Tuesday, 7 January 2020

Kesi Ya Kutekwa Mfanyabiashara Mohammed Dewji Yapigwa Kalenda hadi January 21

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imepiga kalenda kesi ya kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu kama MO inayomkabili dereva wa taksi Mousa Twaleb na wenzake wanne ambao bado hawajakamatwa na kufikishwa mahakamani hapo.

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo kwenda likizo.

Wakili wa Serikali, Faraji Nguka, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Chaungu alisema kesi hiyo itatajwa Januari 21, mwaka huu na mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu.

Watuhumiwa wengine ambao upande wa mashtaka inawatafuta ni raia wanne wa Msumbiji na mmoja wa Afrika Kusini, wanaodaiwa kumteka bilionea huyo.


Share:

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Ndugulile Ataka Taarifa Utoaji Wa Dawa Hospitali Ya Rufaa Iringa.

Na Mwandishi Wetu Iringa
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amemuagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Atupele Mwandiga kuhakikisha anapata taarifa ya utoaji wa dawa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa.

Agizo hilo limekuja mara baada ya ziara ya yake mkoani humo alipotembelea hospitali hiyo kujionea utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kushuhudia mmoja wa mama aliyejifungua Hospitalini hapo kupewa dawa mara moja badala ya mara tatu kama iilivyoandikwa na Daktari.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa amekasirishwa na utendaji kazi wa manesi katika wodi ya Mama na Mtoto kwa kutozingatia utoaji huduma hasa kuhakikisha wazazi na watoto wanapewa dawa kwa wakati zinazotakiwa na kwa idadi sahihi.

Ameongeza kuwa lengo la mgonjwa kupewa huduma ni kuhakikisha anapona na sio kufanya aendelee kupata tabu na shida hivyo Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza fedha nyingi katika kuhakikisha Sekta ya Afya inaboreshwa nchini.

"Haiwezekani mgonjwa kanunua dawa zake kwa fedha zake lakini bado hata hamzingatii kumpatia dawa mnategemea ataponaje” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ndugulile ameutaka uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kuhakikisha wanaratibu utoaji wa huduma hospitalini hapo ili kuepukana na malalamiko ya wagonjwa na kupoteza imani ya wananchi kwa Hospitali hiyo.

"Tukiendelea hivi tutaondoa imani kwa wananchi wetu katika utoaji wa huduma za afya sisi tunatakiwa kutoa huduma kwa wananchi na sio kuwapa kero wananchi" alisema Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Atupele Mwandiga amemuahikikishia Naibu Waziri Dkt. Ndugulile kusimamia utoaji huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na kusimamia vilivyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayostahili.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya tano imetoa kiasi cha Billioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya na maboresho katika Zahanati na vituo vya Afya mkoani humo katika kuhakikisha inaboresha Sekta ya Afya hivyo watasimamia Sekta hiyo kikamilifu.

"Mhe. Naibu Waziri tutahakikisha hatutopoteza imani ya wananchi katika utoaji huduma za afya na tutatendea haki rasimali fedha tulizopewa na Serikali katika kuboresha Sekta ya Afya Mkoani kwetu" alisema Dkt. Atupele

Wakati huo huo Dkt. Ndugulile ametembelea na kujionea utendaji kazi utoaji wa huduma kwa wananchi katika Ofisi ya Bima ya Afya (NHIF), Kampeni ya masuala ya Lishe, Kiwanda cha Ruaha Milling na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile yuko katika ziara ya siku mbili mkoani Iringa kukuagua shughuli za Afya na Maendeleo ya Jamii mkoani humo.


Share:

Mazungumzo kati ya DPP na Kigogo TAKUKURU Yakwama

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania, Kulthum Mansoor amedai wameshindwa kufikia muafaka wa makubaliano baina yake na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Wakili wa utetezi Elia Mwingira, alitoa madai hayo jana kwamba awali walimwandikia DPP barua ya kuomba kukiri makosa yanayomkabili mshtakiwa, lakini mazungumzo yamevunjika.

Alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Isaya.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika.

Wakili wa utetezi Mwingira, alidai kuwa kwa kuwa mazungumzo na DPP yamevunjika upande wa Jamhuri uharakishe upelelezi.

Wakili Wankyo alidai wataelekeza wapelelezi kuhakikisha wanakamilisha upelelezi katika maeneo yaliyobaki.

Hakimu Isaya alisema mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu na kesi hiyo itatajwa Januari 20, mwaka huu.

Mansoor anakabiliwa na mashtaka manane ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh. bilioni 1.477.


Share:

Mhasibu wa Wizara ya Afya Kortini Kwa Mashitaka 280

Mhasibu wa Wizara ya Afya, Luis Lyimo (54) na Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Christian Social Services Commission, Peter Maduki (61) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 280 yakiwemo 150 ya kughushi na moja la kutakatisha fedha.

Mawakili wa Serikali , Zakaria Ndaskoi na Genes Tesha wamewasomea mashtaka washtakiwa hao jana  Jumatatu Januari 6, 2020 huku wakipokezana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.
 
Wakili Ndaskoi amedai washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya mwaka 2017 na mwaka 2019 ndani ya Jiji la Dar es Salaam

Alidai washtakiwa hao kwa nafasi zao wakiwa na nia ovu walighushi hundi mbalimbali zenye thamani ya mamilioni ya fedha na kusaini kwa jina la Upendo Mwingira bila ridhaa yake huku wakijaribu kuonyesha mshtakiwa, Luis Lymo alikuwa akilipwa na taasisi ya Christian Social Services Commission Fedha hizo kama kamisheni wakati si kweli.

Katika mashtaka ya kuwasilisha nyaraka za uongo washtakiwa hao wanadaiwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali walizozighushi katika benki ya Standard Chartered.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongeza chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikilizwa kesi ya uhujumu uchumi.

Upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika, washtakiwa walipelekwa rumande na kesi imeahirishwa mpaka Januari 20 2020


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne January 7





















Share:

Monday, 6 January 2020

Raia Watatu wa Marekani Wauawa Kenya....Pentagon Yasema Tukio Hilo Halina Uhusiano na Mzozo wa Iran

Wafanyakazi watatu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani wameuawa kwenye shambulizi la kigaidi katika kambi ya kijeshi ya Manda ilioko mjini Lamu 

 Wafanyakazi 2 pamoja na makandarasi wawili wameripotiwa kuachwa na majeraha mabaya kufuatia shambulizi hilo la Jumapili, Januari 5. 

" Wakati wa shambulizi hilo la kigaidi katika kambi ya kijeshi ya Manda, wafanyakazi wa wizara ya ulinzi ya Marekani waliuawa, huku wengine wawili wakijeruhiwa vibaya ila hawako katika hali mbaya,"Sehemu ya taarifa ya ubalozi wa Marekani ilisoma. 
 
Aidha, Marekani imeapa kupambana vilivyo na magaidi wa al- Shabaab hasa wale waliotekeleza shambulizi la Manda. 
Hata hivyo, imesema tukio hilo halina uhusiano wowote na mzozo unaoendelea kati yake na Iran 


Share:

Kivuko kipya MV.Ilemela chashushwa kwenye maji Ziwa Victoria Mwanza

NA ALFRED MGWENO (TEMESA MWANZA)
Wakazi wa Ilemela mkoa wa Mwanza leo wameshuhudia kwa mara ya kwanza kivuko kipya cha Kayenze Bezi, MV.Ilemela ambacho kimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kikishushwa kwenye maji baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Tukio hilo limefanyika katika yadi ya Songoro iliyopo Wilaya ya Ilemela ambapo mgeni rasmi alikua Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe. Atashasta J. Nditiye (MB)

Akizungumza katika tukio hilo Mhe. Nditiye alimshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya awamu ya tano kwa kuendelea kutimiza ahadi ya miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

‘’Hadi sasa Mheshimiwa Rais tayari ameshatoa fedha zote kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 9,953,916,200 iliyokuwa imepangwa kwenye bajeti ya miradi ya maendeleo ya vivuko kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020’’, alisema Mhe. Naibu Waziri ambapo aliongeza kuwa kivuko cha MV.Ilemela kitakapoanza kutoa huduma kitaondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi kati ya Kayenze na kisiwa cha Bezi.

‘’Kivuko hiki kitakapoanza kutoa huduma ni dhahiri kuwa kitaondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi kati ya Kayenze na kisiwa cha Bezi hivyo kitainua maisha ya wananchi wa maeneo hayo kibiashara, kiuchumi na kijamii, mara tu mtakapokamilisha majaribio anzeni kutoa huduma ’’. Aliongeza Naibu Waziri ambapo pia alitoa wito kwa watumishi wa TEMESA kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha kivuko hicho pamoja na vivuko vingine vinatunzwa vizuri na vinadumu kwa muda mrefu huku wakizingatia usalama wa abiria na mali zao.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, akisoma taarifa kwa mgeni rasmi katika tukio hilo alisema serikali kupitia TEMESA inaendelea na ujenzi wa vivuko vingine vipya kwa ajili ya Mafia Nyamisati kwa gharama ya shilingi bilioni 5.3, Bugorola Ukara kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 pamoja na Chato Nkome kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1.

‘’Vivuko hivi vyote vinagharimu jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 15.3 na fedha zote hizi zinatolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’, alisema Mhandisi Maselle ambapo aliishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ununuzi wa vivuko, ukarabati na ujenzi wa maegesho ya vivuko, ambapo alisema Fedha hizo zimewezesha miradi hiyo kuanza na mingine kuwepo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Naye Mbunge wa Ilemela Mhe. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula akizungumza katika tukio hilo aliishukuru serikali kwa kuweza kutimiza ahadi iliyoitoa. ‘’Nimshukuru Mhe. Rais niwashukuru TEMESA kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanyika, tunao uhakika sasa kwamba adha ya usafiri katika eneo la visiwa vya Kayenze Bezi sasa litakua ni historia’’, alisema Dkt. Mabula.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella alimuomba Mhe. Nditiye kufikisha salamu za shukrani kwa Rais kwa mambo makubwa anayoufanyia mkoa wa Mwanza hasa kwenye sekta ya usafiri wa majini ambapo alisema watu wa mkoa huo wanategemea mwezi wa pili kuona vivuko  vingine vikiingia ziwani tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Kivuko cha MV.Ilemela kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100. Hadi sasa Wakala unaendesha na kusimamia vivuko 30 katika vituo (Ferry stations) 20 Tanzania Bara na hivyo kukamilika kwa kivuko cha MV. Ilemela kutafanya idadi ya vivuko kufikia 31 na vituo kuwa 21.


Share:

NATO kuangazia upya mpango wa majeshi yake Iraq

MUUNGANO wa kujihami wa NATO unakutana leo kujadili mustakabali wa ujumbe wake wa kutoa mafunzo nchini Iraq wakati ambapo mivutano Mashariki ya Kati inaongezeka baada ya Marekani kumuua jenerali wa ngazi ya juu wa Iran. 

Mabalozi kutoka nchi ishirini na tisa wanachama wa NATO wanatarajiwa kukutana katika makao makuu muungano huo mjini Brussels

Hali imezidi kuwa mbaya nchini Iraq ambapo wabunge wametaka kuondolewa kwa wanajeshi 5,200 wa Marekani walioko nchini humo


Share:

Waziri Ndalichako aamuru kuwekwa ndani mhandisi na mshauri elekezi ujenzi wa VETA Sumbawanga

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameagiza kukamatwa kwa mhandisi wa ujenzi Ding Fubing pamoja na mshauri elekezi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Rukwa Swalehe Kyabega kutokana na kushindwa kukamilisha mradi huo kwa wakati huku wakiendelea kusuasua juu ya ukamilifu wa ujenzi huo ambao ulitakiwa kukamilika 30.12.2019 baada ya kuongezewa siku 100 na hatimae hadi sasa wamefikia asilimia 52 ya ujenzi.

Prof. Ndalichako alisema kuwa kimkataba mkandarasi huyo alitakiwa kuthibitisha kwa risiti matumizi ya shilingi bilioni 1.5 malipo ya awali ya ujenzi kupitia kwa Mshauri elekezi ambae alishindwa kutoa vielelezo vinavyoonesha utekelezaji wa takwa hilo la kisheria na kuongeza kuwa mshauri huyo ameshindwa kusimamia matumizi ya fedha za serikali katika utekelezaji wa mradi huo.

“Mkandarasi aende akakae ndani mpaka vile vifaa mlivyoruhusu viondoke hapa, mpaka vitakaporudi ndio muwaachie, wasababu naona sasa hii inakuwa ni kuchezeana, majibu hamna kitu ambacho kinachoeleweka, utakwenda kukaa sero hadi utakapotoa maelezo ya ufasaha juu ya jambo hili, kwasababu huwezi kucheza na serikali namna hii, mara ya mwisho nilipokja hapa mlikuwa na vifaa kama vyuma chakavu, mmeleta vifaa ahalafu mmeviondoa kuvuipeleka sehemu nyingine, utakaa ndani hadi vifaa hivyo vitakaporudi na uwe na watu wa kutosha kufanya kazi, kwasababu tumechoka tunataka huu ujenzi uishe, wachukue wakae ndani,” Alisisitiza.

Halikadhalika mhandisi huyo alionekana kuwafanyika kazi wafanyakazi wa mradi huo kwa malipo ambayo yapo kinyume na mkataba wa serikali huku baadhi ya watendaji wengine wa sekata ya umeme wakilalamika kufanyishwa kazi bila ya mkataba maalum.

Prof. Ndalichako aliyasema alipotembelea ujenzi wa chuo cha ufundi Stadi VETA katika eneo hilo la Kashai lililopo Manispaa ya Sumbawanga huku akiongozana na watumishi idara ya elimu kutoka halmashauri mbili za wilaya ya Sumbawanga, Mkuu wa Wilaya hiyo, kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na uongozi wa VETA taifa.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini Dkt.Pancras Bujuru alisema kuwa mkandarasi huyo tayari amelipwa shilingi 3,507,174,603 ambayo ni sawa na asilimi 35 ya thamani ya mradi huo na malipo ya mwisho yalikuwa shilingi 330,521,213.79 ambapo alilipwa tarehe 20.12.2019 na kutegemea kuwa baada ya malipo hayo kasi ya ujenzi ingeongezeka lakini haikuwa kama walivyotaraji.

Mh. Waziri kwa hali hii mkandarasi amethibitisha uwezo mdogo kutekeleza mradi huu na hatuna imani kama utatekelezwa kwa wakati kwasababu muda aliopewa na kuongezewa siku 100 vyote vimekwisha nab ado kazi hazijaweza kuisha kwa muda, kwahiyo tunadhani kwamba uwezo wake wa kutekeleza mradi hauturidhishi hata sisi, mshauri elekezi anajukumu la kumsimamia mkandarasi kwa niaba yetu kwasababu tumemuajiri kwa kazi hiyo, tunajua kwamba amekuwa akitoa maelekezo lakini kumekuwa na udhaifu wa kuyasimamia kwa kuchukua hatua zinazostahili na kwa muda muafaka naye tunadhani ana mapungufu,” alisema.

Tarehe 31/8/2019 mkandarasi Tender International alikabidhiwa kiwanja kwaajili ya kuanza ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Manispaa ya Sumbawanga pamoja mshauri Elekezi wa Mradi huo Sky Architect Consultancy Ltd, ambapo mradi huo ulitegemewa kukamillika mwezi Septemba 2019 huku gharama za mradi huo ikiwa shilingi 10,700,488,940.05.


Share:

Mpango:wahasibu Mafisadi Kukiona Cha Moto

Ramadhani Kissimba na Josephine Majura, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.  Dkt. Philip Isdor Mpango, ameiagiza Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wahasibu wote wanaofanya vitendo vinavyokinzana na maadili ya kitaaluma ya uhasibu kama wizi, ubadhirifu wa mali za umma, ufisadi na rushwa.

Dkt. Mpango alitoa maagizo hayo wakati akifungua Kikako Kazi cha kuandaa Hesabu za Majumuisho za Serikali za mwaka 2018/19 pamoja na kuzindua Mfumo mpya wa uandaaji wa taarifa za fedha za Majumuisho (Government Accounting Consolidation System (GACS), Jijini Dar es Salaam

Dkt. Mpango aliwataka wahasibu wote nchini kuwa wazalendo na kusimamia ipasavyo matumizi ya rasimali za Umma na kuwataka kuhakikisha kuwa usalama katika Mifumo ya Fedha unakuwa madhubuti ili kuondoa uwezekano wa mifumo hiyo kudukuliwa na kuleta hasara kubwa kwa Serikali na Wananchi.

Aidha Dk. Mpango alimpongeza Mhasibu Mkuu wa Serikali CPA Francis Mwakapalila, pamoja na Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha Bw. John Sausi kwa kuonesha dhamira na nia ya kweli ya kuhakikisha wanatengeneza Mifumo bora ya kifedha ili kuleta ufanisi mkubwa katika kukusanya na kuhasibu mapato na matumizi ya Serikali.

Aliongeza kuwa dhamira hiyo  imedhihirika kwa kuanzisha Mifumo ya Kifedha ya kimtandao kama Government e-payment Gateway (GePG), Government Salary Payment Platform (GSPP), na sasa Government Accounting Consolidation System (GACS).

‘’Nimefurahi sana kuona kwamba ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, mmeanzisha Mifumo mingi na madhubuti ya kukusanya Mapato na Maduhuli ya Serikali, pamoja na Mifumo ya kuhasibu rasilimali za umma yenye kukidhi viwango vya kimataifa” alisema Dkt. Mpango.

 Aliongeza kuwa ni ushahidi bayana kuwa, watendaji hao wanatafsiri kwa vitendo dhamira na dira ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi shupavu wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  ya kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya Wananchi  hasa Wanyonge.

Pia alieleza kuwa  matarajio ya Serikali ni kwamba mfumo huu ulioanzishwa pamoja na Mifumo iliyokwisha kuanzishwa itaitumika vizuri kwa weledi na uadilifu mkubwa katika kutoa huduma bora kwa Wananchi na ikizingatiwa hilo matarajio ya wananchi na rasimali za umma zitatumika ipasavyo kuboresha Maisha yao.

Awali Mhasibu Mkuu wa Serikali CPA. Fransis Mwakapalila alisema hatua ya kuandaa Hesabu za Majumuisho kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki unaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kutayarisha Hesabu za Majumuisho kwa kutumia mfumo uliandaliwa na wataalamu wake wa ndani kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.

CPA. Mwakapalila alisema kwa sasa Tanzania ni nchi inayoongoza kwa ubora wa Taarifa za FeFha za Majumuisho (CFS) zenye kukidhi viwango vya Kimataifa katika sekta ya Umma (IPSAS) Barani Afrika.

Akizungumza katika kikao kazi hicho Mkurugenzi wa Idara ya Mifumo ya Usimamizi wa fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Sausi, amesema Idara yake itaendelea kujenga mifumo ya kielektroniki ya fedha ili kuhakikisha makusanyo ya pesa za Serikali yanapita katika mifumo sahihi.

“Mafanikio yanayopatikana katika uandaaji wa mifumo hii yanatokana na watalaamu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kuwa na uzalendo wa kuitumikia nchi yao, na wataalamu hao wamekuwa wakiandaa mifumo mbalimbali ukiwemo  mfumo wa kukusanya maduhuli ya Serikali kwa njia ya Mtandao (GePG) ambapo  Taasisi zaidi 616 zimeshaunganishwa kwenye mfumo huo.

Bw.Sausi alisema kuwa mfumo mpya wa uandaaji wa taarifa za fedha za majumuisho (GACS) ambao umezinduliwa na Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango utasaidia kupunguza utiriri wa kuwa na mifumo mingi ya uandaaji wa taarifa za fedha.

Mwisho



Share:

Taarifa Kwa Umma Kuhusu Tuhuma Zinazosambaa Mitandaoni Kwamba Wagonjwa Wengi Wanapoteza Maisha Katika Hospitali Ya Taifa Muhimbili-mloganzila.

Kumekuwa na taarifa kwenye mitandao ya kijamii  ambazo bila kuchanganua zinatuhumu kwamba Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila inasababisha vifo kwa wagonjwa. 

Uongozi wa hospitali unapenda kuwahakikishia Umma wa Watanzania kwamba habari hizi si za kweli na hazitoi picha halisi ya huduma ambazo zinazotolewa hospitalini hapa.
 
Takwimu tulizonazo zinaonyesha kwamba wagonjwa wanaotibiwa MNH- Mloganzila wameongezeka katika makundi yote.  Wagonjwa wa nje wameongezeka kutoka 17,115 katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 kufikia wagonjwa 25,493 katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2019 ambalo ni ongezeko la asilimia 48.8.   

Aidha, wagonjwa wanaotibiwa na kulazwa wameongezeka kutoka 1,459 katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 na kufikia wagonjwa 2,795 katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2019 ambalo ni ongezeko la asilimia 91.6. 
 
Wakati huo huo idadi ya vifo (mortality rate) ikipungua kutoka asilimia 14.9 iliyokuwepo katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 na kufikia asilimia 10.4 katika kipindi cha Julai-Septemba 2019.
 
Aidha, takwimu za MNH-Upanga zinaonyesha kwamba katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba 2018 wagonjwa waliolazwa walikua ni 12,375 ambapo kulitokea vifo 1,000 (mortality rate) ambayo ni asilimia 8.1. 

Vilevile katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2019 MNH Upanga ililaza wagonjwa 17,230 na kati ya hao vifo vilikua 1,673 ambayo ni asilimia 9.7(mortality rate).
 
Hivyo basi takwimu kati ya MNH-Mloganzila na MNH-Upanga za asilimia ya wagonjwa waliofariki hazitofautiani sana ambapo MNH-Upanga ni asilimia 9.7 wakati MNH-Mloganzila ni asilimia 10.4 katika robo ya Julai – Septemba, 2019.  

Hatua hii inaonyesha juhudi ambazo zinafanyika za kuboresha utoaji wa huduma katika MNH- Mloganzila zinazaa matunda.
 
Moja ya sababu ambazo imeelezwa na mtoa taarifa kwamba Madaktari wanaotoa huduma MNH-Mloganzila ni wanafunzi waliopo katika majaribio si za kweli, hivyo tungependa kufafanua kwamba Hospitali ya MNH-Mloganzila ina Madaktari Bingwa 52, Madaktari wa kawaida 50 na kwa sasa ina Madaktari tarajali 53.
 
Licha ya Madaktari Bingwa hawa walioajiriwa MNH-Mloganzila kutoa huduma lakini pia wanashirikiana na Madaktari Bingwa kutoka MNH-Upanga katika kutoa huduma hapa MNH-Mloganzila, vilevile hospitali hii ina madaktari wawili waliobobea wenye hadhi ya Profesa kutoka Korea nao wapo wanatoa huduma.
 
Hivyo sio kweli kwamba madaktari ambao wapo mafunzoni wanafanyakazi bila usimamizi kwani hospitali imeweka utaratibu wa kila mgonjwa anayefika kupata huduma anaonwa na Daktari Bingwa kwa ajili ya maamuzi.
 
Wakati uongozi wa hospitali ukifanyia kazi tuhuma na malalamiko yaliyotolewa juu ya utoaji huduma katika taarifa hii, tunapenda kuutarifu Umma kwamba tangu MNH ipewe dhamana ya kusimamia hospitali hii, tumejielekeza katika kutatua changamoto zilizokuwepo katika utoaji huduma na kwa kiasi kikubwa imeonyesha mafanikio ambayo yanaonyesha kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa na pia kuna ushuhuda wa wagonjwa ambao wametibiwa na kuridhika na utoaji wa huduma zetu.
 
Tunawahakikishia Watanzania kwamba huduma zinazotolewa katika Hospitali ya MNH-Mloganzila zimeboreshwa na tunawakaribisha Watanzania wenye jukumu la kuelimisha jamii waje kuzungumza na wataalam na waone jinsi huduma zinavyotolewa ili waweze kutoa taarifa sahihi kwa jamii.

Imetolewa na
Prof. Lawrence M. Museru
Mkurugenzi Mtendaji,
MNH-Mloganzila.


Share:

Uganda: Bob Wine Akamatwa Tena

Mbunge wa Kyadondo nchini Uganda, Robert Kyagulani, maarufu Bobi Wine, leo Januari 6, 2020, Jeshi la Polisi nchini humo limemkamata na kisha kurusha mabomu ya machozi kwa lengo la kuzuia mkutano wake, uliokuwa umepangwa kufanyika eneo la Gayaza, Kyadondo Mashariki 

Bobi Wine alikamatwa pamoja na wabunge wengine Asuman Basalirwa, Latif Ssebagala,Waiswa Mufumbira na mwenyekiti wa baraza la Kasangati na kwa sasa wanashikiliwa katika kituo cha polisi cha Kasangati.

Gazeti la The Observer limemnukuu Basalirwa akisema walikuwa wakiendesha gari la Kyagulanyi kabla ya polisi kuwazuia katika eneo la Kasangati na kuwapeleka katika kituo cha polisi. Kyagulanyi alikuwa akitarajiwa kuzindua mikutano ya mashauriano kuhusu malengo ya urais kwa uchaguzi mkuu ujao.

Polisi wamedai kuwa ilibidi kuuzuia mkutano huo kwa sababu ulipangwa kufanyika kwenye eneo la wazi, wakati mikutano ya namna hiyo hufanyika ndani ili kutoingilia shughuli za watu wengine.

Pia polisi wamedai kuwa hakukuwa na vyoo vya kutosha kwa ajili ya wageni waliokuwa wakitarajiwa.

Mbunge huyo aliiandikia tume ya uchaguzi kabla ya krisimasi akieleza nia yake ya kufanya mkutano kitaifa kuhusu nia ya kuwania urais. Ingawa alitoa taarifa kwa tume hiyo, ambayo ilimruhusu, imesema hakutimiza vigezo vingine kama vinavyoelezwa kwenye sheria.

Bobi Wine ameeleza nia yake ya kuwanida urais dhidi ya rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.


Share:

Tanasha Donna avunja kimya kuhusiana na madai ya Diamond Kuwa na Mpenzi Mwingine

Mpenzi Mkenya wa msanii Diamond Platinumz, Tanasha Donna hatimaye amevunja kimya chake baada ya kuibuka kwa maneno kuwa mwanamuziki huyo ana uhusiano wa pembeni.

Diamond anadaiwa kuwa katika uhusiano mwingine na mrembo wa Tanzania yapata miezi sita tu baada ya kumkaribisha mwanawe wa kiume Naseeb Junior.

Mama huyo wa mtoto mmoja kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliwaomba watu kukoma kueneza habari ambazo macho yao hayajashuhudia kwa kutumia mdomo.

Ni bayana kuwa mrembo huyo alikuwa anajibu madai kuwa mpenziwe ana uhusiano na mwanadada kwa jina Rose.

Katika hali ya kuzima fununu kuhusu uhusiano wake, mtangazaji huyo wa radio ya NRG alisema mapenzi yake na Diamond hayawezi kuvunjika.

Donna alichapisha picha yake na Diamond katika hali ya mahaba na kuonyesha kuwa hawawezi kutengana hivi karibuni.


Share:

Watu wasiojulikana waiba vifaa vya NIDA Arusha

Watu wasiojulikana wameiba mashine zote za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) zilizokuwa katika kituo kidogo cha NIDA katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha usiku wa kuamkia leo, kituo hicho kimefungwa kwa leo na Polisi wameanza mchakato wa kuwasaka waliohusika na wizi huo.

Mkuu wa wilaya Arumeru, Jerry Muro amesema wizi huo umetokea usiku wa kuamkia leo Jumatatu Januari 6, 2020 katika ofisi za Nida zilizopo jengo la halmashauri ya Wilaya ya Arusha (DC).

Muro amesema vifaa vilivyoibwa ni kamera mbili, stendi mbili, kompyuta mpakato mbili, kompyuta moja (Desk top), stendi mbili, Extation mbili, keyboad moja na Damalog moja.

"Vifaa vyote vimeibiwa, tumepata mshtuko, milango haikuvunjwa inaonekana ni wizi wa kimkakati umefanywa ndani, vifaa vya NIDA ni mali za Taifa sasa hawa wanapata wapi ujasiri wa kuiba!"- Jerry Muro, Mkuu wa Wilaya Arumeru


Share:

Trump atishia kuiwekea Iraq vikwazo Kama Itawafukuza Wanajeshi wa Marekani Nchini Humo

Rais wa Marekani, Donald Trump, ametishia kuiwekea Iraq vikwazo baada ya bunge la nchi hiyo kupiga kura kupitisha azimio linalovitaka vikosi vya Marekani viondoke nchini humo. 

Trump amesema iwapo wanajeshi hao wataondoka, Iraq itapaswa kuilipa Marekani gharama za kambi ya jeshi la anga iliyoko Iraq. 

Trump amebainisha kuwa hawatoondoka hadi hapo Iraq itakapoilipa Marekani gharama za kambi hiyo ambayo amesema iko muda mrefu hata kabla ya wakati wake na iligharimu mabilioni ya dola kuijenga.

 Trump amesema kama Iraq itavitaka vikosi vya Marekani kuondoka na suala hilo kufanyika katika njia isiyokuwa na misingi ya kirafiki, basi nchi yake itaweka vikwazo vikali kwa Iraq ambavyo haijawahi kushuhudia.

 Wakati huo huo, Ikulu ya Marekani imesema kuwa Trump amezungumza na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson kuhusu hali inayoendelea nchini Iraq na Iran.

Soma hii: Ajira Mpya 250+ zilizotangazwa wiki hii

Mvutano bado ni mkubwa baada ya Marekani kuusika kumuua kiongozi wa jeshi wa Marekani jenerali Qasem Soleimani huko Baghdad wiki iliyopita.

Soleimani ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 62, alikuwa akiongoza operesheni za vita katika nchi za mashariki ya kati

Kiongozi mpya wa kikosi cha jeshi la Iran la Quds - ambacho Soleimani aliongoza - ameapa kuwaondoa Wamarekani katika mataifa ya mashariki ya kati.


Share:

Iran yasitisha utekelezaji wa makubaliano wa Nyuklia ya Mwaka 2015

Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo Jumatatu imetoa taarifa ikitangaza kuwa imechukua hatua ya tano na ya mwisho ya kupunguza utekelezaji wa ahadi zake katika makubaliano ya nyuklia maarufu kwa kifupi kama JCPOA.

Taarifa hiyo imesema kuwa, kuanzia sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakuwa na kizuizi chochote katika shughuli zake za nyuklia ikiwa ni pamoja na kurutubisha madini ya urani, asilimia ya urutubishaji wa madini hayo, kiwango kinachorutubishwa na katika masuala ya utafiti na uchunguzi.

Kwa msingi huo katika hatua hii ya tano, Iran imetupilia mbali kizuizi muhimu zaidi cha shughuli zake kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambacho kinahusiana na idadi ya mashinepewa zinazoruhusiwa kufanya kazi.

Iran imesema katika taarifa hiyo kwamba, tokea sasa miradi yake ya kuzalisha nishati ya nyuklia itafanya kazi kwa mujibu wa mahitaji yake ya kiufundi. 

Imesisitiza kuwa, Iran itaendelea kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kwamba iwapo vikwazo vyote vitaondolewa na Tehran ikafaidika na maslahi ya JCPOA,  iko tayari kutekeleza tena vipengee vya makubaliano hayo.


Share:

Serikali Kufuta Vyama 3,436 Vya Ushirika

Serikali  inakusudia kuvifuta vyama vya ushirika vipatavyo 3,436 ambavyo vimeshindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi na havipatikani huku vingine vikiwa havijulikani vilipo.

Kwa kuzingatia matakwa ya sheria no 6 ya mwaka 2013 ya vyama vya ushirika kifungu 100 na kanuni ya 26, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amemuagiza Mrajisi wa vyama hivyo kutoa notisi ya siku 90 kwenye gazeti la serikali ya kusudio la kuvifuta.

Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma jana, Mhe Hasunga amesema asilimia kubwa ya vyama vilivyokusudiwa kufutwa ni vyama vya ushirika wa akiba na mikopo ambavyo ni asilimia 73.8.

Amesema vyama hivyo vingi ni matokeo ya mfumo wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ujulikanao kama Jakaya Kikwete Fund ambao ulilenga kuwawezesha wananchi kiuchumi.

" Katika mpango huu wa JK Fund wananchi wengi walianzisha SACCOS kwa lengo la kupata mikopo kutoka kwenye mfuko huo, Aidha vyama ambavyo havikupata mkopo havikuendelea na majukumu yake na hata vilivyopata mikopo baada ya kupata walitelekeza vyama hivyo jambo linalopelekea kuwa na SACCOS nyingi hewa," Amesema Mhe Hasunga.

Amevitaka vyama ambavyo orodha yake itapatikana kwenye tangazo la mrajisi litakalotolewa kwenye gazeti la serikali, mtandao wa wizara ya kilimo na mtandao wa Tume ya Ushirika kujitokeza na kutoa sababu za kwanini wasifutwe kwenye orodha ya vyama vya ushirika.

" Tunavitaka vyama vyote vya ushirika nchini kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Vyama vyote vinatakiwa kuwahudumia wanachama wake na siyo vinginevyo," Amesema Mhe Hasunga.

Mhe Waziri amesema mpaka sasa daftari la mrajisi wa vyama vya ushirika lina jumla ya vyama 11,149 vilivyoandikishwa kati ya vyama hivyo, 3,436 havijulikani vilipo, vyama 1,250 vimesinzia na vyama 6,463 vipo hai.

Amesema sababu zinazopelekea kufutwa kwa vyama hivyo ni kushindwa kuwa na ofisi huku viongozi wake wakiwa hawajulikani, Chama kushindwa kufanya shughuli zake ndani ya miezi sita tangu kiandikishwe pamoja na idadi ya wanachama kupungua kwa mujibu wa mahitaji ya kisheria.

Sababu nyingine ni vyama hivyo kushindwa kutekeleza takwa la kisheria la kutayarisha makisio ya mapato na matumizi na kuyapeleka kwa mrajisi kuyapitisha, kutayarisha taarifa ya mwaka, kufunga mahesabu na kuyapeleka COASCO kwa ukaguzi, kutofanya mikutano ya mwaka ya wanachama na bodi zao.

Katika orodha ya vyama vya ushirika kimkoa vinavyokusudiwa kufutwa kwenye daftari la mrajisi wa vyama, Mkoa wa Mwanza unaongoza ukiwa na jumla ya vyama 393, Pwani ya pili yenye vyama 335 huku Kagera ikishika nafasi ya tatu kwa vyama 301.

Kwa upande wake Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk Benson Ndiegi amesema serikali haitowavumilia viongozi wa vyama ambavyo vitakaidi maagizo hayo yaliyotolewa na Mhe Waziri.

" Baada ya agizo hili la Mhe Waziri na baada ya kutoa notisi hizo kwenye gazeti la serikali tutakua tayari kupokea maelezo na taarifa kutoka kwenye vyama na wale ambao watakua wanafutwa waje na wanaamini wana nafasi ya kuendelea kuwepo inabidi waje na vielelezo vyao," Amesema Dk Ndiegi


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger