Tuesday 22 April 2014

MEYA SILAA: DAR ITAKUFA

...

MEYA wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa amesema ikiwa Halmashauri ya Jiji haitapewa fedha za kutosha na serikali kuu basi Dar itakufa.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa akifafanua jambo ndani ya chumba cha habari cha Global Publishers, Mwenge, Bamaga jijini Dar.
Akizungumza na waandishi wa habari katika safu ya Live Chumba cha Habari na Global TV On Line, Bamaga Mwenge, Mstahiki Meya Slaa alisema hivi sasa Jiji la Dar linahitaji shilingi bilioni 15 ili kurekebisha miundombinu mbalimbali, fedha ambazo ni ngumu kuzipata.
“Tumewaambia viongozi serikalini kuwa licha ya kutolewa shilingi bilioni 21 lakini hazitoshi na wasipoangalia ndani ya miaka mitano ijayo Dar itakufa. Mwaka 1984 Dar ilikuwa na watu laki tatu lakini leo tuna watu milioni nne na laki tatu, utaona ongezeko ni kubwa sana, na miundombinu na masoko ni yaleyale,” alisema.
Baadhi ya mazungumzo na waandishi wa habari yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwandishi: Barabara ya Uhuru ambayo hutumiwa sana na viongozi wa kimataifa wakati wanaingia nchini ipo katika hali mbaya sana, kwa kuwa ipo katika manispaa yako, je, mna mpango gani wa kuikarabati?
Slaa: Ni kweli barabara ile imekwisha muda wake na zinahitajika shilingi bilioni 15 kukarabati. Hivi sasa haipo chini ya manispaa yetu imechukuliwa na Tanroads (Wakala wa barabara nchini). Sisi Manispaa ya Ilala hatuna uwezo wa kuijenga. Kwa maoni yangu road tall (ushuru wa barabara) ingefaa ugawanywe ili halmashauri za miji nazo zipate fedha hizo kukarabati barabara zao.
Mwandishi: Tugeukie suala la waishio mabondeni, kwa nini hawa hawadhibitiwi na badala yake mnangoja majanga yatokee ndipo mnahangaika kutoa huduma kwao?
Slaa: Kwa kweli tatizo kubwa ni kwamba hatuna askari wa kutosha kuwadhibiti. Katika manispaa yangu nina askari polisi arobaini na tatu tu. Hawatoshi. Hata hivyo, kwa wakazi wa Jangwani bado tuna kesi nao mahakamani, hivyo kuna zuio.
Lakini ukweli ni kwamba hata wao hupata hasara kubwa kwani kila msimu wanalazimika kununua fenicha mpya na madaftari ya watoto wao ambayo huharibiwa na mafuriko, wanaishi maisha aghali sana watu hawa.
Mwandishi: Lipo hili suala la Wamachinga kwa nini haupatikani ufumbuzi wa kudumu badala yake wanasukumana na serikali mara kwa mara?
Slaa: Ni kweli, Wamachinga kwangu mimi siyo tatizo. Kinachotakiwa ni kufanya utaratibu ili wafanye biashara zao kihalali. Kwa ushauri wangu ingefaa zile sehemu wanazofanyia biashara serikali ingenunua majengo mitaa hiyo na wakajengewa sehemu za biashara. Naamini tatizo hilo lingekwisha.
Mawazo ya baadhi ya viongozi ni kukamata watu na kuwafunga jela na gharama za huko ni za serikali. Kumbe tungewasajili, utaratibu ukafanywa na ile Kongo (mtaa) tukawajengea soko lao na pia maeneo wanayofanyia biashara, tungemaliza tatizo.
Mwandishi: Kuna haya malalamiko ya waendesha bodaboda kunyanyaswa na kuzuiwa kuingia mjini. Unalizungumziaje hili?
Slaa:Lazima watu waelewe kuwa kila kitu kina utaratibu wake. Upo ukweli kuwa baadhi ya bodaboda zinatumika kufanyia uhalifu. Mbaya zaidi wanatumia pikipiki hizo kusafirishia madawa ya kulevya. Huwezi kuwa na mji kama huo, hivyo sheria ifuatwe tu.
Mwandishi: Kuna tabia mbaya ya mgambo wa jiji kuvunja meza za wauza magazeti. Je, magazeti ni uchafu?
Slaa: Kuvunja meza za magazeti ni kosa, tunawaelimisha zisivunjwe lakini ziwe na muonekano mzuri. Zisizuie njia za waenda kwa miguu. Mawakala wa magazeti walikuja ofisini kwangu na nikawaelekeza cha kufanya.
Mwandishi: Kuna minong’ono kuwa mwakani utagombea Ubunge Jimbo la Ilala, mheshimiwa, kuna ukweli wowote?
Slaa:Hilo ndiyo kwanza nalisikia hapa Global.Kuna wakati watu walisema nataka kugombea jimbo la Dk. Makongoro Mahanga na hata Ukonga. Ukweli ni kwamba katika nchi hii ukifanya kazi sana watu wanaelekeza nguvu hizo kwenye uchaguzi.
Lakini mambo ya kugombea mbona bado? Kwanza hatujui tutagombea kwa katiba gani. Kwa hiyo hilo siyo kweli hata kidogo, tufanye kazi. Nikitangaza sasa sitawatendea haki wananchi, sasa hivi tunasambaza maendeleo manispaa yote.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger