Mradi huo unasimamiwa na kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) pamoja na Wakala wa Usambazaji Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga na wilaya ya Kahama.
Akizungumza leo Ijumaa Juni 5,2020 katika eneo la mradi huo unaotekelezwa katika kata za Ngogwa na Busoka,Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha ameipongeza SHUWASA,KUWASA na RUWASA namna wanavyotekeleza mradi huo kwa kasi kubwa.
“Nawapongeza sana SHUWASA,KUWASA na RUWASA kwa umoja wenu na ushirikiano na wananchi mnaoendelea nao katika kuhakikisha ujenzi wa mradi unakamilika kabla ya Mwezi Agosti mwaka huu. Lengo la serikali ni kuona wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama”,alisema Macha ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Kahama.
Aidha Macha alisema utekelezaji wa mradi wa Majisafi Ngogwa – Kitwana ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo kwani wananchi wanahitaji kuona maendeleo badala ya maneno tu.
“Tunatekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Wapuuzeni watu wanaokaa Hotelini na kuzungumzia masuala ya Ilani ya CCM. Huwezi kuelewa mambo mazuri yanayofanywa na serikali ukiwa Mjini umejiweka Karantini ‘Lockdown’, Wanaosema Ilani ya CCM haitekelezwi waje huku ‘site’ wajionee wenyewe jinsi miradi inavyotelezwa”,alisema Macha.
Mkuu huyo wa wilaya aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kukubali mabomba ya maji yapite kwenye maeneo yao kwani mradi huo hauna fungu la fidia ya ardhi na mali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Bi. Flaviana Kifizi alisema chanzo cha maji ya Mradi wa Kitwana – Ngogwa ni kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama – Shinyanga (KASHWASA).
“Eneo lililopendekezwa na wataalamu kama chanzo cha maji katika mradi wa Kitwana – Ngogwa ni Nyamhela ambapo limepita bomba la chuma lenye kipenyo cha mm.750 linalopeleka maji katika tenki linalomilikiwa na KUWASA na kuhudumia mji wa Kahama”,alisema Kifizi.
Alisema mradi huo unatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 27,095 baada ya kukamilika na wakazi wapatao 44,618 mwaka 2033 kwa kuwa mradi umesanifiwa kutoka huduma kwa kipindi cha miaka 15 na unatekelezwa na kutumia wataalamu wa ndani ‘ Force Account’.
Kifizi alieleza lengo kuu la mradi huo ni kufikisha huduma ya majisafi katika kata za Ngogwa na Busoka ambapo tayari ujenzi wa tenki la kukusanyia maji la ardhini ‘Ground water tank’ lenye ukubwa wa lita 680,000 katika kijiji cha Ngogwa umefikia asilimia 95.
Alisema pia ujenzi wa tenki la juu kwenye mwinuko ‘Riser’ la mita 12 lenye ukubwa wa lita 135,000 katika kijiji cha Kitwana umefikia asilimia 45 na hatua inayofuata sasa ni uchimbaji wa mtaro mkuu na ulazaji wa bomba kuu kilomita 15.26.