Waziri wa Madini , Anthony Mavunde akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) juu ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini nchini
-Mgodi wa North Mara viongozi wake kwa asilimia 100 ni Watanzania
Waziri wa madini,Mh.Antony Mavunde amesema mgodi wa North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara ambao unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals umekuwa kinara katika utekelezaji wa sheria na kanuni ya Maudhui ya Ndani (Local Content) ikiwemo upande wa ajira ambapo asilimia 100 ya viongozi wanaoendesha mgodi ni Watanzania.
Mbali na viongozi wa mgodi huo pia Meneja wa Barrick nchini (Country Manager) ni Mtanzania.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini, Mhe. Mavunde amesema kwenye miradi ya madini, amesema kumeshuhudiwa ongezeko la ajira kwa watanzania kutoka ajira 6,668 kati ya ajira 7,003 sawa na asilimia 95 kwa mwaka 2018 hadi kufikia ajira 18,853 kati ya ajira 19,356 sawa na asilimia 97 kufikia Desemba 2024.
Amesema katika nafasi zinazohitaji kupata uzoefu kutokana na kukua kwa teknolojia duniani, kumekuwa na utaratibu wa kisheria wa urithishwaji wa Watanzania kwa nafasi zinazoshikiliwa na Wataalamu wa Kigeni na kutoa mfano wa kampuni ya Barrick kupitia mgodi wake wa North Mara ambapo nafasi zote za juu za uongozi wanaoendesha shughuli kwa weredi mkubwa zinashikiliwa na Watanzania kwa asilimia 100.
Kupitia mkutano huo Waziri Mavunde pia ametangaza rasmi orodha ya Huduma na Bidhaa 20 zinazopaswa kutolewa Migodini kupitia kampuni zinazomilikiwa na watanzania kwa asilimia 100 ikilenga kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzimawa sekta ya madini baada ya kufanywa marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini za Mwaka 2018.
"Kwa awamu ya kwanza tarehe 14 Novemba, 2025 Tume ya Madini ilitangaza orodha ya bidhaa na huduma zinazotakiwa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa na kampuni za kitanzania kwa asilimia 100, ambapo kwa mara ya kwanza Tume ya Madini itatatangaza kupitia Kanuni 13A," amesema Waziri Mavunde.
Akizungumzia manunuzi ya huduma na bidhaa kwa kampuni za kitanzania amesema yameongezeka kutoka kiasi cha Shilingi trilioni 1.85 kati ya manunuzi ya huduma na bidhaa za jumla ya kiasi cha Shilingi trilioni 3.01 sawa na asilimia 62 kwa mwaka 2018 hadi kufikia Shilingi trilioni 4.41 ambayo ni sawa na asilimia 88 ya kiasi cha Shilingi trilioni 5.00 ya manunuzi yote yaliyofanyika mwaka 2024.
Pia amesema Serikali inaendelea kufungua wigo kwa ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini na kuongeza manufaa ya rasilimali madini kwa kutenga eneo maalum la uwekezaji la ulipokuwa Mgodi wa uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu la Barrick Buzwagi lenye ukubwa wa ekari 1331, kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za migodini na kusema tayari viwanda sita vimekwisha jengwa huku wamiliki wa viwanda 15 wakionesha nia ya kujenga viwanda katika eneo hilo.
Waziri Mavunde ameitaka sekta binafsi nchini Tanzania kuchangamkia fursa ya usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma migodini ili kuhakikisha fedha kiasi kikubwa inabaki nchini Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Amewasisitiza wawekezaji wote kuzingatia Sheria za madini na utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji Watanzania kwenye sekta ya madini sambambamba na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika miradi ya madini ili kukabiliana na changamoto za ajira kwa manufaa ya mtu mmoja mmoja na manufaa ya taifa.




0 comments:
Post a Comment