuma dhidi yake baada ya kutuhumiwa kutoa habari za upotoshaji juu ya maaskofu, Slaa alisema alichokieleza siku ile anatangaza kujiengua kwenye siasa ni alichoambiwa na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwamba maaskofu 30 kati ya 34 walihongwa.

“Tatizo halikuwa fedha bali askofu anaona sifa mimi kumuunga mkono mtu ambaye alitumia fedha kununua maaskofu, na Watanzania nawaomba mtulie msikurupuke na maneno bila kuyachambua, taifa linaangamia kwa sababu ya ushabiki usio na tija, nimeshtushwa na kauli yake, kiongozi anayepaswa kukemea rushwa, maovu… baba askofu piga magoti Mungu wako atazame dhamira yako,” alisema.

Dk Slaa alisema yeye ana uwezo wa kupambanua siasa na mambo mengine na kwamba ni kweli alikutana na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe katika Hoteli ya Serena na hiyo ni katika kupata taarifa alizozihitaji kwa ajili ya kazi yake ya utafiti na kwamba Mwakyembe ni chanzo cha taarifa cha kwanza na kwamba hakufanya kwa siri.

Akizungumzia picha yake ambayo ilizunguka kwenye mitandao ya kijamii, ikimuonesha yeye akiwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema picha hiyo ni wakati wa mkutano wa vyama vya siasa na Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck alipokuja kwenye ziara ya kikazi Februari mwaka huu.

“Kwenye picha hizo ambazo zinatuonesha mimi, Mwigulu na Profesa Lipumba tukimpokea Rais wa Ujerumani alipotembelea Tanzania, leo ndio zinaletwa kuonesha eti haya ndiyo mazungumzo ya kumng’oa Slaa, naomba niwaambie warudi nyuma waangalie hizo picha ni za lini hazina uhusiano na mimi kujiondoa,” alisema Dk Slaa.

Aidha, Dk Slaa alisema kuwa kuna propaganda nyingine ambayo imetumika ambapo watu wametuma pia picha ambazo zinamuonesha akiwa kwenye ndege, ikisemekana kwamba ametoroka nchini baada ya hotuba, sio kweli.

Alikiri kusafiri lakini sio kwa kutoroka, kama ambavyo imedaiwa na baadhi ya watu na kwamba amekuwa akipiga picha na watu kwenye ndege na kwamba picha hiyo ni ya safari ambayo alishasafiri na kurudi.

“Magazeti na mitandao wanasema Dk Slaa hayuko nchini, lakini nadhani sasa Watanzania wanaona sasa niko hapa studio Dar es Salaam na siko Marekani,” alisema Dk Slaa na kuongeza kuwa uongo huo unaonesha ni aina gani za siasa zilizopo hapa nchini.

Alisema hoja ya wapi amepata fedha kwenda Serengeti na kuishi hotelini ni hafifu. “Nilikwenda Marekani na kukaa kwa zaidi ya miezi 12 na kutembelea majimbo 13 na sikulipiwa na mtu yoyote zaidi ya chama changu kulipia shilingi 500,000 kwa mshauri aliyeandaa nyaraka ya kunisaidia katika ziara hiyo, mbona hawakuniuliza nimepata wapi fedha hizo?”
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger