Saturday, 28 September 2024
TANZANIA YAANZA UZALISHAJI WA VIPURI VYA MIGODINI NA VIWANDANI KUPITIA EACS

Ni kupitia Kiwanda cha East Africa Conveyor Supplies Limited
*Kiwanda kinauza vipuri hadi nje ya nchi
*Kutumika migodini, viwanda vya saruji na viwanja vya ndege
*Ni sehemu ya mpango wa ufungaji wa Mgodi wa Buzwagi
📍 Kahama.
Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya uzalishaji wa vipuri vya migodini na viwandani, baada ya Kiwanda cha kisasa cha East Africa Conveyor Supplies Limited (EACS) kilichopo Kahama, Shinyanga kuanza rasmi uzalishaji wa vipuri vya mitambo vinavyotumika kwenye migodi na viwanda mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwa ni matokeo ya jitihada za Serikali katika kuweka mazingira bora na wezeshi ya uwekezaji hapa nchini pamoja na Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini.
Akizungumza Mjini Kahama, Mkoani Shinyanga na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini, Mkurugenzi Mtendaji wa EACS, Peter Kumalilwa, alisema kuwa kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa ubia wa asilimia 50 Mtanzania na asilimia 50 Wageni kimeanza uzalishaji mwezi Mei 2023, ambako hivisasa vipuri vinavyozalishwa ni pamoja na steel conveyor frames, drop brackets, steel conveyor rollers, impact conveyor rollers, plastic na steel caps for conveyor rollers na bidhaa hizo zinauzwa kwenye migodi mbalimbali nchini Tanzania kama Barrick North Mara, Barrick Bulyanhulu na Buckreef, pamoja na migodi iliyo katika nchi jirani kama Kibali Gold Mine uliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Lumwana Mine uliopo nchini Zambia.
Kiwanda hicho kimejengwa katika eneo la Mgodi wa Buzwagi, ambalo hivi sasa lipo katika hatua za ufungwaji na kubadilishwa kuwa Eneo Maalumu la Uwekezaji Kiuchumi (Buzwagi Special Economic Zone) baada ya kukamilika kwa shughuli za uchimbaji madini zilizokuwa zikifanywa na Kampuni ya Barrick, ambapo uzalishaji huo wa vipuri unafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa, hali inayowezesha bidhaa zake kukidhi viwango vya ubora na ushindani katika masoko ya ndani na kimataifa.
Kumalilwa alibainisha kuwa, malighafi nyingi zinazotumika katika kiwanda hicho, ikiwemo chuma na nondo, zinatoka katika viwanda vya ndani ya Tanzania, hivyo kuchangia katika ukuaji wa sekta ya viwanda nchini, sambamba na kupunguza gharama za uagizaji wa vipuri hivyo kutoka nje ya nchi kwa baadhi ya migodi hapa nchini.
Akifafanua kuhusu soko la bidhaa hizo, Kumalilwa alisema kwamba ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho umevutia masoko mengi, na wanatarajia kupanua biashara zao hadi nchi za Afrika Magharibi katika siku za usoni, na kwamba bdhaa hizo zinatumika katika viwanda vya saruji na viwanja vya ndege, huku akitoa rai kwa taasisi za kifedha kuwaunga mkono Watanzania ambao wamejikita kwenye uzalishaji wa vipuri au wanapanga kuanzisha viwanda kama EACS kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu na kuongeza kwamba, mikopo hiyo itawezesha Watanzania kushindana na wawekezaji wa nje ambao mara nyingi wana mitaji mikubwa.
Katika jitihada za kuendeleza sekta ya madini, Kumalilwa aliwasisitiza Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika migodi, badala ya kubaki mijini. “Nataka niwasisitize Watanzania kuwa madini ni maisha. Changamkieni hizi fursa. Tuje huku migodini tuangalie fursa gani tunaweza kufanya, hasa kwa kushirikiana na wawekezaji wa nje au kwa asilimia 100 ya Watanzania,” alisema Kumalilwa, akiongeza kuwa sekta ya madini inaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira na kuongeza viwanda nchini.
Kumalilwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tanzania Mining Industry Suppliers Association (TAMISA), alifafanua kuwa kuna shilingi trilioni 3.1 zinazozunguka kila mwaka katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, na iwapo wazawa hawatashiriki kikamilifu, fedha hizo zitaishia kwenda nje ya nchi. Aliwahimiza Watanzania kushikana mikono na kuanzisha viwanda vingi zaidi ili kusambaza bidhaa zinazohitajika katika sekta hiyo.
Aidha, aliishukuru Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yamewezesha kuzalisha bidhaa zinazokubalika katika soko la kimataifa. Alimshukuru pia Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, kwa kuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha kiwanda kinasimama.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Kahama Winnifrida Mrema alisema kuwa uwepo wa Kiwanda hicho ni jambo la kujivunia kwani ni moja kati ya miradi itakayosaidia kuliendeleza eneo la mgodi wa Buzwagi ambao upo kwenye hatua ya kufungwa baada ya shughuli ya uzalishaji wa dhahabu kukoma, hivyo kurahisisha upatikanaji wa vipuri ambavyo awali vilikuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi
Aliongeza kuwa, kupitia uwepo wa kiwanda hicho, watanzania watapata fursa ya kujifunza ujuzi kuhusu teknolojia mpya na kubainisha kuwa hatua hiyo ni moja ya uwekezaji mkubwa nchini unaoleta fursa za kiuchumi na ajira kwa Watanzania.
“Kuanzishwa kwa kiwanda cha EACS kinawakilisha hatua muhimu katika kuongeza thamani ya sekta ya madini na viwanda nchini Tanzania na kufungua milango kwa Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji, katika Eneo Maalumu la Uwekezaji Kiuchumi” alisisitiza Mrema.
Naye, Meneja wa Ufungaji Mgodi wa Buzwagi Zonnastraal Mumbi alieleza kuwa katika mipango ya ufungaji mgodi huo, moja kati ya hatua za uendelezaji wa eneo hilo ni kuanzishwa kwa Eneo Maalumu la Uwekezaji Kiuchumi (SEZ) ambapo viwanda tofauti vitajengwa katika eneo hilo kwa matumizi bora ya ardhi na kulinda ajira kwa manufaa ya mnyororo mzima wa shughuli za kiuchumi katika mji wa Kahama huku akiwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo.
Friday, 27 September 2024
TAMASHA KUBWA LA BIA TANZANIA, #SERENGETIOKTOBAFEST 2024, LIMERUDI TENA.
Mabibi na mabwana, Wapenda bia, Wapenda vibe, na wapenzi wa tamaduni za Kitanzania, Tamasha kubwa la Serengeti Oktoberfest lililokuwa likisubiriwa kwa hamu sana limerejea, na mwaka huu, UKUBWA NA UBORA wa #SerengetiOktobaFest2024 haukuwahi kutokea Kabla!.
Mwezi huu wa Oktoba, #SerengetiOktobaFest itakuwa sherehe kubwa itakayoangazia uhalisia wa Mtanzania na kuamsha uhai wa utamaduni wa Kitanzania kupitia mchanganyiko usiomithilika wa Bia, Vyakula na Utamaduni wetu.
Jiandae kwa tafrija ya kitamaduni isiyosahaulika itakayokuwa kivutio cha mwaka. Kama ilivyokuwa mwaka jana, tamasha liliadhimishwa kama tukio kubwa zaidi la bia la Afrika Mashariki, mwaka huu, Oktoberfest itafanya hivyo hivyo katika nchi tatu tofauti za Tanzania, Kenya, na Uganda.
Tamasha hili litaonesha utambulisho wa kipekee wa kitamaduni wa kila eneo kupitia onesho lililopangwa na likapangika la vyakula vya nyumbani, muziki na utamaduni, huku bia yako pendwa ya Serengeti ikitumika kama kiunganisho kinachotuleta pamoja.
Kaa tayari na endelea kutufuatilia kwenye Kurasa za mitandao ya kijamii ya bia yako pendwa ya Serengeti ili kujua tarehe na eneo kutakapowekwa historia nyingine kubwa yenye kutuunganisha Waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatuna Jambo dogo na nikuhakikishie tu kuwa #SerengetiOktobaFest 2024 inatazamiwa kuongeza joto na kutuleta pamoja kwenye kusherehekea bia yetu pendwa, utamaduni na vyakula vyetu.
TANZANIA MINING COMMISSION VISITS EAST AFRICA CONVEYOR SUPPLIES FACTORY IN BUZWAGI SPECIAL ECONOMIC ZONE
Peter Andrew Kumalilwa, CO - Founder of East Africa Conveyor Supplies Limited (EACS)
MKUU WA MAJESHI YA ULINZI TANZANIA ATEMBELEA MSUMBIJI
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali J.J. Mkunda amefanya Ziara ya Kikazi nchini Msumbiji kuanzia tarehe 23 hadi 27 Septemba, 2024.
Wakati wa ziara hiyo, pamoja na masuala mengine, Jenerali Mkunda alitembelea Ubalozi wa Tanzania uliopo Jijini Maputo tarehe 24 Septemba, 2024 na tarehe 25 Septemba, 2024 alishiriki kwenye Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Msumbiji.
Wakati wa Maadhimisho hayo, Jenerali Mkunda alitunukiwa na Mhe. Filipe Jancito Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Nishani Maalum ya Heshima kwa kutambua na kuheshimu mchango wa Tanzania katika ukombozi na ustawi wa amani na usalama nchini Msumbiji.
Vilevile, tarehe 26 Septemba 2024, Jenerali Mkunda alikutana na mwenyeji wake, Admiral Joaquim Rivas Mangrasse, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Msumbiji na kuzungumza masuala mbalimbali ya Ushirikiano kati ya JWTZ na Jeshi la Ulinzi la Msumbiji (FADM) ambapo Viongozi hao walikubaliana na kusisitiza juu ya haja ya kuendelea kushirikiana kwa ukaribu kwa maslahi ya nchi zetu mbili
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania - Maputo.
26 Septemba, 2024.
TACOGA KUSHIRIKISHA TAASISI ZA ELIMU ZA CHINI MPANGO WA KUJENGA KIZAZI CHENYA MAADILI
Na Hadija Bagasha Tanga,
CHAMA cha Ushauri wa Wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati Tanzania (TACOGA 1984) kinafikiria kushirikisha taasisi za elimu za chini kwenye mpango wa kujenga kizazi chenye maadili kuanzia elimu ya awali msingi hadi vyuo vikuu, hatua hiyo inayokuja mara baada ya kubainika maadili kwa jamii yameporomoka.
Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa katibu Mkuu Wizara ya elimu Akwila Sawaya ambaye ni Mdhibiti Mkuu Ubora wa shule kanda ya Kaskazini Mashariki kwenye Mkutano wa Chama cha Ushauri wa Wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati unaofanyika katika jiji la Tanga ikiwa na dhamira ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo masula ya jinsia na elinmu jumuishi kwa wanafunzi.
Amesema kwamba vyuo vikuu vinaweza kushiriki kujenga kizazi chenye maadili kinachoweza kuwa msaada kwa Taifa lakini pia wanaamini watafanya kazi kubwa ya kurejesha vijana wao kwenye tamaduni zinazokubalika na hatimaye kupata viongozi na wataalamu wazuri wenye maadili na wanaofata tamaduni za Tanzania.
“Chama kina malengo na lengo kubwa ndio hilo kama kuhakikisha kwamba elimu jumuishi inakuwepo lakini pia suala la maadili na tamaduni zetu zinazingatiwa kwa vijana wetu hivyo kinachotakiwa kufanya ni kushirikisha na shule nyingine taasisi za elimu za chini kwasababu kuna vyuo vya kati na vyuo vikuu lakini pia bado tunahitaji elimu wanayotoa ifike kwa vijana na watoto kuanzia shule za awali, msingi na sekondari,”alisema
“Changamoto kubwa ambayo imeonekena ni gharama za uendeshaji ni kubwa hivyo tutashirikisha wizara yetu kwa umuhimu wa jambo hili katika elimu kwakuwa hakuna elimu bila maadili huwezi ukasema unamtengeneza mwanafunzi kiakili lakini kimaadili akawa hayaendi sawa na utamaduni wa kitanzania,”alisisitiza
Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA,Prof. Mohamed Makame Haji, ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya wadhamini wa chama hicho amesema mkutano huo unaangalia kwa namna gani chama hicho kinaweza kuwa sehemu kuu ya kutatengeneza wanafunzi na kuwa raia wema wanapohitimu mafunzo yao.
“Chama hiki kina mchango mkubwa sana katika kuwatengeneza wanafunzi ili kuwa wanafunzi bora ili wawapo katika vyuo na taasisi nyingine za elimu lakini pia kuwa raia wema wanapohitimu mafunzo yao na kutengeneza jamii ambayo ina uelewa na inayokwenda na maadili na kuwa na viongozi ambao watakuwa wasimamizi wazuri na wenye kujielewa,”alisema Prof.Makame.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha cha Dodoma(UDOM),Prof.Lughano Kusiluka ,anasema jamii inatakiwa kusadia kujenga kizazi chenye maadili baaada ya dalili zilizopo kuonesha maadli yameporomoka kwa kiwango kikubwa.
Mkutano huo wa siku tatu,wa mafunzo maalumu kuhusu elimu jumuishi na mkutano mkuu wa wa washauri na wanasihi wa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu na kati TACOGA 1984 ,mumeshirikisha wajumbe zaidi na 108.

















































