Wednesday, 15 January 2020
WADAU WA UTALII WATAKIWA KUBORESHA MAZINGIRA ILI YAWE RAFIKI KWA WATU WENYE ULEMAVU
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa akizungumza mara baada ya kutembelea vivutio vya Magofu ya Kale yaliyopo mji Mkongwe, Bagamoyo -Pwani huku akiwa ameongozana na wabunge wenzake wenye ulemavu ziara iliyokuwa imeratibiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki Bi. Caroline Malundo akiwakaribisha wabunge wenye ulemavu mara baada ya kutembelea katika eneo la Mji Mkongwe, Bagamoyo ambapo kuna vivutio vya magofu ya kale. Wabunge hao walikuwa kwenye ziara iliyokuwa imeratibiwa na TFS. Wengine katika picha ni wafanyakazi wa TFS.
Wabunge wenye Ulemavu wakipatiwa maelezo ya historia ya Mji Mkongwe mara baada ya kuwasili kujionea vivutio vya eneo hilo.
Katibu wa Chama cha Wabunge wenye Ulemavu Mhe. Amina Mollel akitoa machache.
Mbunge wa Ulyankulu, Tabora Mhe. John Kadutu (kulia) akizungumza neno mara baada ya kukaribishwa na na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mhe. Amina Mollel wakati wa ziara yao ya utalii mjini Bagamoyo - Pwani.
Wafanyakazi wa TFS wakifuatilia.
Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wenye Ulemavu Mhe. Riziki Lulida ambaye ni mmoja ya mabalozi wa Utalii akitoa shukrani zake kwa TFS kwa namna ilivyoweza kuwapokea na kuwakarimu wakati wa ziara yao ya utalii mjini Bagamoyo - Pwani.
Muongoza watalii Bw. Cathbert akitoa maelezo kwa wabunge waliofika kutembelea vivutio vya mji mkongwe Bagamoyo - Pwani.
Muongoza watalii Bw. Cathbert akitoa maelezo juu ya vivutio vya mji mkongwe Bagamoyo - Pwani.
Moja ya kibao.
Boma ya Wajerumani iliyojengwa mwaka 1897 katika mji Mkongwe Bagamoyo - Pwani.
Boti zikisubiri mzigo kuelekea Zanzibar kutokea mji wa Bagamoyo - Pwani.
Wavuvi wakielekea kuvua samaki katika Bahari ya Hindi.Shughuli za kuandaa chombo zikiendelea.
Wachuuzi wa vinyago wakionyesha biashara zao.
Mbunge wa Ulyankulu, Tabora Mhe. John Kadutu (kushoto) na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mhe. Amina Mollel akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili katika eneo la Magofu ya Kale yaliyopo mji mkongwe, Bagamoyo- Pwani.
Meneja wa Wakala wa Huduma za Misiti Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki Bi. Caroline Malundo akizungumza na wanahabari.
Bango linaloelezea kwa ufupi mji wa Kaole, Bagamoyo - Pwani.
Wageni kutoka mataifa mbali mbali wakipata maelezo mara baada ya kutembelea mji wa Kaole, Bagamoyo - Pwani.Meneja wa Wakala wa Huduma za Misiti Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki Bi. Caroline Malundo (kushoto) akizungumza na wageni aliwakuta eneo la Kaole Bagamoyo-Pwani.
Muongoza watalii akitoa maelezo kwa wageni.Moja ya msikiti ambao ni kivutio katika mji wa Kaole, Bagamoyo - Pwani.
Makaburi.
Moja ya kaburi lenye mnara refu kuliko yote.
Mbunge wa Ulyankulu, Tabora Mhe. John Kadutu akinawa maji ya baraka katika kisima kilichopo mji wa Kaole ambapo kisima hicho hutoa maji kwa mwaka mzima bila kukata. Inasemakana maji hayo huondoa mikosi na kuwapatia watu baraka.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mhe. Amina Mollel (mwenye kilemba) akinawa maji ya baraka.
Wabunge wenye ulemavu wakiongozwa na Naibu Waziri Stella Ikupa wakipita kujionea vivutio katika mji wa Kaole, Bagamoyo - Pwani.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mhe. Amina Mollel akifanya sala katika makaburi ya Kaole, Bagamoyo - Pwani.
Moja ya Bango lililopo katika eneo la Bandari ya Zamani iliyopo Kaole, Bagamoyo - Pwani.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) akiwa katika kaburi la Sharifu, kaburi hili hutumika katika matambiko mbali mbali ikiwemo kutoa mikosi.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/Michuzi TV.
Chama cha Wabunge wenye ulemavu kimewapongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuendelea kusimamia vyema vivutio vya Mji Mkongwe na Kaole vilivyopo Bagamoyo huku kikiwataka wadau wa Utalii kutengeneza mazingira rafiki yatakayowawezesha watu wenye walemavu kufika kirahisi kutembelea hifadhi hizo.
Hayo yamezungumzwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa mara baada ya kutembelea katika vivutio hivyo huku akiwa ameongozana na wabunge wenzake wenye ulemavu ziara iliyokuwa imeratibiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Amesema kuwa ni vyema Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa utalii wanaosimamia hifadhi za Taifa na vitutio vya asilia akiwemo TFS, TAWA na TANAPA ni vyema kutengeneza miundombinu rafiki itakayoweza kuwasaidia watu wenye ulemavu nao kutembelea hifadhi hasa katika upande mambo ya kale.
"Napenda nitoe pongezi zangu kwa Kamishna Mhifadhi Mkuu wa TFS Prof. Dos Santos Silayo na timu yake kwa ujumla kwa kuweza kuwa na vijana mahili wanaojua kutoa elimu sahihi kwa wageni wanaotembelea katika hifadhi zote wanazosomamia ila niwaombe kuendelee kusimamia vyema huku mkitengeneza mazingira rafiki ya miundombinu ili kutuwezesha tufike kwa wingi kutembelea mambo ya kale," amesema Naibu Waziri Ikupa.
Ameongeza kuwa kwa sasa serikali haipo nyuma kuendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa hoteli, watoa huduma kwa jamii kuwapa kipaumbele walemavu ili nao waweze kujikwamua na wasonge mbele kimaendeleo kuliko kubaki wakiwa omba omba.
"Serikali ya Awamu ya Tano haipo nyuma katika kuwashika mkono walemavu ili waweze kusonga mbele kimaendeleo hivyo niwaombe wenzangu wenye ulemavu kuacha kulemaa na kubaki wakiwa omba omba bali wafanye kazi kwa bidii ili waweze kusonga mbele kujenga uchumi wa Taifa," Amesema Naibu Waziri Ikupa.
Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wenye Ulemavu Mhe. Riziki Lulida ambaye ni mmoja ya mabalozi wa Utalii ameishukuru TFS kwa kuweza kuwapa nafasi ya kutembelea vivutio hivyo huku ikiwaomba kuwasaidia vijana kuwawezesha kutumia misitu wanayoisimamia kuzalisha zao la asali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
"Niwapongeze TFS kwa kutupa nafasi sisi wabunge wenye ulemavu kutembelea vivutio vya mambo ya kale ila endeleeni kuzalisha ajira kwa vijana kwa kuweza kupatia maeneo ili waweze kuzalisha zao la asali, unapowaweka wataendelea kutunza mazingira huku wakijikwamua kiuchumi," amesema Mhe. Lulida.
Amesema kwa sasa Wizara na Maliasili na Utalii ni vyema kuvisimamia vyema vivutio maana Utalii ndiyo zao pekee linaloleta pesa kwa nchi mbali na hapo zamani kilimo kilikuwa kinaongoza.
Kwa upande wake Meneja wa TFS Kanda ya Mashariki Bi. Caroline Malundo amewaomba Watanzania kujitokeza kutembelea vivutio vya misitu asili na mambo ya kale ili kuweza kujipatia elimu na historia ya kale ya mababu zetu.
Amesema kuwa katika jitihada za kukuza utalii na kukuza pato la Taifa, TFS kwasasa imeongezewa vivutio mbali na Misitu asilia pia imepewa dhamana ya kusimamia Magofu ya Kale yaliyopo mji Mkongwe na Kaole, Bagamoyo - Pwani, Michoro ya Miamba, Kolo- Kondoa, Magofu ya Tongoni - Tanga.
Aidha TFS imejipanga kusimamia na kuendeleza vyema vivutio vya mambo ya kale na kuweza kuvipa kipaumbele zaidi ili Watanzania wasiweze kupoteza historia ya mababu zetu.
Tuesday, 14 January 2020
MUONEKANO UJENZI WA JENGO LA ABIRIA MWANZA AIRPORT ULIPOFIKIA MPAKA SASA
Mwonekano wa sehemu ya msingi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Mwanza lililoanza kujengwa Septemba 2019.
Mbunifu Majengo kutoka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Chagu Ng'oma akitoa ufafanuzi kuhusu hatua ulipofikia ujenzi wa jengo hilo.
Sehemu ya mwonekano wa jengo hilo linaloendelea kujengwa.
Baada ya hatua hii ya msingi kukamilika, itafuata hatua ya kunyanyua vyuma ili kupata mwonekano hali wa jengo kama picha inavyoonekana hapo chini.
Mwonekano wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Mwanza baada ya ujenzi kukamilika. Ujenzi huu utagharimu shilingi bilioni 12, Halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela zikichangia Bilioni nne na fedha nyingine ikitolewa na Serikali Kuu. Rais Dkt.John Magufuli aliagiza kujekwa kwa jengo hili wakati akizindua miradi ya afya Julai 15, 2019 katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.
Tazama Video hapa chini
Pemba: Maalim Seif Na Salim Bimani Watuhumiwa Kufanya Mkutano Bila Kibali
Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Salim Bimani wametuhumiwa kufanya Mkutano bila kibali mnamo Desemba 2019, huko Micheweni Zanzibar
Hata hivyo, Viongozi hao wameachiwa kwa dhamana na Chama chao kupitia Mtandao wa Twitter kimedai walifanya Mkutano wa ndani usiohitaji kibali
Viongozi hao waliripoti Polisi asubuhi ya leo kuitikia wito wa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Mkoa wa Kaskazini Pemba
UPDATE: Mshauri Mkuu wa @ACTwazalendo @SeifSharifHamad na M/kiti wa Itikadi na Uenezi @salimbimani2 wameshutumiwa kufanya Mkutano bila kibali,Dec 9, 2019 Micheweni Z'bar.— ACT Wazalendo (@ACTwazalendo) January 14, 2020
Hata hivyo, walifanya Mkutano wa ndani usiohitaji kibali. Wameachiwa kwa dhamana.@SuphianJuma,
Afisa Habari. pic.twitter.com/9kf4L140vD
Uturuki Yamuonya jenerali Haftar dhidi ya mashambulizi zaidi
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoÄŸan amesema nchi hiyo haitasita kumpa fundisho Kamanda wa Wapiganaji wa Mashariki mwa Libya, Jenerali Khalifa Haftar iwapo vikosi vyake vitaendelea kuishambulia serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli.
Urusi na Uturuki zilikuwa zinajaribu kupata mkataba wa kudumu wa kusitisha mapigano ambapo mbabe huyo wa kivita wa Libya alitakiwa kutia saini ambapo aliomba muda hadi leo Jumanne kufikiria suala hilo lakini baadaye imefahamika kuwa ameondoka mjini Moscow bila kutia saini makubaliano hayo.
Mazungumzo ya jana Jumatatu yalitarajiwa kuweka rasmi mkataba wa muda wa kusitisha mashambulizi ulioafikiwa siku ya Jumapili lakini mkataba huo haukutekelezwa kikamilifu na kuna ripoti ya mapigano kuendelea nchini Libya.
Taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta lina serikali mbili pinzani. Serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayoongozwa na al-Serraj mjini Tripoli na nyingine yenye makao yake katika mji wa Tobruk, Mashariki mwa Libya inayoongozwa na Haftar.
Urusi na Uturuki zilikuwa zinajaribu kupata mkataba wa kudumu wa kusitisha mapigano ambapo mbabe huyo wa kivita wa Libya alitakiwa kutia saini ambapo aliomba muda hadi leo Jumanne kufikiria suala hilo lakini baadaye imefahamika kuwa ameondoka mjini Moscow bila kutia saini makubaliano hayo.
Mazungumzo ya jana Jumatatu yalitarajiwa kuweka rasmi mkataba wa muda wa kusitisha mashambulizi ulioafikiwa siku ya Jumapili lakini mkataba huo haukutekelezwa kikamilifu na kuna ripoti ya mapigano kuendelea nchini Libya.
Taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta lina serikali mbili pinzani. Serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayoongozwa na al-Serraj mjini Tripoli na nyingine yenye makao yake katika mji wa Tobruk, Mashariki mwa Libya inayoongozwa na Haftar.
Iran yawakamata walioidungua kimakosa ndege ya Ukraine
Msemaji wa idara ya sheria ya Iran Gholamhossein Esmaili amesema, Iran imekamata baadhi ya watu kutokana na kuhusika kwao katika ajali ya ndege ya Ukraine iliyosababisha vifo vya watu 176 waliokuwa ndani ya ndege hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Bw. Esmaili amesema mpaka sasa uchunguzi kuhusu wahusika umefanyika, na wataalamu wa sheria wanajitahidi kuhoji, kuchunguza na kukusanya taarifa.
Amesema sanduku jeusi limepelekwa Ufaransa, na wataalamu wa Iran na Ukraine watashiriki kwenye kazi ya kusoma data.
Jumamosi wiki iliyopita, jeshi la Iran lilisema, limeangusha kwa makosa ndege ya abiria ya Ukraine, na kosa hilo la kibinadamu linapaswa kulaumiwa.
Waliovunja Na Kuiba Pombe Baa Kahama Wapandishwa Kizimbani
Wakazi wawili wa Mtaa wa Malunga wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Meshaki Joakimu (31) na Godfrey Luka (32) wamefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Kahama kwa tuhuma ya kuvunja baa(grocery) na kuiba fedha, na thamani mbalimbali za ndani pamoja na vinjwaji Mali ya Eliasi Mwasenga.
Akisoma Shauri hilo Januari 14 mwaka huu mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Felix Mbisse mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidi wa Mahakama hiyo Evodia Kyaruzi amedai watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Oktoba 8 mwaka 2019 usiku majira ya saa nane usiku.
Alisema kuwa baada ya kuvunja baa hiyo waliiba Televisheni mbili,bia kreti 5,konyagi chupa 10,K vant chupa 10,flash disck mmoja vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya shilingi milioni mmoja laki sita na elfu ishirini mali ya Eliasi Mwasenga.
Katika shauri hilo la jinai namba 10 la mwaka huu Mbisse alisema kuwa wawili hao kwa pamoja wanatuhumiwa kutenda makosa mawili ambapo kosa la kwanza ni la kuvunja nyumba kinyume na kifungu 296 cha kanuni ya adhabu sura 16 marejeo ya mwaka 2002.
Shitaka la pili wote kwa pamoja wanatuhumiwa kuiba mali hizo kinyume na kifungu cha 258 (1) na 265 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.
Washitakiwa wote kwa pamoja walikana kutenda makosa hayo na Shauri hilo limeahirishwa hadi januari 24 mwaka huu na wameachiliwa huru kwa dhamana baada ya kutimza mashariti yake ambapo walitakiwa kuwa na wadhamini wawili wawili ambao walisaini bondi ya shilingi milioni mmmoja kila mmoja.
Mwisho.
Katibu Mkuu Hazina Ahimiza Watumishi Wa Tra Kuongeza Bidii Ukusanyaji Mapato
Veronica Kazimoto na Rachel Mkundai
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, amewahimiza watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, na kwa kuzingata misingi wa Sheria za kodi ili kuhakikisha kuwa TRA inaendelea kuvunja rekodi ya makusanyo ya mapato kama ilivyokuwa katika mwezi Septemba na Desemba, 2019.
Pia, amewapongeza watumishi wote wa Mamlaka hiyo kwa kujituma na kupelekea Serikali kukusanya mapato kiasi cha Sh. trilioni 9.341 sawa na ufanisi wa asilimia 47.67 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 19.595 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019/2020 yaani kuanzia Julai hadi Desemba 2019.
Akizungumza wakati wa mkutano wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi wa nusu mwaka 2019/20 wa Mamlaka hiyo uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha, Bw. James alieleza kuwa, mapato makubwa yanayotegemewa na Serikali ni makusanyo ya kodi ambapo aliwaasa watumishi wa TRA kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuongeza mapato na hatimaye Serikali iweze kutekeleza mipango yake iliyojipangia ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
“Ukiangalia mchanganuo wa makusanyo yote ya Serikali, sehemu kubwa sana ni kodi inayokusanywa na TRA. Kwa msingi huu, TRA inapofanikiwa kukusanya kodi kwa ufanisi mkubwa ndiyo mafanikio ya Serikali katika kutekeleza bajeti inayokuwa imepangwa kwa kipindi hicho,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Aidha, aliwashukuru wananchi na walipakodi wote kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati ambapo makusanyo ya mwezi Septemba na Desemba, 2019 ni ishara kwamba, walipakodi kwa ujumla wao, wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuongeza mapato ya ndani na pia wameendelea kutambua umuhimu wa kulipa kodi baada ya kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini inayofanywa na Serikali yao.
“Tunawashukuru sana walipakodi wa nchi hii kwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria wa kuisadia Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania kukusanya kodi hiyo kubwa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo. Kitendo hiki kiendelee na ikiwezekana iwe zaidi ya hapo”, alieleza Bw. James.
Akizungumzia suala la mifumo ya kieletroniki ya ukusanyaji mapato, ukiwemo mfumo wa mnada wa forodha kwa njia ya mtandao, Katibu Mkuu huyo, ameipongeza TRA kwa kuendelea kuboresha mifumo hiyo ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya Serikali.
“Mfumo wa mnada wa forodha kwa njia ya mtandao ni mfumo mmojawapo kati ya mifumo mingi inayotumiwa na TRA katika kukusanya mapato. Mfumo huu, ambao umejengwa na Watalaam wetu wa TRA, umeonesha mafanikio makubwa kwa sababu unashirikisha watu wengi na kuleta ushindani wa haki kwa wote.
“Ni matarajio yetu kuwa, Serikali itapata mapato yake stahiki kutokana na kuuzwa kwa bidhaa zilizokaa muda mrefu bandarini tofauti na matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na ni matumaini yetu kwamba, kuuzwa kwa wakati kwa bidhaa hizo kupitia mfumo huu, kutapunguza mrundikano wa bidhaa bandari na hivyo kuongeza ufanisi wa bandari zetu na vituo vingine vya forodha”, alieleza.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James amewaagiza viongozi wa TRA kufanya maboresho ya mifumo ndani ya Mamlaka hiyo mara moja pale watakapobaini mapungufu yoyote ambayo yanaweza kukwamisha utendaji kazi wa mfumo husika.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Edwin Mhede, alisema kwamba, mkutano huo wa mapitio na tathmini ya nusu mwaka ulilenga kufanya maboresho katika utendaji kazi ili kuhakikisha kuwa malengo waliyopangiwa na Serikali yanafikiwa.
Dkt. Mhede aliongeza kuwa, TRA imepewa agizo na Serikali la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 19.5 katika mwaka huu wa fedha 2019/20 ambapo pamoja na kufanya vizuri katika miezi ya Septemba na Desemba, 2019, alikiri kuwa bado Mamlaka hiyo haijafikia malengo ya makusanyo kwa asilimia 100. Hivyo, mkutano huo ulilenga kufanya marejeo na maboresho ya mikakati ya utendaji kazi itakayowezesha kufikia malengo hayo kwa asilimia 100.
“Kupitia Sheria ya Bajeti, SURA 439, TRA tumepewa agizo na Serikali la kukusanya mapato kiasi cha sh. trilioni 19.595 hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2020 na wakati tukitekeleza robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha 2019/2020, hatukufanikiwa kufikisha asilimia 100 ya makusanyo ya robo hizo. Hii ndiyo moja ya sababu tumeona tukutane ili tubaini maeneo yenye mapungufu na kisha tufanye marejeo shirikishi ili tujisahihishe na kuweka mikakati itakayotuwezesha kufikia lengo”, alisema Dkt. Mhede.
Mkutano wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi wa nusu mwaka 2019/20 wa TRA ulihudhuriwa na jumla ya washiriki 361 ukihusisha Menejimenti nzima ya Mamlaka, Mameneja wote wa Mikoa na Wilaya kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo.
Washiriki wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na wawakilishi kutoka baadhi ya Asasi za Serikali kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Ofisi ya Rais - Tume ya Utumishi wa Umma, Ofisi ya Mganga Mkuu - Mkoa wa Arusha, na Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAeSA) iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira) ambapo kwa siku ya kwanza wawakilishi wa Asasi hizo walitoa maada kuhusu masuala mbalimbali ya kuisaidia TRA kuongeza makusanyo ya Serikali.
MWISHO.
Viongozi Wa AMCOS Waliotafuna Fedha Za Wakulima Shinyanga Wakubali Yaishe
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga imeokoa Shilingi milioni 30, laki tano na elfu tatu miasita na hamsini kutoka kwa Viongozi wa Vyama vya ushirika (AMCOS) waliofanya ubadhirifu wa Fedha za Wakulima wa Pamba msimu wa Mwaka 2018/2019.
Akizungumza na waandishi wa habari januari 14 mwaka huu Kaimu Mkuu wa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa alisema kuwa ofisi yake ilifuatilia kwa kina madeni ya Wakulima wa Pamba wanaodai fedha zao kutokana na pamba waliyouza kupitia AMCOS na kubaini kuwepo ubadhilifu wa fedha za wakulima.
Alisema kuwa Baada ya uchunguzi TAKUKURU ilibaini kuwa AMCOS saba za Lugana, Mwakipoya, Ng'washinong'hela, Nyenze, Kalitu, Kweli Balimi na Ibadakuli ndizo zinadaiwa fedha na wakulima wa pamba shilingi 109,497,130 licha kuwa fedha hizo zimekwisha kutolewa na Kampuni za Ununuzi.
“TAKUKURU ilibaini kuwa mpaka kufikia mwezi Desemba 2019 makampuni yaliyonunua pamba mkoani Shinyanga yalikuwa hayadaiwi Fedha za Wakulima bali walikuwa yanadaiwa ushuru wa AMCOS jumla ya Shilingi 890,105,580 alisema Mussa.
Amefafanua kuwa kuwa baada ya kubaini ubadhirifu huo Takukuru iliweza kuwakamata baadhi ya Viongozi wa AMCOS waliofanya ubadhilifu wa fedha za Wakulima na waliweza kurejesha kiasi cha Shilingi 30,503,650 fedha ambazo zinatarajiwa kugaiwa kwa Wakulima hivi Karibuni.
“ Viongozi wa AMCOS ya Kweli Balimi ya Wilaya ya Shinyanga ambao walirejesha Fedha walizokuwa wanadaiwa kiasi cha Shilingi 6,362,400 walikuwa wamezifanyia ubadhilifu na tayari fedha hizo zimeshatolewa kwa Wakulima” alisema Mussa.
Aliwataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU ili Kuhakikisha wanatokomeza rushwa katika mkoa wa Shinyanga.
Mwisho.
























