Saturday, 4 April 2020
Wanaokunywa Pombe Kali Kwa Madai Ya Kujikinga Na Corona Wapewa Onyo
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amewaonya wananchi wa mkoa huo wanaoaminisha vijana kuwa pombe kali inaweza kutibu virusi vya corona kuacha mara moja imani hizo potofu, na kuwataka kuendelea kujikinga kwa kutumia vitakasa mikono na kuepuka makundi mbalimbali.
Chalamila amezungumza mara baada ya kukabidhiwa vifaa maalum vya kunawia mikono vilivyobuniwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST) ili kusaidia makundi mbalimbali kujikinga dhidi ya janga hilo.
Kiongozi huyo amesema baadhi ya watu wanafanya utani kwa kutumia pombe kali kusafisha mikono yao badala ya kutumia vitakasa mikono maalum vilivyoundwa kwa kazi hiyo.
“Na wengine wameanza kunywa pombe, wanasema kuwa wakilewa hawawezi kupata corona [virusi], mnajidanganya,” amesema Chalamila huku akiwataka wananchi kufuata utaratibu unaotolewa na wataalamu wa afya.
Vifaa vilivyotolewa na chuo hicho vitawasaidia wananchi lakini pia vitawaepusha kushika sehemu ambapo mtu mwingine ameshika mfano wakati wa kufungua koki au kuminya sauti.
Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ( MUST) leo kimemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila mashine ya kunawia mikono iliyotengenezwa na wanafunzi wa chuo hicho kwa ajili kusaidia juhudi za Mkoa katika kujikinga na virusi vya Corona (COVID-19) pic.twitter.com/WDLQaghct0— Ofisi ya MKuu wa Mkoa Mbeya (@OfisiWa) April 1, 2020
Waziri Wa Elimu Aagiza Walimu Wote Walioanzisha Vituo Vya Tution Baada ya Shule Kufungwa Kuepuka Corona Wakamatwe
Waziri wa Elimu, Sanyansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amewaagiza wakurugenzi, wakuu wa wilaya na mikoa kuwachukulia hatua wale wote walioanzisha vituo vya mafunzo ya ziada (tuition) wakati ambao shule zote zimefungwa kwa ajili ya kujikinga na corona.
Profesa Ndalichako alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kuwataka wanafunzi walioko nyumbani kuacha kuzurura ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
“Wanafunzi watambue kuwa hiyo si likizo bali wamerudi nyumbani kwa sababu ya janga kubwa linaloitesa dunia la virusi vya corona. Kuna baadhi ya sehemu baada ya kusikia watoto wako nyumbani wameanzisha ‘tuition’. Nawataka wote walioanzisha ‘tuition’ waache mara moja,” alionya.
Ndalichako alitoa maelekezo kwa wakurugenzi, wakuu wa wilaya na mikoa, wasimamie kikamilifu maelekezo ya serikali na kutowafumbia macho watu walioanzisha vituo vya kufundishia kwa sababu wanapingana na maelekezo na wanakuwa tishio la usalama katika maeneo hayo.
Kadhalika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Watoto (Unicef), wametoa angalizo na tahadhari ambazo watoto, wazazi, walezi na walimu wanapaswa kuzichukua wakati wote wa likizo.
“Kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona, walimu wakuu wasiwaruhusu wanafunzi kukusanyika katika maeneo shule kwa kipindi chote ambacho shule zimefungwa,” tangazo lilielekeza hivyo.
Tahadhari nyingine iliyotolewa, inaitaka jamii iwalinde wanafunzi na watoto wote katika maeneo yao kwa kuhakikisha hawaendi katika maeneo hatarishi yakiwamo yenye msongamano.
Kadhalika wametahadharisha wazazi na walezi wazungumze na watoto wao kuhusu njia za kujikinga na virusi vya corona na kuwasaidia kuendelea kujisomea wakiwa nyumbani.
Mahakama yataifisha bilioni 16 za upatu kuwa mali ya serikali.
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa maarufu kama Mahakama ya Ufisadi imetaifisha zaidi shilingi bilioni 16 za upatu kuwa mali ya serikali.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga kuwasilisha maombi mahakamani hapo kuomba fedha hizo zitaifishwe kwa kuwa washtakiwa katika kesi hiyo hawajawahi kufika mahakamani.
Jaji wa mahakama hiyo, Elinaza Luvanda ametoa uamuzi huo baada ya kujiridhisha na vielelezo vilivyowasilishwa na DPP dhidi ya washtakiwa hao.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Huebenthal raia wa Ujerumani, na Frankricket raia wa Uingereza.
Februari 11, 2019, DPP aliwafungulia mashtaka matatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam lakini hawajawahi kuripoti.
Katika kesi ya msingi washtakiwa hao wanadaiwa kuja nchini na kuanzisha Kampuni ya IMS Marketing Tanzania Limited, Novemba 19, 2014 na kupewa usajili wa namba 113133, ambapo baadaye walianza kuendesha upatu kinyume na sheria.
Katika kipindi hicho, washtakiwa hao wanadaiwa kuanza kusaini nyaraka mbalimbali kwa mawakili kwa ajili ya hiyo kampuni, ambapo Aprili 23, 2015 walifungua akaunti mbili za dola za Marekani katika Benki ya Afrika (BOA), Tawi la NDC jijini Dar es Salaam kwa jina la Kampuni ya IMS.
Aidha, baada ya kutaifishwa kwa fedha hizo Jaji Luvanda aliyesikiliza shauri hilo, amekataa ombi la DPP la kutaka mahakama itoe amri ya kuamrisha Benki ya BOA kulipa riba ya kipindi chote walichohifadhi fedha hizo.
Juhudi Za Wizara Ya Madini Kufungua Masoko Ya Madini Yasababisha Wachimbaji Wadogo Kuvamia Maeneo Ya Migodi Midogo[rush].
Bunge limeelezwa kuwa ,Kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara ya Madini katika kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kufungua masoko ya madini nchi nzima, kumesababisha ongezeko la wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakivamia maeneo mbalimbali ya Migodi midogo (rush) .
Taarifa hiyo imetolewa April 3,2020 Bungeni jijini Dodoma kutoka wizara ya Madini kwa njia ya Maandishi wakati Wizara hiyo ikijibu swali la mbunge wa viti Maalum Salome Wycliffe Makamba aliyehoji Je, ni sifa zipi ambazo mzabuni anatakiwa kuwa nazo ili kupewa nafasi ya usimamizi mapato ya Serikali kwenye migodi midogo midogo (Rush) kama Mwabomba, namba Mbili, Segese.
Katika Majibu ya Wizara ya Madini imefafanua kuwa maeneo ambayo yanavamiwa zaidi na wachimbaji wadogo ni yale yaliyotengwa, maeneo yenye leseni kubwa za utafiti, maeneo ya uchimbaji mkubwa, maeneo yasiokuwa na leseni, na maeneo ambayo leseni zake hazijaendelezwa kwa shughuli za uchimbaji.
Aidha Majibu ya wizara hiyo yameendelea kufafanua kuwa ,Serikali kupitia Tume ya Madini ilitoa Waraka wa Ndani Na. 3 ulioanza kutumika tarehe 15 Oktoba, 2019 wenye dhumuni la kutoa mwongozo kwa Maafisa Madini Wakazi na watumishi wengine katika kusimamia, kudhibiti shughuli za madini na mapato ya Serikali katika maeneo yenye Migodi midogo[rush.]
Kwa mujibu wa Waraka huo, utaratibu unaotumika kuwapata wasimamizi wa rush ni kupitia Kamati ya Uongozi inayofuatilia na kuimarisha usimamizi katika eneo la rush.
Majibu ya Wizara ya madini yameendelea kubainisha kuwa ,Kamati hiyo huteua Wasimamizi wa migodi midogomidogo[ rush], ambapo Mwenyekiti wa rush anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:- Awe mchimbaji mzoefu hasa katika usimamizi wa maeneo ya aina hiyo; Asiwe na historia ya wizi wa fedha za Serikali; na Awe mwaminifu.
Aidha, wajumbe wengine kwenye usimamizi wa rush ni pamoja na Katibu, Mweka Hazina, M/kiti wa Kijiji, M/kiti wa Kitongoji, Mjumbe wa REMA, TAWOMA na Mwakilishi wa eneo/shamba.
Serikali Yasema Uboreshaji Wa Elimu Hapa Nchini Ni Endelevu
Serikali imesema Suala la uboreshaji wa utoaji wa Elimu hapa nchini ni endelevu, ambalo litaendelea kutokana na mabadiliko yanayotokea .
Hayo yamesemwa April 3,2020 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe.William Ole Nasha wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum Mhe.Zainab Athuman Katimba aliyehoji Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanyia maboresho Mfumo wa Elimu Tanzania?
Katika majibu yake kwa njia ya Maandishi Naibu Waziri wa Elimu Mhe.William Ole Nasha amesema maboresho ya Elimu ni endelevu katika utegemezi wa nyanja za kiuchumi na kijamii, pamoja na ulinganisho wa maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Mhe.Nasha ameendelea kufafanua kuwa , suala la uboreshaji wa mifumo ya elimu limekuwa likifanyika na hutegemea tathmini mbalimbali za kitaalamu zinazofanyika kwa nyakati tofauti ,Mfano elimu ya sekondari ya chini (O Level) kutambuliwa kuwa ni sehemu ya Elimumsingi na inatolewa bila malipo ya ada.
Aidha, katika elimu ya ualimu Mhe.Nasha amesema serikali imeongeza miaka ya kumwandaa mwalimu wa elimu ya awali kutoka miaka 2 kuwa miaka 3.
Pamoja na mabadiliko hayo, Serikali imeendelea na uimarishaji wa elimu Tanzania kuwa ya umahiri (Competence based) kutoka katika mfumo wa awali ambao ulimwandaa mhitimu kwa nadharia bila mafunzo kwa vitendo ya kutosha.
Pia Nasha amesema Uboreshaji huo umefanyika sambamba na uimarishaji wa mitaala katika ngazi zote.
Katika kuboresha mfumo wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi, Serikali imeunda mabaraza ya ujuzi ya Kisekta ambayo yanakuwa kiungo kati ya Vyuo vya Elimu ya Ufundi na wadau, vikiwemo viwanda na waajiri ambapo Mabaraza hayo yatahakikisha kuwa mitaala inayotumika inakidhi mahitaji ya wadau na soko la ajira.
Elimu Juu Ya Tahadhari Ya Corona Bado Haitoshelezi
Mpaka sasa hakuna dawa wala chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona hivyo njia bora ya kupambana na ugonjwa huo ni utoaji wa elimu juu ya tahadhari za kujikinga ili mtu asipate ugonjwa huo ambapo kwa Mkoa wa Songwe Elimu hiyo bado haitoshelezi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameyasema hayo wakati wa kikao cha Wadau wa Afya waliokutana mapema leo kujadili utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwa Mkoa wa Songwe.
Brig. Jen. Mwangela amesema hadi sasa kuna maeneo bado wananchi hawajapata elimu ya tahadhari ya kujikinga na virusi vya Corona huku akiwaagiza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Waganga Wakuu wa Wilaya zote kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wote.
Amesema elimu itolewe kwa kutumia vyombo vyote vya habari vilivyopo na kwa namna zote bora ambazo zitawezesha kuwafikia wananchi wote na kwa wataalamu wa afya ambao baadhi yao bado hawana elimu hiyo.
Brig. Jen. Mwangela ameongeza kwa kulitaka Jeshi la Polisi Mkoani Songwe kuendelea kufanya ukaguzi katika mabasi yote endapo yanazingatia tahadhari za kujikinga na Ugonjwa wa Virusi vya Corona pia wananchi wote waepuke mikusanyiko isiyo ya lazima.
Amesema taasisi zote ziendelee kuchukua hatua za tahadhari zilizo elekezwa na wataalamu wa Afya huku akimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za haraka kutokana na kuwa maji ya kunawa katika geti la kuingilia Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa yalikua hayana dawa hali ambayo sio sahihi.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Hamad Nyembea amesema atahakikisha tahadhari za kujikinga na Ugonjwa wa Virusi vya Corona zinachukuliwa katika hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe huku akieleza kuwa tayari wameweka utaratibu wa kupima jotoridi watu wote wanaoingia hospitalini hapo.
Dkt Nyembea amesema hapo awali watu wengi walikua wakichukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Virusi vya Corona na Kufuata maelekezo ya wataalamu wa Afya lakini sasa baadhi wameanza kupuuzia hivyo anawasihi wasifanye hivyo kwani ugonjwa huo bado ni tishio.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila amesema Mkoa wa Songwe ni lango kuu la kuingilia na kutoka katika nchi za SADC hivyo hatua za tahadhari juu ya Corona zinazo chukuliwa zinapaswa kuwa madhubuti Zaidi kuliko maeneo mengine.
Download App Yetu Kwenye Simu Yako Ili Uweze Kupata Habari Zetu Kwa Haraka Zaidi
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa urahisi kabisa kupitia simu yako ya mkononi muda wowote hata usiku wa manane au ukiwa kazini...
Pata kurasa za mbele Magazetini, habari za kitaifa, matukio yote ya kisiasa, burudani na udaku kupitia simu yako ya mkononi.
Pata kurasa za mbele Magazetini, habari za kitaifa, matukio yote ya kisiasa, burudani na udaku kupitia simu yako ya mkononi.
Huhitaji tena kuwa na Computer. Ingia Play Store, pakua App yetu tukuhabarishe masaa 24.
Ni rahisi tu << BOFYA HAPA KUPAKUA APP YETU>>
Friday, 3 April 2020
Profesa Anne Tibaijuka Aaga Bunge Kwamba Hatagombea Tena
Mbunge wa Muleba Kusini Balozi Profesa Anna Tibaijuka, leo Aprili 3, 2020, amewaaga rasmi Wabunge wenzake na kusema Bunge lijalo atakua ameng'atuka madarakani na kwamba anaenda kuandika kitabu chake.
Aidha Profesa Tibaijuka akizungumzia suala la Virusi vya Corona, ameiomba Serikali kuangalia njia mbadala ikiwemo kutumia tiba za asili ili kuweza kukabiliana na ugonjwa huo kwa sababu hao wazungu wanaotuletea tiba zao sasa, hapo kabla walitukuta na tiba zetu za asili.
"Sisi lazima tuwe na mpango mbadala ambao unajikita kwenye jamii yetu, inabidi tuseme tiba zetu mbadala ziko wapi, hakuna jamii itakayokaa kusubiri kifo lazima itajihami, tayari nimemuandikia barua Dkt Ndugulile ya kwamba lazima tuangalie Plan B, nashukuru sana wananchi wa Muleba kwa kunipa nafasi kwa miaka 10 nimejifunza mengi, naenda kuandika kitabu" amesema Profesa Tibaijuka.
Aidha Profesa Tibaijuka akizungumzia suala la Virusi vya Corona, ameiomba Serikali kuangalia njia mbadala ikiwemo kutumia tiba za asili ili kuweza kukabiliana na ugonjwa huo kwa sababu hao wazungu wanaotuletea tiba zao sasa, hapo kabla walitukuta na tiba zetu za asili.
"Sisi lazima tuwe na mpango mbadala ambao unajikita kwenye jamii yetu, inabidi tuseme tiba zetu mbadala ziko wapi, hakuna jamii itakayokaa kusubiri kifo lazima itajihami, tayari nimemuandikia barua Dkt Ndugulile ya kwamba lazima tuangalie Plan B, nashukuru sana wananchi wa Muleba kwa kunipa nafasi kwa miaka 10 nimejifunza mengi, naenda kuandika kitabu" amesema Profesa Tibaijuka.
DC Katambi Ampa Siku 3 Masanja Mkandamizaji Kuripoti Ofisini Kwake Jijini Dodoma Baada Ya Kufanya Mzaha Juu Ya Corona
Mkuu wa Wilaya Dodoma Mjini Mhe.Patrobas Katambi amempa siku 3 Mwigizaji wa vichekesho Emanuel Mgaya[Masanja Mkandamizaji ]kuripoti Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Dodoma baada ya kuleta Mzaha juu ya suala la Corona.
Akizungumza jijini Dodoma mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Mkuu huyo wa wilaya mhe.Patrobas Katambi amesema Mwigizaji huyo, Emmanuel Mgaya [Masanja Mkandamizaji ]ambaye pia anafanya vipindi kupitia Shirika la Utangazaji Ujerumani [DW]akiwa Jijini Dodoma amefanya Mzaha juu ya ugonjwa wa Corona hivyo anatakiwa kuripoti ofisini kwa mkuu wa wilaya Dodoma kujibu tuhuma kwanini analeta mzaha .
“Mhe.Mkuu wa Mkoa kuna jambo muhimu nimeliona ,ninakumbuka kwenye mkoa wako huu,pia Wilaya ya Dodoma viongozi wametuagiza tusifanye mzaha juu ya Ugonjwa huu wa Corona lakini cha kushangaza kuna mwigizaji pia anafanya kazi na shirika la Utangazaji Ujeruman [DW]anaitwa Masanja Mkandamizaji amefanya mzaha juu ya ugonjwa huu akiwa Dodoma akithibitisha kuwa watu wa Dodoma hawajui maana ya ugonjwa huo akitumia neon la kiingereza [COVID-19]kwa hiyo tunamwomba mtu huyu kufIkia Jumatatu afike hapa Dodoma atuambie malengo yake yalikuwa ni nini hasa “amesema Katambi.
Hivi Karibuni Emmanuel Mgaya[Masanja Mkandamizaji] akiwa makao makao makuu ya nchi ya nchi wakati akifanya mahojiano na baadhi ya wananchi wakati akifanya kipindi chake kutoka DW aliwahoji wakazi wa Dodoma kuwa wanataka kuletewa COVID -19 ngapi ambapo bila ya kujua maana ya COVID 19 baadhi ya wananchi walisema wanahitaji waletewe COVID 19 elfu tano[5,000].
Ikumbukwe kuwa COVID -19 ni ufupisho wa maneno ya Kiingereza “Corona Viruse Disease ambapo virusi hivyo viligunduliwa mwaka 2019 .
Serikali Yaongeza Tija NIC Kwa Kukomesha Ubadhirifu
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, amesema hakuna ubadhirifu unaoendelea katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) baada ya Serikali kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kubadili uongozi wa Shirika hilo pamoja na kuimarisha mifumo yake ya ukusanyaji mapato.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Dkt. Kijaji, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ubungo. Mhe. Saed Kubenea, aliyetaka kujua ukweli kuhusu kuendelea kwa ubadhirifu katika Shirika la NIC na mpango wa Serikali wa kulisaidia shirika hilo kukabiliana na ushindani wa kibiashara.
Alisema kuwa hivi sasa Shirika hilo linatumia Mfumo wa Ukusanyaji Mapato ya Serikali (GePG) hatua iliyoimarisha mapato yake pamoja na kuanza kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kufanya malipo yake yote badala ya kutumia Hundi.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Shirika la NIC lilianza kutumia Mfumo wa Makusanyo ya Mapato ya Serikali kuanzia Novemba, 2019 na kuondoa ukusanyaji wa mapato kwa fedha taslimu pamoja na kuongeza udhibiti katika ulipaji wa madai ikiwemo kufanya ukaguzi maalum wa madai yote ya bima za maisha ili kujiridhisha kuhusu uhalali wake.
Alisema Matumizi ya Hundi (cheque) yamesitishwa kuanzia Desemba, 2019 katika malipo yake yote na kuanza kutumia mfumo wa malipo wa kielektroniki, ili kuongeza udhibiti wa uwezekano wa matumizi ya hundi za kughushi.
Dkt. Kijaji alisema pamoja na kufanya mabadiliko ya Uongozi wa Shirika hilo, pia imelipatia Shirika hilo wataalam katika nyanja za mifumo ya TEHAMA na mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu (e-Office) ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji
Alisema kuwa Serikali imechukua hatua ya kuliimarisha Shirika la NIC kitaalam kwa kuliondoa shirika hilo kutoka kwenye mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa na kuliwezesha kushiriki katika biashara ya bima kwa ushindani.
Katika kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za Shirika, ufungaji wa Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Kihasibu na Malipo katika Taasisi za Umma (MUSE) uko katika hatua za mwisho na kwamba mfumo huo utakapokamilika utaongeza udhibiti katika malipo yote yanayofanyika.
Alingeza kuwa Serikali inaendelea kupitia upya Mpango Mkakati wa NIC ili uendane na mahitaji halisi ya biashara ya ushindani, kuongeza uwekezaji katika mifumo ya TEHAMA ili kuwafikia wateja wengi zaidi, kuongeza ubora wa huduma na kulipa madai, kutoa gawio kubwa kwa Serikali na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya Taifa.
Mwisho.
MBARAWA AMTUMBUA AFISA KITENGO CHA MANUNUZI TANGA UWASA
WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Tanga iliyoanza leo kushoto ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly akizungumza wakati wa ziara hiyo kushoto ni Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo
WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa kulia akinawa mikono kabla ya kuingia kwenye ukumbi wa mamlaka ya maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga(Tanga Uwasa) wakati wa ziara yake
WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa kushoto akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hillywakati wa ziara yake mara baada ya kutembelea chanzo cha maji eneo la Horohoro wilayani Mkinga katikati ni Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo
WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa kulia akiwa na
Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly wakati akitoka kutembelea miradi wa maji eneo la Horohoro
WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa akitoka kutembelea miradi wa maji eneo la Horohoro
WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa amemuondoa kwenye nafasi yake aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Menejimenti ya Manunuzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira jijini Tanga(Tanga UWASA)Jamal Ngereja kwa kushindwa kufanya taratibu za manunuzi ya mabomba na vifaa katika miradi saba ya maji katika wilaya nne mkoani Tanga inayotekelezwa na Mamlaka hiyo.
Pia Profesa Mbarawa amefanya maamuzi hayo katika Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira za Moshi,Babati na Arusha nakuahidi kuendelea kufanya mabadiliko katika mamlaka nyingine za maji za Morogoro,Mwanza,
Tabora,Shinyanga na Kahama.
Profesa Mbarawa amefikia uamuzi huo baada ya Wizara ya Maji kutoa fedha takribani Sh.Milioni 700 katika miradi saba ya maji katika wilaya za Pangani,Mkinga,Muheza na Handeni kwa ajili ya ununuzi wa mabomba tangu mwezi Novemba mwaka jana lakini hakuna chochote kilichofanyika.
Pamoja na kufanya maamuzi hayo lakini pia aliwaonya wahasibu katika mamlaka za maji nchini nao wajiandae iwapo tu watafanya uzembe katika matumizi ya fedha za miradi ya maji .“Haiwezekani tumetoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maji katika mikoa ya Mbeya,Iringa na Tanga kiasi hicho hicho cha fedha lakini wenzenu wamefikia asilimia 70 ya utekelezaji lakini Tanga hakuna kilichofanyika,”alisema.
Aliongeza, “ kutokana na hilo nakuambia kabisa wewe(Afisa Manunuzi) nakuondoa hapa na hili nitafanya pia kwenye mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira za Morogoro,Mwanza,Kahama,Shinyanga na Tabora kama nilivyofanya Babati,Moshi na Arusha,”alisema.
Aidha, kwa upande wa miradi ya maji ambayo haiendi vizuri haswa ya mabwawa,Profesa Mbarawa aliahidi kuhakikisha anapeleka wataalamu kutoka wizarani kuchunguza miradi hiyo kila kitu ilikujua kama inakwenda na thamani ya fedha zilizotumika.
“Nitahakikisha kuwa ndani ya wiki kwenye miradi ya maji ambayo haiendi vizuri tunaleta wataalamu kuja kuchunguza kila item(kitu) kuanzia tofali,urefu wa kibanda,kina cha mabwawa kuona kama inakwenda na value for money (thamani ya fedha),kutokana tumegundua kuna watu kuanzia ngazi ya Halmashauri hadi Wizarani walihusika na hujuma za miradi ya maji kwa kupandisha gharama,”alisema.
Aliongeza, “Nataka nimiambie wakandarasi na watumishi wa Wizara ambao wamehusika na huo mchezo mchafu wajiandae safari hii hatuna mchezo”.
Katika hatua nyingine,Waziri Mbarawa amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/21,Serikali kupitia Wizara ya Maji imetenga fedha kwa ajili ya kutoa maji katika chanzo cha mto Zigi hadi katika mjiwa Horohoro wilayani Mkinga wenye urefu wa kilometa 40.
Amesema kuwa,mradi huo utavinufaisha vijiji zaidi ya 30 vitakavyopitiwa na mradi huo na kuahidi pia kuleta wataalamu wa Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi(DDCA) kuja kuchunguza na kufanya tathminikatika bwawa la maji la Horohoro.
WARATIBU WA TARURA WA MIKOA WATAKIWA KUFANYA UKAGUZI WA MARA KWA MARA KATIKA MADARAJA NA BARABARA
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff akiwa kwenye kikao kazi na Waratibu wa TARURA wa Mikoa, kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa TARURA Makao Makuu- Mtumba jijini Dodoma hivi karibuni.
Na Erick Mwanakulya
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amewataka Waratibu wote wa TARURA nchini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika barabara na madaraja ili kubaini maeneo yanayohitaji ukarabati na kuyafanyia kazi kabla ya kuleta madhara.
Mhandisi Seff ameyasema hayo, alipokutana na Waratibu wa TARURA wa Mikoa jijini Dodoma katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za TARURA Makao Makuu zilizopo Mtumba, ikiwa ni sehemu ya kikao kazi kilicholenga kutoa maelekezo na miongozo mbalimbali ya ufanyaji kazi ili kuwapatia wananchi huduma ya usafiri na usafirishaji.
Aidha, Mtendaji Mkuu amesisitiza kuwa, ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu unasaidia kupunguza gharama kwani uharibifu au uchakavu wa miundombinu ukibainika mapema ukarabati wake unaweza kufanyika katika hatua za awali kwa gharama nafuu na kwamba miundombinu inapoharibika moja kwa moja gharama inakuwa kubwa sana pale inapobidi kujengwa upya.
Pia, Mhandisi Seff amesisitiza juu ya uwekwaji wa alama za barabarani hasa katika maeneo maalumu kama madaraja na maeneo yaliyoharibika ili watumiaji wa barabara watambue vizuri maeneo hayo wakati wa kupita.
‘‘Natoa maelekezo juu ya uwekwaji wa alama za barabarani kwamba, hakikisheni mnaweka alama za kudumu maana sitamsikiliza yeyote atakayekuja na sababu kuwa kibao kimeibiwa wakati angeweza kuweka kibao cha kudumu hata kwa kutumia zege maana bila kuwa na alama hizo inaweza kuwa chanzo cha ajali”, amesisitiza Mhandisi Seff.
Ili kurahisisha usimamizi wa kazi kwa mikoa yote kiongozi huyo ameeleza kuwa, anaendelea kutoa magari kwa Waratibu wote wa TARURA na kisha atatoa magari kwa Mameneja wa TARURA wa Halmashauri ili kuhakikisha wanasimamia kazi na wananchi wanasafiri kwa urahisi.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) unaendelea kutekeleza majukumu yake katika Mji wa Serikali Mtumba baada ya kukamilisha ujenzi wa ofisi yake na kuhamia rasmi.
KUANZIA MEI 1 MARUFUKU KULA NYAMA YA PAKA NA MBWA
Shenzhen umekuwa mji wa kwanza wa Uchina kupiga marufuku ulaji wa kitoweo cha nyama za mbwa na paka.Hii inakuja baada ya mlipuko wa virusi vya corona kuhusishwa na ulaji wa wanyamapori, jambo lililowafanya maafisa wa Uchina kupiga marufuku biashara na ulaji wa wanyama hao.
Shenzhen ilichukua hatua zaidi, kwa kuweka marufuku ya ulaji wa mbwa na paka. Sheria hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Mei,2020.
Mbwa milioni thelathini huuawa kote katika bara la Asia kwa ajili ya nyama, linasema shirika la kutetea haki za wanyama, Humane Society International (HSI).
Hata hivyo, ulaji wa nyama ya mbwa nchini Uchina si wa kawaida sana-wengi wa Wachina hawajawahi kufanya hivyo na wanasema hawataki kufanya hivyo.
"Mbwa na paka kama wanyama wa nyumbani wameweza kuwa na uhusiano wa karibuu sana na binadamu kuliko wanyama wengine wote, na kupiga marufuku ulaji wa nyama za mbwa na paka na wanyama wengine wa nyumbani ni jambo la kawida katika mataifa yaliyoendelea na kama miji ya Hong Kong na Taiwan," ilisema serikali ya jiji la Shenzhen kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Reuters.
"Marufuku hii pia inaitika mahitaji na moyo wa kistaarabu wa ubinadamu.''
Shirika HSI limepongeza hatua hiyo.
"Haya kusema ukweli ni mafanikio makubwa katika juhudi za kumaliza ukatili huu ambao unakadiriwa kuwauwa mbwa milioni 10 na paka milioni 4 nchini Uchina kila mwaka," alisema Dkt. Peter Li, mtaalamu wa sera katika kampuni ya Uchina ya HSI.
Hata hivyo wakati huo huo wakati hukumu hii inatolewa, Uchina imeidhinisha matumizi ya nyongo ya dubu katika kuwatibu wagonjwa wa coronavirus.
Nyongo ya dubu - ambayo ni kimiminika kinachosaidia kusaga chakula huchukuliwa kutoka kwa dubu ambao ni hai - imekua ikitumika kwa muda mrefu nchini Uchina kama dawa ya kienyeji.
Nyongo hiyo ambayo ina tindikali ya ursodeoxycholic , hutumiwa kuyeyusha mawe yanayojitengeneza katika kibofu cha mkojo na kutibu ugonjwa wa maini . Lakini hakuna uthibitisho kuwa ina ufanisi dhidi coronavirus na mchakato wa kuitoa huwasababishia machungu sana wanyama hao.
Brian Daly, msemaji wa wakfu wa Animals Asia Foundation, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa: "Hatupaswi kuwa tunategemea bidhaa za wanyama kama nyongo ya dubu kama suluhu ya kukabiliana na virusi vinavyoua ambavyo vinaonekana kuwa asili yake ni wanyamapori."
Soko la wanyamapori
Picha ya maktaba ya soko la nyama Uchina.
Picha ya maktaba ya soko la nyama Uchina.Mwezi Februari, mamlaka za Uchina zilipiga marufuku biashara na ulaji wa wanyama wa pori.
Hatua hiyo ilichukulia baada ya kubainika kuwa soko la Wuhan linalouza wanyama wa porini na nyama za wanyamapori huenda kilikua ndio kitovu cha mlipuko wa virusi vipya vya corona, na kutoa njia ya virusi kusafiri kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu.
Taarifa hizi ziliifanya serikali ya Uchina kufunga biashara hizo na masoko yanayouza bidhaa za aina hiyo.
Kwa sasa kunakaribu wagonjwa milioni moja walioothibitishwa kuwa na virusi vya corona kote duniani, na zaidi ya vifo 47,000, kwa mujibu wa hesabu za Chuo kikuu cha Johns Hopkins cha Marekani.
Nchini Uchina pekee, kuna wagonjwa 81,589 na vifo 3,318.
Wanasayansi na watafiti bado hawajaweza kutambua chanzo hasa cha mlipuko huo wa virusi na kwa namna gani viliwafikia wanadamu.
Chanzo - BBC
UPDATES: Mgonjwa Mwingine Wa Corona Apona Nchini Tanzania
"Mungu ni mwema. Na leo pia hatuna case mpya za COVID19. Mgonjwa wa Kagera (Ngara) amepona. Sasa jumla ya waliopona ni 3. Mgonjwa aliebaki wa Arusha vipimo vyake siku ya 9 leo ni Negative. Tutampima siku ya 14 ili kujiridhisha kama amepona. Wengine 15 waliobaki wanaendelea vzr"-UMMY MWALIMY
Mungu ni mwema. Na leo pia hatuna case mpya za COVID19. Mgonjwa wa Kagera (Ngara) amepona. Sasa jumla ya waliopona ni 3. Mgonjwa aliebaki wa Arusha vipimo vyake siku ya 9 leo ni Negative. Tutampima siku ya 14 ili kujiridhisha kama amepona. Wengine 15 waliobaki wanaendelea vzr pic.twitter.com/DcZVFTKrt1— Ummy Mwalimu, MP (@umwalimu) April 3, 2020
RAIS PUTIN WA URUSI AAAMURU WATU WA NCHI HIYO KUTOKWENDA KAZINI NA KUBAKI MAJUMBANI KUKABILIANA NA CORONA

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameamuru raia wa nchi hiyo kutokwenda kazini na kusalia nyumbani hadi mwishoni mwa mwezi Aprili kama sehemu ya juhudi za kuzuia kusambaa kwa virusi hatari vya corona.
Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Putin amesema anarefusha sera ya kutofanya kazi kwa muda wa wiki tatu zaidi na wafanyakazi wote wanapaswa kulipwa mishahara ndani ya kipindi hicho.
Putin amesema baadhi ya viwanda vinavyozalisha bidhaa muhimu vitaendelea kufanya kazi na maduka ya vyakula na dawa yanaruhusiwa kufunguliwa.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa mkakati wa Urusi wa kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona umefanikiwa lakini ameonya kuwa idadi ya watu walio na maambukizi ya virusi hivyo itaendelea kuongezeka.
Hadi kufikia Alhamisi Urusi imerikodi visa 3,548 vya wagonjwa wa COVID-19 pamoja na vifo vya watu 30




























