Monday, 31 January 2022
Sunday, 30 January 2022
SERIKALI YAAHIDI MAZINGIRA BORA ZAIDI SHIRIKA LA POSTA
MHESHIMIWA YAKUBU AIPONGEZA UDSM KWA MIKAKATI YA KUKUZA VIPAJI KUPITIA SANAA NA UBUNIFU
KATIBU CCM :TARIME SIYO YA MCHEZO ITAKUPANDISHA CHEO,ITAKUSHUSHA ITAKUONDOA
Na Dinna Maningo, Tarime
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Tarime mkoa wa Mara Valentine Maganga amesema kuwa watu wa wilaya ya Tarime ni majasiri si waoga na hawana aibu kumkosoa mtu.
Akizungumza na Malunde 1 blog Katibu huyo alisema kuwa wananchi wa Tarime wako tayari kumkosoa mtu yeyote na hawana mambo ya kona kona kwa kuwa ukosoaji kwao ni utamaduni.
"Tarime siyo ya mchezo ni wilaya ya kuwapima viongozi ukiletwa Tarime ujue kuna kupanda cheo au kushushwa,watu wake ni majasiri hawana aibu, kukukosoa kwao ni jambo la kawaida ni watu wasio na kona kona ukikosea hawaogopi kusema kwa sababu ndiyo utamaduni wao" amesema Maganga.
Maganga amewaomba viongozi wa Chama na Serikali walioko Tarime kushirikiana katika maendeleo na kutatua changamato zinazowakabili wananchi kwakuwa hitaji kubwa la wananchi ni kusikilizwa na kutatuliwa kero zao.
Wakizungumza na Malunde 1 blog kwa nyakati tofauti,Baadhi ya wananchi wameunga mkono kauli hiyo,Mwita Ryoba mkazi wa kijiji cha Matongo-Nyamomgo anasema kuwa wilaya hiyo hutizamwa kama mahali pa kuwapima viongozi utendaji wao wa kazi.
"Tarime ndiyo kipimo cha viongozi maana sisi watu wa Tarime hatuna uoga wala kumvumilia kiongozi anayekwenda kinyume tunapenda haki na hatupendi uonevu na tuna ujasiri ambao unatusaidia kutoogopa kumkosoa mtu yeyote hata kama ni kiongozi wakurya ndiyo tuko hivyo hata akija mgeni akiishi Tarime naye anakuwa jasiri", anasema Ryoba.
John Mseti mkazi wa kijiji cha Turugeti kata ya Bumera anasema" Tarime ni kipimo cha matendo ya watu hasa viongozi tumeshuhudia baadhi walioletwa kufanya kazi Tarime wakashushwa vyeo na wengine kuondolewa kwenye nafasi za kazi"
"Wapo waliokuwa DC Tarime walitumbuliwa ,wapo walioletwa kuwa RPC wamepanda kutoka kuongoza wilaya mbili za kipolisi Tarime/Rorya sasa wanaongoza mikoa,wapo waliokuwa OCD hapa Tarime leo ni RPC,wapo watendaji waliokuwa nafasi za kawaida na wamepanda vyeo huko Serikalini na kwenye vyama" anasema Mseti .
Chacha Marwa mkazi wa mtaa wa Sabasaba anasema kuwa watu wa Tarime si wakorofi kama inavyodhaniwa bali ni watu wanaojiamini,wenye msimamo,wanapenda haki na hawapendi kuonewa.
Rhobi Marwa mkazi wa Rebu anasema kuwa faida ya mtu kuwa jasiri inamsaidia kutokuwa na uoga katika kufanya maamuzi sahihi na kwamba kumkosoa mtu ni kumsaidia kujua tatizo lake ili ajisahihishe.
Muhiri Chacha Mkami mkazi wa kijiji cha Nyangoto kata ya Matongo anasema"Watu wa Tarime usiwaone hivyo ukija kama wewe ni kiongozi huwa hawana papara watatulia kwanza we utaona hawasemi jambo kumbe wanakupima kwanza matendo yako,siku wakikuamria hutoboi.
"Hata kwenye siasa ukipewa uongozi alafu ukaichezea nafasi uliyopewa kukubadilikia ni dakika moja ndiyo maana utaona Tarime inaongozwa na CCM na Chadema wao hawaangalii chama wanaangalia mtu atakayefaa bila kujali anatoka chama gani,ukifanya vizuri watakusema kwa mazuri ukifanya vibaya utasemwa kwa mabaya" anasema Muhiri.
Lucy John anasema kuwa watu wa Tarime ni wachapa kazi si tegemezi na ujituma kuhakikisha wanajiinua kiuchumi wakiwemo wanawake na hata uchumi ukiyumba hawakati tamaa kutafuta pesa.
DC SHEKIMWERI ATAKA JAMII KUKOMESHA MAUAJI, WIZI
*****
Na Dotto Kwilasa Malunde 1 blog- DODOMA.
MKUU wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kukubali kusimamia ulinzi na usalama wao kwa kushirikiana kuwabaini watu wenye viashiria vya vitendo viovu hali itakayopunguza mauaji yanayotokea mara kwa mara.
Aidha ameuagiza uongozi wa Kata ya Kikuyu kwa kushirikiana na Kamati ya ulinzi na usalama kusimamia suala la usalama kutokana na kuibuka kwa vitendo vya wizi pamoja na mauaji katika eneo hilo.
Shekimweri ametoa maagizo hayo jana Jijini Dodoma wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kikuyu Kusini wakati walipokuwa wakitoa kero mbalimbali zilizopo katika eneo hilo.
Aidha ametaka pia Viongozi wa dini kuhubiri suala la kuwajenga kiroho wananchi ili kuwa na hofu ya Mungu kwani hivi sasa kumekuwa na matukio ya ajabu ambayo yanatishia usalama wa maisha ya watu.
"Naomba Viongozi husika mkae mjadili haya masuala ya usalama kama ajenda wapi wakristo wanaenda kwenye jumuiya hebu muongelee na masuala ya upendo mnapokutana haiwezekani watu wanafikia hatua ya kutoana uhai suala hili halikubaliki,"amesema
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha anatekeleza kero za wananchi hao hasa suala la fidia ya viwanja kutokana na mashamba yao kuchukuliwa na Serikali kwa ajili ya maendeleo.
Pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kuzingatia suala usafi wa mazingira ili kuhakikisha Jiji linakuwa na hadhi ya Makao Makuu.
"Hapo baadae nitakuja na Sheria nikikuta mazingira yako ni machafu tutakutoza faini wala hakutakuwa na mjadala na katika kuonyesha kuwa tupo makini na hilo tayari tumeajiri migambo wa Jiji kutekeleza hilo,"amesema.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ,Joseph Mafuru ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa wapo katika mchakato wa kuwapatia viwanja wananchi ambao mashamba yao yamechukuliwa kama fidia.
Alisema jumla ya wananchi 328 wa Kata ya Kinyambwa wa Jijini hapa watapatiwa viwanja kama fidia kwa mashamba yao yalichukuliwa na Jiji kwa ajili ya uendelezaji wa Jiji hilo.
Mafuru alisema mpaka hivi sasa tayari wameshatoa viwanja 25 kati ya 328 ambapo zoezi la upimaji linaendelea ili kuweza kukamilisha haraka na kugawa viwanja hivyo.
Awali baadhi ya wakazi hao wameeleza kero zinazo wakabili wamesema waliahidiwa na Jiji hilo kupewa viwanja mbadala baada ya kuwachukulia mashamba yao lakini mpaka sasa bado hawajapewa.
"Mheshimiwa Mkurugenzi tunaomba uliangalie suala hili kwa umakini kwani imekuwa ni muda mrefu sasa hatuoni kinachoendelea kuhusiana na suala hili la kupatiwa haki zetu,"walisema.
Pia wamelalamikia kitendo cha baadhi ya watu kutupa taka ovyo katika maeneo ya makazi ya watu bila kuchukuliwa hatua na kutaka suala hilo kutatuliwa kwani ni kero kwao inayoweza kusababisha maradhi ya magonjwa ya mlipuko.
"Huu ni msimu wa mvua ,hali ya uchafu imezidi kuwa mbaya zaidi,takataka kila kona,tunaomba Mkurugenzi utusidie suala hili la sivyo magonjwaya mlipuko yatatumaliza,"wamesema baadhi ya wananchi hao.
TPC YATAKIWA KUBUNI HUDUMA MPYA ZA WATEJA KWA KUTUMIA MFUMO WA ANUANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI
*****
Na Dotto Kwilasa Malunde 1 Blog,DODOMA.
SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC) limetakiwa kutumia mfumo wa anuani za makazi na postikodi kubuni huduma mpya kwa wateja ili utekelezaji wa mfumo huo utakapokamilika uweze kutumika ipasavyo kufikisha huduma na bidhaa kwa wateja.
Hayo yameelezwa na jana Jijini hapa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Teddy Njau wakati akifungua semina ya mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu mfumo wa anuani za makazi na postikodi kwa Mameneja wa Mikoa ya Shirika hilo wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Njau amewataka washiriki hao kuweka anuani za makazi kwenye maeneo yao; kwa wateja wao na kubuni huduma mpya zitakazotumiwa na wateja kupitia mfumo wa anwani za makazi utakapokamilika utekelezaji wake kwa kuwa Shirika hilo lina mtandao mpana nchi nzima na ni wadau wa msingi wanaotakiwa kutumia miundombinu hiyo.
“Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha anuani za makazi zinawekwa na kutumika nchi nzima, leo mnapatiwa mafunzo ya kujenga uelewa ili mkasimamie na kushiriki utekelezaji wa mfumo huu kwenye mikoa yenu Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuwa ninyi ni wadau muhimu na ni wajumbe kwenye kamati za kitaalamu,” amesisitiza Njau
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo, Caroline Kanuti amesema kuwa mfumo wa anuani za makazi utakuwa wa kidijitali ili kutoa fursa kwa Serikali kutekeleza majukumu ya sensa ya watu na makazi ili anuani zijumuishwe kwenye sensa inayoanza mwezi Agosti mwaka huu.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi utafanyika kwa miezi mitano nchi nzima kwenye kata na wadi 4,174; halmashauri 196 na mikoa 31 ili zoezi hili likamilike ipasavyo na taarifa zake ziwekwe kwenye tovuti maalum na zitumike kwenye simu za mkononi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi
Naye Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Macrice Mbodo amesema kuwa Shirika lake ni mdau muhimu katika anuani za makazi na postikodi ndani na nje ya nchi kwa kuwa posta zote duniani zina jukumu la kutoa anuani zinazotambulika na muundombinu huu utakapokamilika Shirika litatumia anwani za makazi kusafirisha huduma na bidhaa kwa wananchi mpaka nyumbani kwa kuwa tayari tuna duka mtandao.